13
Sehemu za Kanaani ambazo hazijatwaliwa
1 Yoshua alipokuwa mzee, umri wake ukiwa umesogea sana, Mwenyezi Mungu akamwambia, “Wewe ni mzee sana, na bado imesalia sehemu kubwa sana ya nchi ambayo haijatwaliwa.
2 “Nchi iliyosalia ni hii:
“maeneo yote ya Wafilisti na Wageshuri: 3 kutoka Mto Shihori ulioko mashariki mwa Misri, kuelekea kaskazini kwenye eneo la Ekroni, ambayo yote ilihesabika kama ya Wakanaani, maeneo yale matano ya watawala wa Wafilisti, ambayo ni Gaza, Ashdodi, Ashkeloni, Gathi na Ekroni;
nchi ya Waavi 4 kuanzia kusini;
nchi yote ya Wakanaani, kuanzia Ara ambayo ni ya Wasidoni, ikienea hadi Afeki, na eneo la Waamori,
5 eneo la Wagebali;
na Lebanoni yote kuelekea mashariki, kuanzia Baal-Gadi chini ya Mlima Hermoni hadi Lebo-Hamathi.
6 “Na kuhusu wakaaji wote katika maeneo ya milima, kuanzia Lebanoni hadi Misrefoth-Maimu, pamoja na eneo lote la Wasidoni, mimi mwenyewe nitawafukuza, niwaondoe kwa ajili ya Waisraeli. Hakikisha umegawa nchi hii kwa Israeli kuwa urithi, kama nilivyokuagiza, 7 sasa basi, ligawanye eneo hili kwa yale makabila tisa na ile nusu ya kabila la Manase kuwa urithi.”
Mgawanyo wa nchi mashariki mwa Yordani
8 Ile nusu nyingine ya Manase, Wareubeni na Wagadi, walishapokea urithi Musa aliokuwa amewapa mashariki mwa Yordani, sawasawa na mtumishi wa Mwenyezi Mungu alivyowagawia.
9 Eneo lao lilienea toka Aroeri, iliyo ukingoni mwa Bonde la Arnoni, kuanzia mji ulio katikati ya bonde, likijumlisha nchi ya uwanda wa juu wote wa Medeba hadi Diboni, 10 nayo miji yote ya Sihoni mfalme wa Waamori, aliyetawala Heshboni, hadi mpakani mwa Waamoni.
11 Vilevile ilijumlisha Gileadi, eneo la Wageshuri na Wamaaka, mlima wote wa Hermoni na Bashani yote ikienea hadi Saleka: 12 yaani ufalme wote wa Ogu katika Bashani, aliyekuwa ametawala katika Ashtarothi na Edrei, na ndiye pekee alisalia kwa Warefai. Musa alikuwa amewashinda na kuteka nchi yao. 13 Lakini Waisraeli hawakuwafukuza Wageshuri na Wamaaka, kwa hiyo wanaendelea kuishi miongoni mwa Waisraeli hadi leo.
14 Lakini kwa kabila la Lawi, Musa hakupeana urithi, kwa kuwa sadaka za kuteketezwa kwa moto zilizotolewa kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, ndizo zilikuwa urithi wao, kama alivyowaahidi.
15 Haya ndio maeneo ambayo Musa alikuwa amewapa kabila la Reubeni kufuatana na koo zao:
16 Eneo la Aroeri lililo ukingoni mwa Bonde la Arnoni, na kuanzia mji ulio katikati ya bonde, pia uwanda wote wa juu kupita Medeba 17 hadi Heshboni na miji yake yote kwenye uwanda wa juu, ikijumlishwa miji ya Diboni, Bamoth-Baali, Beth-Baal-Meoni, 18 Yahasa, Kedemothi, Mefaathi, 19 Kiriathaimu, Sibma, Sereth-Shahari juu ya kilima kilicho katika bonde, 20 Beth-Peori, miteremko ya Pisga na Beth-Yeshimothi: 21 miji yote ya uwanda wa juu na eneo lote la utawala wa Sihoni mfalme wa Waamori, aliyetawala katika Heshboni. Musa alikuwa amemshinda Sihoni, pia watawala wakuu wa Wamidiani, ambao ni Evi, Rekemu, Suri, Huri na Reba, waliokuwa wameungana na Sihoni, ambao waliishi katika nchi ile. 22 Pamoja na wale waliouawa katika vita, Waisraeli walikuwa wamemuua kwa upanga Balaamu mwana wa Beori aliyekuwa mwaguzi.
23 Mpaka wa Wareubeni ulikuwa ni ukingo wa Mto Yordani. Miji hii na vijiji vyake ilikuwa urithi wa Wareubeni kufuatana na koo zao.
24 Haya ndio maeneo ambayo Musa alikuwa amewapa kabila la Gadi, kufuatana na koo zao:
25 Nchi ya Yazeri, miji yote ya Gileadi na nusu ya nchi ya Amoni iliyoenea hadi Aroeri, karibu na Raba; 26 na kuanzia Heshboni hadi Ramath-Mispa na Betonimu, na kutoka Mahanaimu hadi eneo la Debiri; 27 na katika bonde, Beth-Haramu, Beth-Nimra, Sukothi na Safoni na sehemu iliyobaki ya eneo la utawala wa Sihoni mfalme wa Heshboni (upande wa mashariki mwa Mto Yordani, eneo inayoishia kwenye Bahari ya Kinerethi*yaani Bahari ya Galilaya).
28 Miji hii na vijiji vyake ilikuwa urithi wa kabila la Gadi kufuatana na koo zao.
29 Haya ndio maeneo ambayo Musa alikuwa amewapa nusu ya kabila la Manase, yaani kwa nusu ya jamaa ya uzao wa Manase, kufuatana na koo zao:
30 Eneo lililoenea kuanzia Mahanaimu, na kujumlisha Bashani yote, ufalme wote wa Ogu mfalme wa Bashani, makazi yote ya Yairi huko Bashani, miji sitini, 31 nusu ya Gileadi, na Ashtarothi na Edrei (miji ya kifalme ya Ogu katika Bashani).
Hii ilikuwa kwa ajili ya wazao wa Makiri mwana wa Manase, kwa ajili ya nusu ya wana wa Makiri, kufuatana na koo zao.
32 Huu ndio urithi Musa alipeana alipokuwa katika tambarare za Moabu, ng’ambo ya Yordani, mashariki mwa Yeriko. 33 Lakini kwa kabila la Walawi, Musa hakuwapa urithi; Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli ndiye urithi wao, kama alivyowaahidi.