22
Matumizi ya sadaka takatifu
1 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, 2 “Mwambie Haruni na wanawe kushughulikia kwa uangalifu sadaka takatifu Waisraeli wanazoziweka wakfu kwangu, ili wasilinajisi Jina langu takatifu. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
3 “Waambie: ‘Katika vizazi vijavyo, ikiwa yeyote wa wazao wako ni najisi, naye akakaribia sadaka takatifu zile Waisraeli wanazoweka wakfu kwa Mwenyezi Mungu, mtu huyo lazima akatiliwe mbali na uso wangu. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
4 “ ‘Ikiwa mzao wa Haruni ana ugonjwa wa ngozi unaoambukiza au anatokwa na usaha mwilini, hawezi kula sadaka takatifu hadi atakasike. Pia atakuwa najisi akigusa kitu chochote kilicho najisi kutokana na kugusa maiti, au akigusa mtu aliyetokwa na shahawa, 5 au akigusa kitu chochote kinachotambaa kimfanyacho mtu najisi, au mtu yeyote awezaye kumtia unajisi, hata unajisi uwe gani. 6 Mtu anayegusa kitu chochote cha aina hiyo atakuwa najisi hadi jioni. Kamwe hatakula sadaka yoyote takatifu hadi yeye mwenyewe awe ameoga kwa maji. 7 Jua linapotua, atakuwa safi, na baadaye anaweza kula sadaka takatifu, kwa kuwa ni vyakula vyake. 8 Kamwe asile nyama ya mzoga wala iliyoraruliwa na wanyama pori, naye akatiwa unajisi kwa hilo. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
9 “ ‘Makuhani lazima washike maagizo yangu ili wasiwe na hatia, wakafa kwa kuyadharau. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu ninayewafanya watakatifu.
10 “ ‘Hakuna mtu yeyote asiye wa jamaa ya kuhani anayeruhusiwa kula sadaka takatifu, hata mgeni wa kuhani au mfanyakazi wake haruhusiwi kuila. 11 Lakini ikiwa kuhani amenunua mtumwa kwa fedha, au mtumwa amezaliwa katika nyumba ya kuhani huyo, mtumwa huyo aweza kula chakula cha huyo kuhani. 12 Ikiwa binti ya kuhani ameolewa na mtu asiye kuhani, binti huyo haruhusiwi kula chochote cha matoleo matakatifu. 13 Lakini ikiwa binti ya kuhani amekuwa mjane au amepewa talaka, naye hana watoto, na akarudi kuishi na jamaa ya baba yake kama wakati wa usichana wake, binti huyo anaweza kula chakula cha baba yake. Hata hivyo, mtu asiyeruhusiwa hawezi kula chochote katika chakula hiki.
14 “ ‘Ikiwa mtu yeyote amekula sadaka takatifu kwa makosa, lazima atoe malipo ya sadaka hiyo kwa kuhani na kuongeza sehemu ya tano ya thamani ya sadaka hiyo. 15 Kamwe makuhani wasiinajisi sadaka takatifu ambayo Waisraeli wameitoa kwa Mwenyezi Mungu 16 kwa kuwaruhusu kuzila sadaka hizo takatifu, na hivyo kuwaletea hatia ya kudaiwa malipo. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu niwafanyaye watakatifu.’ ”
Dhabihu zisizokubalika
17 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, 18 “Sema na Haruni na wanawe, na Waisraeli wote uwaambie: ‘Ikiwa mmoja wenu, aliye Mwisraeli au mgeni anayeishi katika nchi ya Israeli, atatoa matoleo kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa kwa moto kwa Mwenyezi Mungu, iwe kutimiza nadhiri au kuwa sadaka ya hiari, 19 lazima amtoe mnyama dume asiye na dosari, akiwa ng’ombe, mbuzi au kondoo, ili aweze kukubalika kwa niaba yako. 20 Kamwe usitoe kitu chochote chenye dosari kwa sababu hakitakubaliwa kwa niaba yako. 21 Mtu yeyote aletapo sadaka ya amani kwa Mwenyezi Mungu kutoka kundi la ng’ombe au la mbuzi ili kutimiza nadhiri maalum au sadaka ya hiari, lazima sadaka hiyo isiwe na dosari au waa ili ikubalike. 22 Kamwe usimtolee Mwenyezi Mungu mnyama aliye kipofu, aliyejeruhiwa wala aliye kilema, au chochote kilicho na uvimbe, au chenye upele au vidonda vinavyotoka usaha. Kamwe chochote cha aina hii kisiwekwe juu ya madhabahu kuwa sadaka iliyotolewa kwa Mwenyezi Mungu ya kuteketezwa kwa moto. 23 Lakini unaweza ukamtoa ng’ombe au kondoo mwenye kilema au aliyedumaa kuwa sadaka ya hiari, lakini hii haitakubalika kuwa sadaka ya kutimiza nadhiri. 24 Kamwe usimtolee Mwenyezi Mungu mnyama ambaye mapumbu yake yamejeruhiwa, au kuhasiwa, au kuraruliwa au kukatwa. Kamwe usifanye hivi katika nchi yako mwenyewe, 25 na kamwe usikubali wanyama wa aina hii kutoka mkono wa mgeni ili kuwatoa wanyama hao kuwa chakula kwa Mungu wako. Wanyama hao hawatakubaliwa kwa niaba yako, kwa sababu wana vilema, nao wana dosari.’ ”
26 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, 27 “Ndama, mwana-kondoo au mwana-mbuzi anapozaliwa, atabaki na mama yake kwa siku saba. Kuanzia siku ya nane na kuendelea anaweza kukubaliwa kuwa sadaka iliyotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa kuteketezwa kwa moto. 28 Usimchinje ng’ombe na ndama wake, au kondoo na kitoto chake siku moja.
29 “Unapomtolea Mwenyezi Mungu dhabihu ya shukrani, itoe kwa namna ambayo itakubalika kwa niaba yako. 30 Ni lazima iliwe siku hiyo hiyo, pasipo kubakiza chochote hadi asubuhi. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
31 “Shikeni maagizo yangu na kuyafuata. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu. 32 Msilinajisi Jina langu takatifu. Lazima nikubalike kuwa mtakatifu kwa Waisraeli. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu ninayewafanya watakatifu, 33 na niliyewatoa katika nchi ya Misri niwe Mungu wenu. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.”