10
Jua lasimama
1 Baada ya haya Adoni-Sedeki mfalme wa Yerusalemu alisikia kuwa Yoshua alikuwa ameteka mji wa Ai na kuuangamiza kabisa, tena alikuwa ameua mfalme wake, kama alivyofanya huko Yeriko na mfalme wake, tena ya kuwa watu wa Gibeoni walikuwa wamefanya mapatano ya amani na Waisraeli, na walikuwa wakiishi karibu yao. 2 Yeye na watu wake wakataharuki mno kwa kuwa Gibeoni ulikuwa mji mkubwa kama mmoja wa miji ya kifalme; ulikuwa mkubwa kuliko Ai, na watu wake wote walikuwa mashujaa wa vita. 3 Hivyo Adoni-Sedeki mfalme wa Yerusalemu akaomba msaada kwa Hohamu mfalme wa Hebroni, Piramu mfalme wa Yarmuthi, Yafia mfalme wa Lakishi, na Debiri mfalme wa Egloni. 4 Akawaambia, “Njooni mnisaidie kuipiga Gibeoni, kwa sababu imefanya mkataba wa amani na Yoshua na Waisraeli.”
5 Ndipo hao wafalme watano wa Waamori, ambao ni wafalme wa Yerusalemu, Hebroni, Yarmuthi, Lakishi na Egloni, wakaunganisha majeshi yao. Wakapanda na vikosi vyao vyote, nao wakajipanga dhidi ya Gibeoni na kuishambulia.
6 Nao Wagibeoni wakatuma ujumbe kwa Yoshua kwenye kambi ya Gilgali na kumwambia, “Usiwatelekeze watumishi wako. Panda haraka uje kwetu utuokoe! Tusaidie, kwa sababu wafalme wote wa Waamori wanaokaa nchi ya vilima wameunganisha majeshi yao pamoja dhidi yetu.”
7 Basi Yoshua akaondoka Gilgali pamoja na jeshi lake lote, wakiwepo mashujaa wote. 8 Mwenyezi Mungu akamwambia Yoshua, “Usiwaogope watu hao, nimewatia mkononi mwako. Hakuna yeyote atakayeweza kushindana nawe.”
9 Baada ya Yoshua kutembea usiku kucha kutoka Gilgali, akawashambulia ghafula. 10 Mwenyezi Mungu akawafadhaisha mbele ya Waisraeli, naye Yoshua na Waisraeli wakawashinda kwa ushindi mkuu huko Gibeoni. Waisraeli wakawafukuza kwa njia inayopanda kwenda Beth-Horoni, huku wakiwaua hadi kufikia Azeka na Makeda. 11 Walipokuwa wanawakimbia Waisraeli kwenye barabara inayoteremka kutoka Beth-Horoni hadi Azeka, Mwenyezi Mungu akawavurumishia mawe makubwa kama mvua kutoka mbinguni, na wengi wao walikufa kwa mawe kuliko wale waliokufa kwa panga za Waisraeli.
12 Siku ile Mwenyezi Mungu alipowakabidhi Waamori kwa Waisraeli, Yoshua akanena na Mwenyezi Mungu akiwa mbele ya Waisraeli, akasema:
“Wewe jua, simama juu ya Gibeoni,
wewe mwezi, tulia juu ya Bonde la Aiyaloni.”
13 Hivyo jua likasimama,
nao mwezi ukatulia,
hadi taifa hilo lilipokwisha
kujilipizia kisasi kwa adui zake,
kama ilivyoandikwa katika Kitabu cha Yashari.
Jua likasimama katikati ya mbingu, likachelewa kuzama muda wa siku nzima. 14 Hakujakuwa na siku nyingine kama hiyo kabla au baada, siku ambayo Mwenyezi Mungu alimsikiliza mwanadamu. Hakika Mwenyezi Mungu alikuwa akiwapigania Israeli.
15 Ndipo Yoshua akarudi kambini huko Gilgali pamoja na Israeli yote.
Wafalme watano wa Waamori wauawa
16 Basi wale wafalme watano wakawa wamekimbia kujificha kwenye pango huko Makeda. 17 Yoshua alipoambiwa kuwa wafalme hao watano wamekutwa wakiwa wamejificha ndani ya pango huko Makeda, 18 akasema, “Vingirisheni mawe makubwa kwenye mlango wa pango, tena mweke walinzi wa kulilinda. 19 Lakini msiwaache! Wafuatieni adui zenu, washambulieni kutoka nyuma, wala msiwaache wafike kwenye miji yao, kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, amewatia mkononi mwenu.”
20 Hivyo Yoshua pamoja na Waisraeli wakawaangamiza, isipokuwa wachache waliosalia walifika kwenye miji yao yenye ngome. 21 Basi jeshi lote likarudi salama kwa Yoshua kule kambini Makeda, na hakuna yeyote aliyetoa neno kinyume cha Waisraeli.
