16
Mgawo kwa Efraimu na Manase
Mgawanyo wa Yusufu ulianzia Yordani ya Yeriko, mashariki mwa miji ya Yeriko na kutoka hapo ulipanda kupitia jangwani na kuingia katika nchi ya vilima ya Betheli. Ukaendelea kutoka Betheli (ndiyo Luzu), ukavuka kuingia eneo la Waarki huko Atarothi, ukateremkia kuelekea magharibi hadi eneo la Wayafleti ukienea hadi eneo la Beth-Horoni ya Chini hadi Gezeri, ukiishia baharini.
Kwa hiyo Manase na Efraimu, wazao wa Yusufu, walipokea urithi wao.
 
 
Hili ndilo lilikuwa eneo la Efraimu, kufuatana na koo zao:
 
Mpaka wa urithi wao ulianzia Ataroth-Adari upande wa mashariki hadi Beth-Horoni ya Juu, na kuendelea mpaka baharini. Kutoka Mikmeta upande wa kaskazini ulipinda kuelekea mashariki hadi Taanath-Shilo, ukiupita hadi Yanoa upande wa mashariki. Kisha uliteremka kutoka Yanoa hadi Atarothi na Naara, ukagusa Yeriko na kutokea katika Mto Yordani. Kutoka Tapua, mpaka ulienda magharibi hadi Bonde la Kana na kuishia baharini. Huu ulikuwa ndio urithi wa kabila la Waefraimu, kufuatana na koo zao.
Pia ulijumuisha miji yote na vijiji vyake ambavyo vilitengwa kwa ajili ya Waefraimu ndani ya urithi wa kabila la Manase.
10 Hawakuwatoa Wakanaani walioishi Gezeri; hadi leo Wakanaani wanaishi miongoni mwa watu wa Efraimu, lakini wanatumikishwa kwa kazi ngumu.