8
Kuwekwa wakfu kwa Haruni na wanawe
(Kutoka 29:1-37)
1 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, 2 “Waletee Haruni na wanawe mavazi yao, mafuta ya upako, fahali kwa ajili ya sadaka ya dhambi, kondoo dume wawili na kikapu chenye mikate iliyotengenezwa bila chachu. 3 Kisha kusanya watu wote kwenye ingilio la Hema la Kukutania.” 4 Musa akafanya kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza, na watu wakakusanyika kwenye ingilio la Hema la Kukutania.
5 Musa akawaambia kusanyiko, “Hili ndilo Mwenyezi Mungu ameagiza lifanyike.” 6 Kisha Musa akamleta Haruni na wanawe mbele, akawaosha kwa maji. 7 Akamvika Haruni koti, akamfunga mshipi, akamvika joho, na kumvalisha kizibau. Pia akamfunga hicho kizibau kiunoni mwake kwa mshipi uliofumwa kwa ustadi. 8 Akaweka kifuko cha kifuani juu yake, na kuweka Urimu na Thumimu*Urimu na Thumimu maana yake ni Nuru na Kweli; vifaa hivi viliwekwa kwenye kifuko cha juu cha kisibau cha kuhani mkuu ili kujua mapenzi ya Mungu kwenye mambo ya kutatanisha. kwenye hicho kifuko. 9 Kisha akamvika Haruni kilemba kichwani pake, akaweka lile bamba la dhahabu, lile taji takatifu, upande wa mbele wa kilemba, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa.
10 Kisha Musa akachukua mafuta ya upako, na kuipaka maskani ya Mungu na kila kitu kilichokuwamo; hivyo akaviweka wakfu. 11 Akanyunyiza sehemu ya mafuta juu ya madhabahu mara saba, akaipaka madhabahu mafuta na vyombo vyake vyote, pamoja na sinia na kinara chake, ili kuviweka wakfu. 12 Akamimina sehemu ya hayo mafuta ya upako kichwani mwa Haruni, akampaka mafuta ili kumweka wakfu. 13 Kisha akawaleta wana wa Haruni mbele, akawavika makoti, akawafunga mishipi na kuwavika vilemba, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa.
14 Kisha akamtoa fahali kwa ajili ya sadaka ya dhambi, nao Haruni na wanawe wakaweka mikono yao juu ya kichwa chake. 15 Musa akamchinja yule fahali na akachukua sehemu ya hiyo damu, kisha kwa kidole chake akaitia kwenye pembe zote za madhabahu ili kutakasa madhabahu. Akaimwaga damu iliyobaki chini ya madhabahu. Kwa hiyo akayaweka wakfu ili kufanya upatanisho kwa ajili ya madhabahu. 16 Pia Musa akachukua mafuta yote yanayofunika sehemu za ndani, na kipande kirefu cha ini, na figo zote mbili pamoja na mafuta yake, akayateketeza juu ya madhabahu. 17 Lakini fahali, ikiwa pamoja na ngozi yake na nyama yake na sehemu zake za ndani na matumbo, akaiteketeza nje ya kambi, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa.
18 Kisha Musa akamleta kondoo dume kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, naye Haruni na wanawe wakaweka mikono yao juu ya kichwa chake. 19 Ndipo Musa akamchinja yule kondoo dume na kunyunyiza damu yake pande zote za madhabahu. 20 Musa akamkata yule kondoo dume vipande vipande na kukiteketeza kichwa, vile vipande na yale mafuta. 21 Kisha akamsafisha sehemu za ndani na miguu kwa maji, na kumteketeza yule kondoo dume mzima juu ya madhabahu kuwa sadaka ya kuteketezwa, harufu nzuri ya kupendeza, sadaka iliyotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa moto, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa.
22 Kisha Musa akamleta yule kondoo dume wa pili, ndiye kondoo dume kwa ajili ya kuwaweka wakfu, naye Haruni na wanawe wakaweka mikono yao juu ya kichwa chake. 23 Musa akamchinja yule kondoo dume, akaichukua sehemu ya damu yake na kuipaka juu ya ncha ya sikio la kuume la Haruni, na juu ya kidole gumba cha mkono wake wa kuume na juu ya kidole kikubwa cha mguu wake wa kuume. 24 Pia Musa akawaleta hao wana wa Haruni mbele, akaipaka sehemu ya hiyo damu kwenye ncha za masikio yao ya kuume, juu ya vidole gumba vya mikono yao ya kuume, na juu ya vidole vikubwa vya miguu yao ya kuume. Kisha akanyunyiza damu pande zote za madhabahu. 25 Akachukua mafuta ya mnyama, mafuta ya mkia, mafuta yote yanayofunika sehemu za ndani, kipande kirefu cha ini, figo zote mbili pamoja na mafuta yake, na paja la kulia. 26 Kisha kutoka kwa kikapu cha mikate iliyotengenezwa bila chachu, kilichokuwa mbele za Mwenyezi Mungu, akachukua andazi moja, na jingine lililotengenezwa kwa mafuta, na mkate mwembamba; akaviweka hivi vyote juu ya mafungu ya mafuta ya mnyama, na juu ya lile paja la kulia. 27 Akaviweka hivi vyote mikononi mwa Haruni na wanawe, na kuviinua mbele za Mwenyezi Mungu kuwa sadaka ya kuinuliwa. 28 Kisha Musa akavichukua kutoka mikononi mwao na kuviteketeza juu ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa kuwa sadaka ya kuwekwa wakfu, harufu nzuri ya kupendeza, sadaka iliyotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa moto. 29 Kisha akachukua kidari, kilicho fungu la Musa la kondoo dume kwa ajili ya kuwekwa wakfu, na kukiinua mbele za Mwenyezi Mungu kuwa sadaka ya kuinuliwa, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa.
30 Kisha Musa akachukua sehemu ya mafuta ya upako, na sehemu ya damu kutoka madhabahu, na kuvinyunyiza juu ya Haruni na mavazi yake, na juu ya wanawe na mavazi yao. Kwa hiyo akamweka Haruni na mavazi yake wakfu, pamoja na wanawe na mavazi yao.
31 Kisha Musa akamwambia Haruni na wanawe, “Pikeni hiyo nyama kwenye ingilio la Hema la Kukutania, na muile hapo pamoja na mkate kutoka kikapu cha sadaka ya kuweka wakfu, kama nilivyoagiza: ‘Haruni na wanawe wataila.’ 32 Kisha mteketeze nyama na mikate iliyobaki. 33 Msitoke kwenye ingilio la Hema la Kukutania kwa muda wa siku saba, hadi siku zenu za kuwekwa wakfu ziwe zimetimia, kwa kuwa muda wenu wa kuwekwa wakfu utakuwa siku saba. 34 Lile lililofanyika leo liliagizwa na Mwenyezi Mungu ili kufanya upatanisho kwa ajili yenu. 35 Lazima mkae kwenye ingilio la Hema la Kukutania usiku na mchana kwa siku saba, na kufanya lile Mwenyezi Mungu analolitaka, ili msife; kwa kuwa hilo ndilo nililoamriwa.” 36 Kwa hiyo Haruni na wanawe wakafanya kila kitu Mwenyezi Mungu alichoamuru kupitia kwa Musa.
*8:8 Urimu na Thumimu maana yake ni Nuru na Kweli; vifaa hivi viliwekwa kwenye kifuko cha juu cha kisibau cha kuhani mkuu ili kujua mapenzi ya Mungu kwenye mambo ya kutatanisha.