11
Wafalme wa kaskazini washindwa
Yabini mfalme wa Hazori aliposikia habari hizo, akatuma ujumbe kwa Yobabu mfalme wa Madoni, na kwa mfalme wa Shimroni, na kwa mfalme wa Akshafu, na pia kwa wafalme wa upande wa kaskazini wale waliokuwa milimani, katika Araba upande wa kusini mwa Kinerethi, katika Shefela*au upande wa magharibi chini ya vilima, na katika miinuko ya Nafoth-Dori upande wa magharibi; kwa Wakanaani upande wa mashariki na magharibi; kwa Waamori, Wahiti, Waperizi na Wayebusi katika nchi ya vilima; na kwa Wahivi chini ya Hermoni katika eneo ya Mispa. Wakaja na vikosi vyao vyote na idadi kubwa ya farasi na magari ya vita: jeshi kubwa, kama wingi wa mchanga ulio pwani ya bahari. Wafalme hawa wote wakaunganisha majeshi yao na kupiga kambi pamoja kwenye Maji ya Meromu, ili kupigana dhidi ya Israeli.
Mwenyezi Mungu akamwambia Yoshua, “Usiwaogope, kwa sababu kesho saa kama hii nitawatia wote mikononi mwa Israeli, wakiwa wameuawa. Utakata mishipa ya nyuma ya miguu ya farasi wao na kuyachoma moto magari yao ya vita.”
Hivyo Yoshua na jeshi lake lote wakaja dhidi yao ghafula kwenye Maji ya Meromu na kuwashambulia, naye Mwenyezi Mungu akawatia mikononi mwa Israeli. Wakawashinda na kuwafukuza hadi Sidoni Kuu na kuwafikisha Misrefoth-Maimu, hadi Bonde la Mispa upande wa mashariki, hata pakawa hakuna yeyote aliyebaki. Yoshua akawatendea kama Mwenyezi Mungu alivyoamuru. Akakata mishipa ya nyuma ya miguu ya farasi wao na kuchoma moto magari yao ya vita.
10 Wakati huo Yoshua akarudi na kuuteka mji wa Hazori na kumuua mfalme wake kwa upanga. (Hazori ulikuwa mji mkuu wa falme hizo zote.) 11 Kila aliyekuwa ndani yake wakamuua kwa upanga. Wakawaangamiza kabisa, wala hawakusaza chochote chenye pumzi, na akauchoma Hazori kwa moto.
12 Yoshua akaiteka hii miji yote ya kifalme pamoja na wafalme wake, na akawaua kwa upanga. Akawaangamiza kabisa wote, jinsi Musa mtumishi wa Mwenyezi Mungu alivyowaagiza. 13 Lakini Israeli hawakuichoma moto hata mojawapo ya miji iliyojengwa katika vilima vyao vidogo, isipokuwa mji wa Hazori, ambao Yoshua aliuchoma kwa moto. 14 Waisraeli wakajichukulia nyara zote na mifugo yote ya miji hii, bali waliwaua watu wote kwa upanga hadi walipowaangamiza kabisa, pasipo kumbakiza yeyote mwenye pumzi. 15 Kama vile Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa mtumishi wake, vivyo hivyo Musa alimwagiza Yoshua, naye Yoshua akafanya vivyo hivyo; hakukosa kufanya lolote katika yale yote Mwenyezi Mungu aliyomwagiza Musa.
16 Yoshua akaiteka nchi hii yote: nchi ya vilima, Negebu yote, eneo yote ya Gosheni, na Shefela, Araba na milima ya Israeli pamoja na materemko yake, 17 kuanzia Mlima Halaki ambao umeinuka kuelekea Seiri hadi Baal-Gadi katika Bonde la Lebanoni chini ya Mlima Hermoni. Akawateka wafalme wake wote, akawapiga na kuwaua. 18 Yoshua akapigana vita dhidi ya wafalme hawa wote kwa muda mrefu. 19 Hakuna mji wowote katika eneo hili uliofanya mkataba wa amani na Israeli, isipokuwa hao Wahivi wa Gibeoni. Wengine wote walishindwa katika vita. 20 Kwa maana Mwenyezi Mungu mwenyewe ndiye aliifanya mioyo yao iwe migumu, ili kupigana vita dhidi ya Israeli, ili apate kuwaangamiza kabisa, awafutilie mbali pasipo huruma, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa.
21 Wakati huo Yoshua akaenda kuwaangamiza Waanaki kutoka nchi ya vilima: kuanzia Hebroni, Debiri na Anabu, na kutoka nchi yote ya vilima ya Yuda, na kutoka nchi yote ya vilima ya Israeli. Yoshua akawaangamiza kabisa pamoja na miji yao. 22 Hakuna Waanaki waliosalia katika eneo la Waisraeli; ila tu, kuna wachache waliosalia katika maeneo ya Gaza, Gathi na Ashdodi. 23 Hivyo Yoshua akaiteka nchi hiyo yote kama vile Mwenyezi Mungu alivyokuwa amemwagiza Musa, naye Yoshua akawapa Israeli kuwa urithi wao, kulingana na walivyogawanyika katika makabila yao.
Ndipo nchi ikawa na amani bila vita.

*11:2 au upande wa magharibi chini ya vilima