3
Sadaka ya amani
“ ‘Ikiwa mtu anatoa sadaka ya amani, naye akatoa ng’ombe, akiwa dume au jike, atamleta mnyama asiye na dosari mbele za Mwenyezi Mungu. Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha sadaka yake na kumchinja penye ingilio la Hema la Kukutania. Ndipo makuhani, wana wa Haruni, watanyunyiza damu ya huyo mnyama pande zote za madhabahu. Katika hiyo sadaka ya amani ataleta sadaka iliyotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa moto: sehemu za ndani na mafuta yote yanayoungana nazo, figo zote pamoja na mafuta yaliyozifunika karibu na kiuno, na kipande kirefu cha ini; utayaondoa pamoja na figo. Kisha wana wa Haruni wataiteketeza juu ya madhabahu, juu ya ile sadaka ya kuteketezwa iliyo juu ya kuni zinazowaka; ni sadaka ya kuteketezwa kwa moto, harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi Mungu.
“ ‘Akitoa kondoo au mbuzi kutoka kundi kuwa sadaka ya amani kwa Mwenyezi Mungu, atamtoa dume au jike asiye na dosari. Akimtoa mwana-kondoo, atamleta mbele za Mwenyezi Mungu. Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha sadaka yake, naye atamchinja mbele ya Hema la Kukutania. Kisha wana wa Haruni watanyunyiza damu ya huyo mnyama pande zote za madhabahu. Katika hiyo sadaka ya amani ataleta dhabihu iliyotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa moto: mafuta yake, mafuta yote ya mkia uliokatwa karibu na uti wa mgongo, mafuta yote yanayofunika sehemu za ndani au yale yanayounganika nazo, 10 figo mbili pamoja na mafuta yanayozifunika yaliyo karibu na kiuno, na kipande kirefu cha ini, ambayo utayaondoa pamoja na figo. 11 Kuhani ataviteketeza juu ya madhabahu viwe chakula, sadaka iliyotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa moto.
12 “ ‘Ikiwa sadaka yake ni mbuzi, ataileta mbele za Mwenyezi Mungu. 13 Ataweka mkono wake juu ya kichwa chake na kumchinja mbele ya Hema la Kukutania. Kisha wana wa Haruni watanyunyiza damu ya huyo mnyama pande zote za madhabahu. 14 Katika ile sadaka anayotoa, atatoa hii sadaka ya kuteketezwa kwa Mwenyezi Mungu: mafuta yote yanayofunika sehemu za ndani na yale yanayoungana nazo, 15 figo zote mbili pamoja na mafuta yaliyo juu yake karibu na kiuno, na kipande kirefu cha ini, ambayo atayaondoa pamoja na figo. 16 Kuhani ataviteketeza juu ya madhabahu viwe chakula, sadaka iliyotolewa kwa moto, harufu nzuri. Mafuta yote ya mnyama ni ya Mwenyezi Mungu.
17 “ ‘Hili ni agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo, popote mnapoishi: Msile mafuta yoyote ya mnyama wala damu.’ ”