Isa akamilisha huduma yake
11
(Yohana 11:1–13:30)
Kifo cha Lazaro
Basi mtu mmoja, jina lake Lazaro, alikuwa mgonjwa. Yeye alikuwa akiishi Bethania, kijiji cha Mariamu na Martha dada yake. (Huyu Mariamu, ambaye Lazaro kaka yake alikuwa mgonjwa, ndiye alimpaka Bwana Isa mafuta na kuifuta miguu yake kwa nywele zake.) Hivyo hawa dada wawili walituma ujumbe kwa Isa kumwambia, “Bwana, yule umpendaye ni mgonjwa.”
Lakini Isa aliposikia hayo, akasema, “Ugonjwa huu hautaleta mauti, bali ni wa kudhihirisha utukufu wa Mungu, ili Mwana wa Mungu apate kutukuzwa kutokana na ugonjwa huu.” Isa aliwapenda Martha, Mariamu na Lazaro ndugu yao. Hata hivyo, baada ya kusikia kwamba Lazaro ni mgonjwa, alikawia huko alikokuwa kwa siku mbili zaidi.
Ndipo akawaambia wanafunzi wake, “Haya, turudi Yudea.”
Wanafunzi wake wakamwambia, “Mwalimu, Wayahudi walikuwa wanataka kukupiga mawe, nawe unataka kurudi huko?”
Isa akawajibu, “Si kuna saa kumi na mbili za mchana katika siku moja? Wanaotembea mchana hawawezi kujikwaa, kwa maana wanaona kwa nuru ya ulimwengu huu. 10 Lakini wale wanaotembea usiku hujikwaa kwa sababu hawana nuru ndani yao.”
11 Baada ya kusema haya, Isa akawaambia, “Rafiki yetu Lazaro amelala, lakini naenda kumwamsha.”
12 Wanafunzi wakamwambia, “Bwana, kama amelala usingizi ataamka.” 13 Hata hivyo, Isa alikuwa anazungumzia kuwa Lazaro amekufa, lakini wanafunzi wake hawakuelewa, walidhani kwamba anasema Lazaro amelala usingizi tu.
14 Kwa hiyo Isa akawaambia waziwazi, “Lazaro amekufa. 15 Hata hivyo nafurahi kwa kuwa sikuwako huko kabla ya Lazaro kufa, ili mpate kuamini. Lakini sasa twendeni kwake.”
16 Tomaso (aliyeitwa Pacha) akawaambia wanafunzi wenzake, “Sisi nasi twendeni tukafe pamoja naye.”
Isa ndiye ufufuo na uzima
17 Isa alipowasili huko alikuta Lazaro amekuwa kaburini siku nne. 18 Basi Bethania ulikuwa karibu na Yerusalemu, umbali wa yamkini maili mbili*kama kilomita 3, 19 na Wayahudi wengi walikuwa wamekuja kuwafariji Martha na Mariamu kwa ajili ya kufiwa na ndugu yao. 20 Martha aliposikia kwamba Isa anakuja, alitoka kwenda kumlaki, ila Mariamu alibaki nyumbani.
21 Martha akamwambia Isa, “Bwana, kama ungekuwa hapa, ndugu yangu hangekufa. 22 Lakini sasa ninajua kuwa chochote utakachomwomba Mungu, atakupa.”
23 Isa akamwambia, “Ndugu yako atafufuka.”
24 Martha akamjibu, “Ninajua ya kuwa atafufuka wakati wa ufufuo wa wafu siku ya mwisho.”
25 Isa akamwambia, “Mimi ndiye huo ufufuo na uzima. Yeye aniaminiye mimi, hata akifa atakuwa anaishi; 26 na yeyote aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je, unasadiki haya?”
27 Martha akamwambia, “Ndiyo Bwana, ninaamini ya kuwa wewe ndiwe Al-MasihiAl-Masihi maana yake Aliyetiwa mafuta., Mwana wa Mungu, yeye ajaye ulimwenguni.”
Isa alia
28 Baada ya kusema haya, Martha alienda akamwita Mariamu dada yake faraghani na kumwambia, “Mwalimu yuko hapa anakuita.” 29 Mariamu aliposikia hivyo, akaondoka upesi, akaenda hadi alipokuwa Isa. 30 Isa alikuwa hajaingia kijijini, bali alikuwa bado yuko mahali pale alipokutana na Martha. 31 Wale Wayahudi waliokuwa pamoja na Mariamu nyumbani wakimfariji walipoona ameondoka haraka na kutoka nje, walimfuata wakidhani kwamba alikuwa anaenda kule kaburini kulilia huko.
32 Mariamu alipofika mahali pale Isa alipokuwa, alipiga magoti miguuni pake na kusema, “Bwana, kama ungekuwa hapa, ndugu yangu hangekufa.”
33 Isa alipomwona Mariamu akilia na wale Wayahudi waliokuja pamoja naye pia wakilia, Isa alisikia uchungu moyoni, akafadhaika sana. 34 Akauliza, “Mmemweka wapi?”
Wakamwambia, “Bwana, njoo upaone.”
35 Isa akalia machozi.
36 Ndipo Wayahudi wakasema, “Tazama jinsi alivyompenda Lazaro!”
