12
Mariamu ampaka Isa mafuta huko Bethania
(Mathayo 26:6-13; Marko 14:3-9; Luka 7:35-38)
1 Siku sita kabla ya Pasaka, Isa alienda Bethania, makao ya Lazaro, aliyekuwa amemfufua kutoka kwa wafu. 2 Wakaandaa karamu kwa heshima ya Isa. Martha akawahudumia, wakati Lazaro alikuwa miongoni mwa waliokaa mezani pamoja na Isa. 3 Kisha Mariamu akachukua chupa ya painti moja*painti moja ni kama nusu lita yenye manukato ya nardo†aina ya mafuta yaliyokuwa yanatengenezwa kutokana na mimea yenye mizizi inayotoa harufu nzuri safi ya thamani kubwa, akayamimina miguuni mwa Isa na kuifuta kwa nywele zake. Nyumba nzima ikajaa harufu nzuri ya manukato.
4 Ndipo Yuda Iskariote mwana wa Simoni, mmoja wa wanafunzi wa Isa, ambaye baadaye angemsaliti Isa, akasema, 5 “Kwa nini manukato haya hayakuuzwa kwa dinari mia tatu‡Dinari 300 ni sawa na mshahara wa kibarua wa siku 300., na fedha hizo wakapewa maskini?” 6 Yuda hakusema hivi kwa kuwa aliwajali maskini, bali kwa kuwa alikuwa mwizi; ndiye alikuwa akitunza mfuko wa fedha, na akawa akiiba zile fedha.
7 Isa akasema, “Mwacheni. Aliyanunua manukato hayo ili ayaweke kwa ajili ya siku ya maziko yangu. 8 Maskini mtakuwa nao siku zote, lakini mimi hamtakuwa nami siku zote.”
Njama ya kumuua Lazaro
9 Umati mkubwa wa Wayahudi walipojua kwamba Isa alikuwa huko Bethania, walikuja si tu kwa ajili ya Isa, lakini pia kumwona Lazaro ambaye Isa alikuwa amemfufua. 10 Kwa hiyo viongozi wa makuhani wakapanga njama ya kumuua Lazaro pia, 11 kwa kuwa kutokana na habari za kufufuliwa kwake, Wayahudi wengi walikuwa wanamfuata Isa na kumwamini.
Isa aingia Yerusalemu kwa shangwe
(Mathayo 21:1-11; Marko 1:1-11; Luka 19:28-40)
12 Siku iliyofuata umati mkubwa wa watu waliokuwa wamekuja kwenye Sikukuu walisikia kwamba Isa angekuja Yerusalemu. 13 Basi wakachukua matawi ya mitende, wakatoka kwenda kumlaki, huku wakipaza sauti wakisema,
“Amebarikiwa yeye ajaye kwa Jina la Mwenyezi Mungu!”
“Amebarikiwa mfalme wa Israeli!”
14 Isa akamkuta mwana-punda, akampanda, kama ilivyoandikwa,
15 “Usiogope, ewe Binti Sayuni;
tazama, mfalme wako anakuja,
amepanda mwana-punda!”
16 Wanafunzi wake Isa mwanzoni hawakuelewa mambo haya. Lakini Isa alipotukuzwa, ndipo walipokumbuka kuwa mambo haya yalikuwa yameandikwa kwa ajili yake na alitendewa yeye.
17 Wale waliokuwepo Isa alipomwita Lazaro kutoka kaburini na kumfufua kutoka kwa wafu waliendelea kushuhudia. 18 Na kwa sababu walikuwa wamesikia kwamba alikuwa ametenda muujiza huu, umati wa watu wakaenda kumlaki. 19 Hivyo Mafarisayo*Kundi la kidini la Wayahudi; walifuata Torati kwa dhati, hasa maagizo kuhusu utakaso. Pia waliamini katika malaika, ufufuo wa wafu, na kuja kwa Masihi ambaye atarejesha ufalme wa Daudi na ukuu wa taifa la Israeli. walipoona hayo, wakaambiana, “Mnaona, hamwezi kufanya lolote. Angalieni, ulimwengu wote unamfuata yeye!”
Isa atabiri kifo chake
20 Basi palikuwa Wayunani fulani miongoni mwa wale waliokuwa wameenda kuabudu wakati wa Sikukuu. 21 Hawa wakaenda kwa Filipo, aliyekuwa raia wa Bethsaida huko Galilaya, wakiwa na ombi. Wakamwambia, “Tungependa kumwona Isa.” 22 Filipo akaenda akamweleza Andrea, nao wote wawili wakamwambia Isa.
23 Isa akawajibu, “Saa imewadia ya Mwana wa Adamu kutukuzwa. 24 Amin, amin nawaambia, mbegu ya ngano isipoanguka ardhini na kufa, hubakia kama mbegu peke yake. Lakini ikifa, huzaa mbegu nyingi. 25 Mtu yeyote anayependa maisha yake atayapoteza, naye ayachukiaye maisha yake katika ulimwengu huu atayaokoa hata kwa uzima wa milele. 26 Mtu yeyote akinitumikia lazima anifuate, nami mahali nilipo ndipo mtumishi wangu atakapokuwa. Mtu akinitumikia, Baba yangu atamheshimu.
