4
Sadaka ya dhambi
Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Waambie Waisraeli: ‘Mtu yeyote afanyapo dhambi bila kukusudia na akatenda lile lililokatazwa katika amri yoyote ya Mwenyezi Mungu:
“ ‘Ikiwa kuhani aliyepakwa mafuta amefanya dhambi na kuwaletea watu hatia, lazima alete kwa Mwenyezi Mungu fahali mchanga asiye na dosari, kuwa sadaka ya dhambi kwa ajili ya dhambi aliyotenda. Atamkabidhi huyo fahali kwenye ingilio la Hema la Kukutania mbele za Mwenyezi Mungu. Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha huyo fahali na kumchinja mbele za Mwenyezi Mungu. Kisha kuhani huyo aliyepakwa mafuta atachukua sehemu ya damu ya huyo fahali na kuileta katika Hema la Kukutania. Atachovya kidole chake katika hiyo damu, na kuinyunyiza sehemu yake mara saba mbele za Mwenyezi Mungu, mbele ya pazia la mahali patakatifu. Kisha kuhani atatia sehemu ya hiyo damu juu ya pembe za madhabahu ya kufukizia uvumba wenye harufu nzuri iliyo mbele za Mwenyezi Mungu katika Hema la Kukutania. Damu iliyobaki ya huyo fahali ataimwaga chini ya hayo madhabahu ya kuteketezea sadaka kwenye ingilio la Hema la Kukutania. Atayaondoa mafuta yote ya fahali huyo wa sadaka ya dhambi: mafuta yale yanayofunika sehemu za ndani au zile zinazounganika nazo, figo zote mbili na mafuta yaliyo juu yake karibu na kiuno, na kipande kirefu cha ini, ambayo atayaondoa pamoja na figo zote, 10 kama vile mafuta yanavyoondolewa kutoka kwa ng’ombe aliyetolewa sadaka ya amani. Kisha kuhani ataviteketeza juu ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa. 11 Lakini ngozi ya huyo fahali na nyama zake zote, pamoja na kichwa na miguu yake, sehemu za ndani na matumbo, 12 yaani sehemu nyingine zote zilizobaki za huyo fahali, lazima azitoe nje ya kambi hadi mahali palipo safi, ambapo majivu hutupwa; naye atamchoma kwa moto wa kuni juu ya lundo la majivu.
13 “ ‘Ikiwa jumuiya yote ya Israeli watatenda dhambi pasipo kukusudia na kufanya lile lililokatazwa katika amri yoyote ya Mwenyezi Mungu, hata kama jumuiya hawafahamu jambo hilo, wana hatia. 14 Wanapotambua dhambi waliyoitenda, lazima kusanyiko walete fahali mchanga kuwa sadaka ya dhambi, na kuikabidhi mbele ya Hema la Kukutania. 15 Wazee wa jumuiya wataweka mikono yao juu ya kichwa cha huyo fahali mbele za Mwenyezi Mungu, naye huyo fahali atachinjwa mbele za Mwenyezi Mungu. 16 Kisha kuhani aliyepakwa mafuta ataingiza sehemu ya damu ya huyo fahali ndani ya Hema la Kukutania. 17 Atachovya kidole chake kwenye damu na kuinyunyiza mara saba mbele za Mwenyezi Mungu mbele ya hilo pazia. 18 Atatia sehemu ya hiyo damu juu ya pembe za madhabahu yaliyo mbele za Mwenyezi Mungu katika Hema la Kukutania. Damu iliyobaki ataimwaga chini ya madhabahu ya kuteketezea sadaka, penye ingilio la Hema la Kukutania. 19 Atayaondoa mafuta yote ya yule fahali na kuyateketeza juu ya madhabahu, 20 naye atamfanyia fahali huyu kama alivyomfanyia yule fahali mwingine wa sadaka ya dhambi. Kwa njia hii kuhani atawafanyia watu upatanisho, nao watasamehewa. 21 Kisha atamchukua yule fahali nje ya kambi na kumteketeza kama alivyomteketeza yule wa kwanza. Hii ni sadaka ya dhambi kwa ajili ya jumuiya.
22 “ ‘Wakati kiongozi ametenda dhambi bila kukusudia na kufanya yaliyokatazwa katika amri yoyote ya Mwenyezi Mungu, Mungu wake, ana hatia. 23 Atakapofahamishwa dhambi aliyotenda, ni lazima alete beberu asiye na dosari kuwa sadaka yake. 24 Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha yule mbuzi na kumchinja mahali pale sadaka za kuteketezwa huchinjiwa mbele za Mwenyezi Mungu. Hii ni sadaka ya dhambi. 25 Kisha kuhani atachukua sehemu ya damu ya sadaka ya dhambi kwa kidole chake na kuitia kwenye pembe za madhabahu ya sadaka ya kuteketeza, na kuimwaga damu iliyobaki chini ya madhabahu. 26 Atayateketeza mafuta yote juu ya madhabahu, kama alivyoteketeza mafuta ya mnyama wa sadaka ya amani. Kwa njia hii kuhani atafanya upatanisho wa dhambi kwa ajili ya yule mtu, naye atasamehewa.
27 “ ‘Kama mtu katika jumuiya ametenda dhambi pasipo kukusudia, na kufanya lile lililokatazwa katika amri yoyote ya Mwenyezi Mungu, yeye ana hatia. 28 Atakapofahamishwa dhambi aliyoitenda, ni lazima alete mbuzi jike asiye na dosari kuwa sadaka yake kwa ajili ya dhambi aliyotenda. 29 Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha sadaka ya dhambi na kumchinjia mahali pa kuteketezea sadaka. 30 Kisha kuhani atachukua sehemu ya ile damu kwa kidole chake na kuitia kwenye pembe za madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na kuimwaga damu iliyobaki chini ya madhabahu. 31 Atayaondoa mafuta yote, kama vile mafuta yaondolewavyo kwenye sadaka ya amani, naye kuhani atayateketeza juu ya madhabahu kama harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi Mungu. Kwa njia hii kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake, naye atasamehewa.
32 “ ‘Akileta mwana-kondoo kuwa sadaka yake ya dhambi, atamleta jike asiye na dosari. 33 Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha huyo mwana-kondoo na kumchinja kwa ajili ya sadaka ya dhambi mahali ambako sadaka ya kuteketezwa huchinjiwa. 34 Kisha kuhani atachukua sehemu ya damu ya sadaka ya dhambi kwa kidole chake na kuitia juu ya pembe za madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, na ile damu iliyobaki ataimwaga chini ya madhabahu. 35 Ataondoa mafuta yote, kama vile mafuta yaondolewavyo kutoka kwa mwana-kondoo wa sadaka ya amani, naye kuhani atayateketeza juu ya madhabahu juu ya zile sadaka zilizotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa moto. Kwa njia hii kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake kwa dhambi aliyoitenda, naye atasamehewa.