9
Makuhani waanza huduma yao
1 Katika siku ya nane, Musa akawaita Haruni na wanawe, na wazee wa Israeli. 2 Akamwambia Haruni, “Chukua ndama dume kwa ajili ya sadaka yako ya dhambi, na kondoo dume kwa sadaka yako ya kuteketezwa, wote wawili wasiwe na dosari, nao uwalete mbele za Mwenyezi Mungu. 3 Kisha waambie Waisraeli: ‘Chukueni beberu kwa ajili ya sadaka ya dhambi, na ndama na mwana-kondoo, wote wawili wawe wa umri wa mwaka mmoja, na wasio na dosari, kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, 4 na pia maksai na kondoo dume kwa ajili ya sadaka ya amani, ili kutoa dhabihu mbele za Mwenyezi Mungu, pamoja na sadaka ya nafaka iliyochanganywa na mafuta. Kwa kuwa leo Mwenyezi Mungu atawatokea.’ ”
5 Wakavileta vile vitu Musa alivyowaagiza mbele ya Hema la Kukutania, na kusanyiko lote wakakaribia na kusimama mbele za Mwenyezi Mungu. 6 Ndipo Musa akasema, “Hili ndilo Mwenyezi Mungu alilowaagiza mlifanye, ili utukufu wa Mwenyezi Mungu upate kuonekana kwenu.”
7 Musa akamwambia Haruni, “Njoo madhabahuni utoe dhabihu ya sadaka ya dhambi na sadaka ya kuteketezwa, kuwa upatanisho kwa ajili yako mwenyewe na kwa ajili ya watu. Kisha utoe sadaka ya upatanisho kwa ajili ya watu, kama vile Mwenyezi Mungu alivyoagiza.”
8 Hivyo Haruni akaja madhabahuni na kumchinja yule ndama kuwa sadaka ya dhambi kwa ajili yake mwenyewe. 9 Wanawe wakamletea damu, naye akachovya kidole chake katika hiyo damu, akaitia kwenye pembe za madhabahu, nayo damu iliyobaki akaimwaga chini ya madhabahu. 10 Juu ya madhabahu akateketeza mafuta, figo na kipande kirefu cha ini kutoka hiyo sadaka ya dhambi, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa. 11 Akateketeza nyama na ngozi nje ya kambi.
12 Kisha Haruni akachinja sadaka ya kuteketezwa. Wanawe wakamletea damu, naye akainyunyiza pande zote za madhabahu. 13 Wakamletea sadaka ya kuteketezwa kipande kwa kipande, pamoja na kichwa, naye akaviteketeza juu ya madhabahu. 14 Akasafisha sehemu za ndani na miguu, akaviteketeza juu ya sadaka ya kuteketezwa juu ya madhabahu.
15 Kisha Haruni akaleta sadaka ile iliyokuwa kwa ajili ya watu. Akachukua yule mbuzi wa sadaka ya dhambi kwa ajili ya watu, akamchinja na kumtoa kwa ajili ya sadaka ya dhambi, kama alivyofanya kwa ile ya kwanza.
16 Haruni akaleta sadaka ya kuteketezwa na kuitoa kama ilivyoelekezwa. 17 Pia akaleta sadaka ya nafaka, akachukua konzi moja na kuiteketeza juu ya madhabahu, pamoja na sadaka ya kuteketezwa ya asubuhi.
18 Akachinja maksai na kondoo dume kuwa sadaka ya amani kwa ajili ya watu. Wanawe Haruni wakampa ile damu, naye akainyunyiza pande zote za madhabahu. 19 Lakini sehemu zile za mafuta ya yule maksai na ya yule kondoo dume, yaani mafuta ya mkia, yaliyofunika tumbo, ya figo na kipande kirefu cha ini, 20 hivi vyote wakaviweka juu ya vidari, kisha Haruni akayateketeza hayo mafuta ya wanyama juu ya madhabahu. 21 Haruni akaviinua vile vidari na paja la kulia mbele za Mwenyezi Mungu ili viwe sadaka ya kuinuliwa, kama Musa alivyoagiza.
22 Kisha Haruni akainua mikono yake kuwaelekea watu na kuwabariki. Naye baada ya kutoa dhabihu ya sadaka ya dhambi, sadaka ya kuteketezwa, na sadaka ya amani, akashuka chini.
23 Kisha Musa na Haruni wakaingia kwenye Hema la Kukutania. Walipotoka nje, wakawabariki watu. Nao utukufu wa Mwenyezi Mungu ukawatokea watu wote. 24 Moto ukaja kutoka kwa uwepo wa Mwenyezi Mungu, ukaiteketeza ile sadaka ya kuteketezwa, pamoja na sehemu ya mafuta yaliyokuwa juu ya madhabahu. Watu wote walipoona jambo hili, wakashangilia kwa furaha na kusujudu.