27 “Sasa roho yangu imefadhaika sana. Niseme nini? ‘Baba, niokoe katika saa hii’? Lakini ni kwa kusudi hili nimeufikia wakati huu. 28 Baba, litukuze jina lako.”
Ndipo ikaja sauti kutoka mbinguni, ikasema, “Nimelitukuza, nami nitalitukuza tena.” 29 Umati ule wa watu waliokuwa mahali pale waliisikia ile sauti, nao wakasema hiyo ilikuwa sauti ya radi; wengine wakasema malaika ameongea naye.
30 Isa akawaambia, “Sauti hii imesikika kwa faida yenu, wala si kwa faida yangu. 31 Sasa ni saa ya hukumu kwa ajili ya ulimwengu huu, sasa mkuu wa ulimwengu huu atatupwa nje. 32 Lakini mimi, nikiinuliwa kutoka nchi, nitawavuta watu wote waje kwangu.” 33 Isa aliyasema haya akionesha ni kifo gani atakachokufa.
34 Umati ule wa watu wakapaza sauti, wakasema, “Tumesikia kutoka Torati kwamba Al-Masihi†Al-Masihi maana yake Aliyetiwa mafuta. adumu milele; hivyo wewe wawezaje kusema, ‘Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa juu’? Huyu ‘Mwana wa Adamu’ ni nani?”
35 Ndipo Isa akawaambia, “Bado kitambo kidogo nuru ingali pamoja nanyi. Nendeni maadamu mna nuru, msije mkakumbwa na giza. Mtu anayetembea gizani hajui anakoenda. 36 Wekeni tumaini lenu katika nuru hiyo ili mpate kuwa wana wa nuru.” Baada ya kusema haya, Isa aliondoka, akajificha wasimwone.
Wayahudi waendelea kutokuamini
37 Hata baada ya Isa kufanya miujiza hii yote mbele yao, bado hawakumwamini. 38 Hili lilikuwa ili kutimiza lile neno la nabii Isaya lililosema:
“Mwenyezi Mungu, ni nani aliyeamini ujumbe wetu,
na mkono wa Mwenyezi Mungu umefunuliwa kwa nani?”
39 Kwa hivyo hawakuamini, kwa sababu Isaya anasema mahali pengine:
40 “Amewafanya vipofu,
na kuifanya mioyo yao kuwa migumu,
ili wasiweze kuona kwa macho yao,
wala kuelewa kwa mioyo yao,
wasije wakageuka nami nikawaponya.”
41 Isaya alisema haya alipoona utukufu wa Isa na kunena habari zake.
42 Lakini wengi miongoni mwa viongozi wa Wayahudi walimwamini, lakini kwa sababu ya Mafarisayo hawakukiri waziwazi kwa maana waliogopa kufukuzwa katika masinagogi.‡Nyumba za ibada na mafunzo. 43 Wao walipenda sifa za wanadamu kuliko sifa zinazotoka kwa Mungu.
Amwaminiye Isa hatabaki gizani
44 Isa akapaza sauti akasema, “Yeyote aniaminiye, haniamini mimi peke yangu, bali pia yeye aliyenituma. 45 Yeyote anionaye mimi amemwona yeye aliyenituma. 46 Mimi nimekuja kama nuru ulimwenguni, ili kila mtu aniaminiye asibaki gizani.
47 “Mimi simhukumu mtu yeyote anayesikia maneno yangu na asiyatii, kwa maana sikuja kuuhukumu ulimwengu, bali kuuokoa. 48 Yuko anayehukumu yule anayenikataa mimi na kuyakataa maneno yangu; yale maneno niliyoyasema yenyewe yatamhukumu siku ya mwisho. 49 Kwa maana sisemi kwa ajili yangu mwenyewe, bali Baba aliyenituma aliniamuru ni nini cha kusema na jinsi ya kukisema. 50 Nami ninajua amri zake huongoza hadi kwenye uzima wa milele. Hivyo lolote nisemalo, ndilo lile Baba aliloniambia niseme.”
*12:3 painti moja ni kama nusu lita
†12:3 aina ya mafuta yaliyokuwa yanatengenezwa kutokana na mimea yenye mizizi inayotoa harufu nzuri
‡12:5 Dinari 300 ni sawa na mshahara wa kibarua wa siku 300.
§12:13 Kiebrania kusema Okoa; basi likawa neno la shangwe.
*12:19 Kundi la kidini la Wayahudi; walifuata Torati kwa dhati, hasa maagizo kuhusu utakaso. Pia waliamini katika malaika, ufufuo wa wafu, na kuja kwa Masihi ambaye atarejesha ufalme wa Daudi na ukuu wa taifa la Israeli.
†12:34 Al-Masihi maana yake Aliyetiwa mafuta.
‡12:42 Nyumba za ibada na mafunzo.