22 Ndipo Yoshua akasema, “Haya fungueni mdomo wa pango, mniletee hao wafalme watano.” 23 Kwa hiyo wakawatoa hao wafalme watano nje ya pango: wafalme wa Yerusalemu, Hebroni, Yarmuthi, Lakishi na Egloni. 24 Walipokuwa wamewaleta hawa wafalme kwa Yoshua, akawaita wanaume wote wa Israeli, na kuwaambia majemadari wa vita walioenda pamoja naye, “Njooni hapa mweke nyayo zenu juu ya shingo za hawa wafalme.” Basi wakaja wakaweka nyayo zao shingoni.
25 Yoshua akawaambia, “Msiogope, wala msivunjike moyo. Kuweni hodari na wenye ushujaa. Hili ndilo Mwenyezi Mungu atakalowatendea adui zenu wote mnaoenda kupigana nao.” 26 Ndipo Yoshua akawapiga na kuwaua wale wafalme na kuwatundika juu ya miti mitano, nao wakaachwa wakining’inia juu ya ile miti hadi jioni.
27 Wakati wa kuzama jua Yoshua akaamuru, nao wakawashusha kutoka ile miti na kuwatupa kwenye lile pango ambalo walikuwa wamejificha. Wakaweka mawe makubwa kwenye mlango wa pango, ambayo yapo hadi leo.
28 Siku ile Yoshua akateka Makeda. Akamuua kila mmoja katika ule mji, pamoja na mfalme wake kwa upanga. Hakubakiza mtu yeyote. Akamfanyia mfalme wa Makeda kama vile alivyokuwa amemfanyia mfalme wa Yeriko.
Israeli yaangamiza miji ya kusini
29 Ndipo Yoshua akaondoka Makeda akiwa pamoja na Israeli yote hadi mji wa Libna na kuushambulia. 30 Mwenyezi Mungu pia akautia huo mji wa Libna pamoja na mfalme wake mikononi mwa Israeli. Yoshua akaangamiza ule mji na kila mtu aliyekuwa ndani yake kwa upanga. Hakubakiza huko mtu yeyote. Akamfanyia mfalme wa Libna kama alivyokuwa amemfanyia mfalme wa Yeriko.
31 Kisha Yoshua akaondoka Libna kwenda Lakishi akiwa pamoja na Israeli yote; wakajipanga dhidi yake na kuushambulia. 32 Mwenyezi Mungu akautia Lakishi mikononi mwa Israeli, hivyo Yoshua akauteka siku ya pili. Yoshua akauangamiza mji na kila kilichokuwa ndani yake kwa upanga, kama tu vile alivyokuwa ameufanyia mji wa Libna. 33 Wakati huo huo, Horamu mfalme wa Gezeri alikuwa amepanda ili kusaidia Lakishi, lakini Yoshua akamshinda pamoja na jeshi lake, hadi hapakubakia mtu yeyote.
34 Ndipo Yoshua akaondoka Lakishi kwenda Egloni akiwa pamoja na Israeli yote; wakajipanga dhidi yake na kuushambulia. 35 Wakauteka mji huo siku ile ile, wakaupiga kwa upanga na kumwangamiza kila mmoja aliyekuwa ndani yake, kama vile walivyokuwa wameufanyia Lakishi.
36 Kisha Yoshua na Waisraeli wote wakapanda kutoka Egloni hadi Hebroni, na kuushambulia. 37 Wakauteka mji na kuupiga kwa upanga, pamoja na mfalme wake, vijiji vyake na kila mmoja aliyekuwa ndani yake. Hawakubakiza mtu yeyote. Kama vile huko Egloni, waliuangamiza kabisa pamoja na kila mmoja aliyekuwa ndani yake.
38 Ndipo Yoshua na Waisraeli wote wakageuka na kushambulia Debiri. 39 Wakauteka mji, mfalme wake na vijiji vyake, na kuupiga kwa upanga. Kila mmoja aliyekuwa ndani yake wakamwangamiza kabisa. Hawakubakiza mtu yeyote. Wakaufanyia Debiri na mfalme wake kama vile walivyokuwa wameifanyia miji ya Libna na Hebroni na wafalme wao.
40 Hivyo Yoshua akalishinda eneo hilo lote, ikiwa ni pamoja na nchi ya vilima, na Negebu, na Shefela*au upande wa magharibi chini ya vilima, miteremko ya milima, pamoja na wafalme wake wote. Hakubakiza mtu yeyote. Akaangamiza kabisa kila kitu chenye pumzi, kama vile Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, alivyokuwa ameamuru. 41 Yoshua akawashinda kuanzia Kadesh-Barnea hadi Gaza na kutoka eneo lote la Gosheni hadi Gibeoni. 42 Wafalme hawa wote pamoja na nchi zao Yoshua aliwashinda kwa wakati mmoja, kwa sababu Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, aliwapigania Israeli.
43 Ndipo Yoshua akarudi pamoja na Israeli yote kwenye kambi huko Gilgali.