37 Lakini wengine wakasema, “Je, yule aliyefungua macho ya kipofu, hakuweza kumfanya na huyu asife?”
Isa amfufua Lazaro
38 Isa akafika penye kaburi akiwa amefadhaika sana kwa mara nyingine. Hilo kaburi lilikuwa pango ambalo jiwe liliwekwa kwenye ingilio lake. 39 Isa akasema, “Liondoeni jiwe.”
Martha dada yake yule aliyekuwa amekufa akasema, “Lakini Bwana, wakati huu atakuwa ananuka kwani amekwisha kuwa kaburini siku nne.”
40 Isa akamwambia, “Sikukuambia kwamba ukiamini utauona utukufu wa Mungu?”
41 Kwa hiyo wakaliondoa lile jiwe kutoka kaburini. Isa akainua macho yake juu, akasema, “BabaJina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu., ninakushukuru kwa kuwa wanisikia. 42 Ninajua ya kuwa wewe hunisikia siku zote, lakini nimesema haya kwa ajili ya watu hawa waliosimama hapa, ili wapate kuamini ya kuwa wewe umenituma.”
43 Baada ya kusema haya, Isa akapaza sauti yake, akaita, “Lazaro, njoo huku!” 44 Yule aliyekuwa amekufa akatoka nje, mikono yake na miguu yake ikiwa imeviringishiwa vitambaa vya kitani na leso usoni pake.
Isa akawaambia, “Mfungueni; mwacheni aende zake.”
Njama ya kumuua Isa
(Mathayo 26:1-5; Marko 14:1-2; Luka 22:1-2)
45 Hivyo Wayahudi wengi waliokuwa wamekuja kumfariji Mariamu walipoona yale Isa aliyoyatenda, wakamwamini. 46 Lakini baadhi yao wakaenda kwa Mafarisayo§Kundi la kidini la Wayahudi; walifuata Torati kwa dhati, hasa maagizo kuhusu utakaso. Pia waliamini katika malaika, ufufuo wa wafu, na kuja kwa Masihi ambaye atarejesha ufalme wa Daudi na ukuu wa taifa la Israeli. na kuwaambia mambo Isa aliyoyafanya. 47 Kwa hiyo viongozi wa makuhani na Mafarisayo wakaita mkutano wa Baraza la Wayahudi*Baraza la Wayahudi ina maana ya Sanhedrin ambalo lilikuwa baraza la juu kabisa la utawala wa Kiyahudi; liliundwa na wazee 70 pamoja na kuhani mkuu..
Wakaulizana, “Tufanyeje? Huyu mtu anafanya ishara nyingi. 48 Tukimwacha aendelee hivi, kila mtu atamwamini, nao Warumi watakuja na kupaharibu mahali petu patakatifu na taifa letu.”
49 Mmoja wao aliyeitwa Kayafa, aliyekuwa kuhani mkuu mwaka huo, akasema, “Ninyi hamjui kitu chochote! 50 Hamjui kwamba ni afadhali mtu mmoja afe kwa ajili ya watu, kuliko taifa lote liangamie?”
51 Hakusema haya kutokana na mawazo yake mwenyewe, bali kama kuhani mkuu mwaka huo, alitabiri kuwa Isa angekufa kwa ajili ya taifa la Wayahudi; 52 wala si kwa ajili ya taifa hilo pekee, bali pia kwa ajili ya watoto wa Mungu waliotawanyika, ili kuwaleta pamoja na kuwafanya wawe wamoja. 53 Hivyo tangu siku hiyo wakawa wanafanya mipango ili wamuue Isa.
54 Kwa hiyo Isa akawa hatembei tena hadharani miongoni mwa Wayahudi, bali alijitenga akaenda sehemu iliyo karibu na jangwa kwenye kijiji kiitwacho Efraimu. Akakaa huko na wanafunzi wake.
55 Basi Pasaka ya Wayahudi ilipokuwa imekaribia, watu wengi walitoka vijijini wakaenda Yerusalemu ili wakajitakase kabla ya Pasaka. 56 Watu wakawa wanamtafuta Isa, nao waliposimama kwenye ua la Hekalu, waliulizana, “Je, mtu huyu hatakuja kamwe kwenye Sikukuu?” 57 Viongozi wa makuhani na Mafarisayo walikuwa wametoa amri kuwa yeyote atakayejua mahali Isa aliko, lazima atoe taarifa ili wapate kumkamata.

*11:18 kama kilomita 3

11:27 Al-Masihi maana yake Aliyetiwa mafuta.

11:41 Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu.

§11:46 Kundi la kidini la Wayahudi; walifuata Torati kwa dhati, hasa maagizo kuhusu utakaso. Pia waliamini katika malaika, ufufuo wa wafu, na kuja kwa Masihi ambaye atarejesha ufalme wa Daudi na ukuu wa taifa la Israeli.

*11:47 Baraza la Wayahudi ina maana ya Sanhedrin ambalo lilikuwa baraza la juu kabisa la utawala wa Kiyahudi; liliundwa na wazee 70 pamoja na kuhani mkuu.