9
Udanganyifu wa Wagibeoni
1 Basi ikawa wafalme wote waliokuwa magharibi mwa Yordani waliposikia haya yote, na wale waliokuwa katika nchi ya vilima, na katika Shefela*au upande wa magharibi chini ya vilima, na katika pwani yote ya Bahari Kuu†yaani Bahari ya Mediterania hadi kufikia Lebanoni (wafalme wa Wahiti, Waamori, Wakanaani, Waperizi, Wahivi na Wayebusi), 2 waliungana ili kupigana vita dhidi ya Yoshua na Israeli.
3 Hata hivyo, watu wa Gibeoni waliposikia kuhusu yote Yoshua aliyowatendea watu wa Yeriko na Ai, 4 waliamua kufanya hila: Wakajifanya kama wajumbe wakiwa na punda waliobebeshwa mizigo ya magunia yaliyochakaa, na viriba vikuukuu vya mvinyo, vyenye nyufa zilizozibwa. 5 Walivaa miguuni mwao viatu vilivyoraruka na kushonwa, kisha wakavaa nguo kuukuu. Chakula chao kilikuwa mkate uliokauka na kuingia koga. 6 Ndipo wakamwendea Yoshua kambini huko Gilgali, wakamwambia yeye pamoja na Waisraeli, “Tumetoka katika nchi ya mbali; fanyeni mkataba nasi.”
7 Basi Waisraeli wakawaambia hao Wahivi, “Lakini huenda mnakaa karibu nasi. Twawezaje basi kufanya mkataba nanyi?”
8 Wakamwambia Yoshua, “Sisi ni watumishi wako.”
Yoshua akawauliza, “Ninyi ni nani, na mnatoka wapi?”
9 Nao wakamjibu: “Watumishi wako wametoka nchi ya mbali sana kwa ajili ya umaarufu wa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu. Kwa kuwa tumesikia taarifa zake: hayo yote aliyofanya huko Misri, 10 pia yale yote aliyowatendea wafalme wawili wa Waamori mashariki mwa Yordani; huyo Sihoni mfalme wa Heshboni na Ogu mfalme wa Bashani, aliyetawala huko Ashtarothi. 11 Basi wazee wetu na wale wote wanaoishi katika nchi yetu walituambia, ‘Chukueni chakula cha safari; nendeni mkakutane na watu hao na kuwaambia, “Sisi tu watumishi wenu, fanyeni mapatano nasi.” ’ 12 Mkate huu wetu ulikuwa wa moto tulipoufunga siku tulipoanza safari kuja kwenu, lakini sasa angalia jinsi ulivyokauka na kuota ukungu. 13 Viriba hivi vya mvinyo vilikuwa vipya tulipovijaza, lakini ona jinsi vilivyo na nyufa. Nguo zetu na viatu vimechakaa kwa ajili ya safari ndefu.”
14 Basi Waisraeli wakavikagua vyakula vyao bila kupata shauri kutoka kwa Mwenyezi Mungu. 15 Ndipo Yoshua akafanya nao mkataba wa amani ili kuwaacha waishi, na viongozi wa kusanyiko wakauthibitisha kwa kiapo.
16 Siku ya tatu baada ya kufanya mkataba na Wagibeoni, Waisraeli wakapata habari kuwa watu hao ni majirani zao, walioishi karibu nao. 17 Ndipo Waisraeli wakasafiri, na siku ya tatu wakafika kwenye miji yao: yaani Gibeoni, Kefira, Beerothi na Kiriath-Yearimu. 18 Lakini Waisraeli hawakuwashambulia kwa kuwa viongozi wa kusanyiko walikuwa wamewaapia kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli.
Kusanyiko lote wakanung’unika dhidi ya hao viongozi, 19 lakini viongozi wote wakawajibu, “Tumeshawaapia kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, kwa hiyo hatuwezi kuwagusa sasa. 20 Hivi ndivyo tutakavyowafanyia: Tutawaacha waishi, ili ghadhabu isije juu yetu kwa kuvunja kiapo tulichowaapia.” 21 Wakaendelea kusema, “Waacheni waishi, lakini wawe wapasua kuni na wachota maji kwa ajili ya jamii yote.” Hivyo ahadi waliyoweka viongozi kwao ikawa hivyo.
22 Kisha Yoshua akawaita Wagibeoni na kuwaambia, “Kwa nini mmetudanganya kwa kutuambia, ‘Tunaishi mbali nanyi,’ ilhali mnaishi karibu nasi? 23 Sasa mko chini ya laana: Daima mtakuwa wapasua kuni na wachota maji kwa ajili ya nyumba ya Mungu wangu.”
24 Wakamjibu Yoshua, “Watumwa wako waliambiwa waziwazi jinsi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, alivyomwamuru mtumishi wake Musa kuwapa ninyi nchi hii yote na kuwaangamiza wakazi wake wote toka mbele zenu. Kwa hiyo tuliogopa mno kwa ajili ya uhai wetu kwa sababu yenu, ndiyo maana tukafanya neno hili. 25 Sasa tupo mikononi mwako. Tufanyieni lolote mnaloona kuwa jema na haki kwenu.”
26 Kwa hiyo Yoshua akawaokoa mikononi mwa Waisraeli, nao hawakuwaua. 27 Siku hiyo Yoshua akawafanya Wagibeoni wapasua kuni na wachota maji kwa ajili ya jamii na kwa ajili ya madhabahu ya Mwenyezi Mungu mahali pale Mwenyezi Mungu angepachagua. Hivyo ndivyo walivyo hadi hivi leo.