7
Sadaka ya hatia
1 “ ‘Haya ndio masharti kwa ajili ya sadaka ya hatia, ambayo ni takatifu sana: 2 Sadaka ya hatia itachinjiwa mahali pale sadaka ya kuteketezwa huchinjiwa, nayo damu yake itanyunyizwa pande zote za madhabahu. 3 Mafuta yake yote yatatolewa sadaka: mafuta ya mkia, na mafuta yale yanayofunika sehemu za ndani, 4 figo zote mbili pamoja na mafuta yanayozifunika karibu na kiuno, na kipande kirefu cha ini, ambayo yataondolewa pamoja na hizo figo. 5 Kuhani atayateketeza juu ya madhabahu kuwa sadaka iliyotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa moto. Hii ni sadaka ya hatia. 6 Mwanaume yeyote katika jamaa ya kuhani aweza kuila, lakini lazima iliwe mahali patakatifu; ni takatifu sana.
7 “ ‘Sheria hii ya sadaka ya hatia ni sawasawa na ile ya sadaka ya dhambi: Nyama ya yule mnyama aliyetolewa sadaka ni ya yule kuhani anayesimamia ibada ya upatanisho. 8 Kuhani anayetoa sadaka ya kuteketezwa kwa ajili ya mtu yeyote anaweza kuichukua ngozi ya mnyama yule aliyetolewa iwe yake. 9 Kila sadaka ya nafaka iliyookwa jikoni au kupikwa katika sufuria au katika kikaango itakuwa ya kuhani anayeitoa. 10 Nayo kila sadaka ya nafaka, iwe imechanganywa na mafuta au iko kavu, itakuwa ya wana wa Haruni, nayo itagawanywa sawa kati yao.
Sadaka ya amani
11 “ ‘Haya ndio masharti kwa ajili ya sadaka ya amani ambayo mtu aweza kuileta kwa Mwenyezi Mungu:
12 “ ‘Ikiwa mtu atatoa sadaka ya amani kwa ajili ya kuonesha shukrani, pamoja na sadaka hii ya shukrani, atatoa maandazi yasiyotiwa chachu yaliyochanganywa na mafuta, mikate myembamba isiyotiwa chachu na iliyopakwa mafuta, na maandazi ya unga laini uliokandwa vizuri na kuchanganywa na mafuta. 13 Pamoja na sadaka yake ya amani ya shukrani, ataleta sadaka ya maandazi yaliyotengenezwa kwa chachu. 14 Ataleta moja ya kila aina ya andazi kuwa sadaka, matoleo kwa Mwenyezi Mungu; hii ni ya kuhani anayenyunyiza damu ya sadaka ya amani. 15 Nyama ya sadaka ya amani kwa ajili ya shukrani lazima iliwe siku hiyo hiyo inapotolewa; hutabakiza kitu chochote hadi asubuhi.
16 “ ‘Lakini ikiwa sadaka yake ni kwa ajili ya nadhiri au ni sadaka ya hiari, sadaka hiyo italiwa siku hiyo inapotolewa, lakini chochote kinachobakia kinaweza kuliwa kesho yake. 17 Nyama yoyote ya sadaka inayobaki hadi siku ya tatu lazima iteketezwe kwa moto. 18 Kama nyama yoyote ya sadaka ya amani italiwa siku ya tatu, Mwenyezi Mungu hataikubali. Haitahesabiwa kwake huyo aliyeitoa, kwa kuwa ni najisi. Mtu atakayekula sehemu yake yoyote atahesabiwa hatia.
19 “ ‘Nyama inayogusa chochote kilicho najisi kamwe haitaliwa; lazima iteketezwe kwa moto. Kuhusu nyama nyingine, mtu yeyote aliyetakaswa anaweza kuila. 20 Lakini kama mtu yeyote najisi akila nyama yoyote ya sadaka ya amani iliyotolewa kwa Mwenyezi Mungu, huyo mtu lazima akatiliwe mbali na watu wake. 21 Kama mtu yeyote akigusa kitu kilicho najisi, iwe ni uchafu wa mwanadamu, au mnyama najisi, au kitu chochote kilicho najisi, kitu cha kuchukiza, kisha akala nyama yoyote ya sadaka ya amani iliyotolewa kwa Mwenyezi Mungu, mtu huyo ni lazima akatiliwe mbali na watu wake.’ ”
Kula mafuta na kunywa damu kwakatazwa
22 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, 23 “Waambie Waisraeli: ‘Msile mafuta yoyote ya ng’ombe, kondoo wala mbuzi. 24 Mafuta ya mnyama aliyekutwa amekufa au ameraruliwa na wanyama pori yanaweza kutumika kwa kazi nyingine yoyote, lakini kamwe msiyale. 25 Mtu yeyote alaye mafuta ya mnyama ambaye ametolewa sadaka kwa Mwenyezi Mungu kwa moto ni lazima akatiliwe mbali na watu wake. 26 Popote mtakapoishi, kamwe msile damu ya ndege yeyote wala ya mnyama. 27 Mtu yeyote atakayekula damu lazima akatiliwe mbali na watu wake.’ ”
Fungu la makuhani
28 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, 29 “Waambie Waisraeli: ‘Mtu yeyote aletaye sadaka ya amani kwa Mwenyezi Mungu ataleta sehemu ya sadaka hiyo kama dhabihu yake kwa Mwenyezi Mungu. 30 Ataleta sadaka kwa mikono yake mwenyewe iliyotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa moto; ataleta mafuta ya huyo mnyama pamoja na kidari, naye atainua hicho kidari mbele za Mwenyezi Mungu kuwa sadaka ya kuinuliwa. 31 Kuhani atayateketeza hayo mafuta juu ya madhabahu, lakini kidari kitakuwa cha Haruni na wanawe. 32 Paja la kulia la sadaka zako za amani utampa kuhani kama matoleo. 33 Mwana wa Haruni atoaye damu na mafuta ya mnyama wa sadaka ya amani ndiye atakayepewa paja hilo la kulia kuwa fungu lake. 34 Kutoka kwa sadaka za amani za Waisraeli, mimi Mungu nimepokea kidari kile kilichoinuliwa, pamoja na lile paja lililotolewa, nami nimevitoa kwa kuhani Haruni na wanawe kuwa fungu lao la milele kutoka kwa Waisraeli.’ ”
35 Hii ndiyo sehemu ya sadaka zilizotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa moto, ambazo zilitengwa kwa ajili ya Haruni na wanawe siku ile walipowekwa wakfu ili kumtumikia Mwenyezi Mungu katika kazi ya ukuhani. 36 Siku ile walipopakwa mafuta, Mwenyezi Mungu aliagiza kwamba Waisraeli wawape hili kama fungu lao la milele kwa vizazi vijavyo.
37 Basi haya ndio masharti kuhusu sadaka ya kuteketezwa, sadaka ya nafaka, sadaka ya dhambi, sadaka ya hatia, sadaka ya kuwekwa wakfu, na sadaka ya amani, 38 ambayo Mwenyezi Mungu alimpa Musa juu ya Mlima Sinai siku ile alipowaagiza Waisraeli walete sadaka zao kwa Mwenyezi Mungu, katika Jangwa la Sinai.