23
Sikukuu zilizoamriwa
Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Sema na Waisraeli na uwaambie: ‘Hizi ndizo sikukuu zangu zilizoamriwa, sikukuu zilizoamriwa za Mwenyezi Mungu, ambazo mtazitangaza kuwa makusanyiko matakatifu.
Sabato
“ ‘Kuna siku sita mnazoweza kufanya kazi, lakini siku ya saba ni Sabato ya kupumzika, siku ya kusanyiko takatifu. Hamtafanya kazi yoyote. Popote mnapoishi, ni Sabato kwa Mwenyezi Mungu.
Pasaka na Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu
(Hesabu 28:16-25)
“ ‘Hizi ni sikukuu za Mwenyezi Mungu zilizoamriwa, makusanyiko matakatifu mtakayoyatangaza kwa nyakati zilizoamriwa: Pasaka ya Mwenyezi Mungu huanza jioni ya siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza. Siku ya kumi na tano ya mwezi huo wa kwanza, Sikukuu ya Mwenyezi Mungu ya Mikate Isiyotiwa Chachu huanza; kwa siku saba, mtakula mikate isiyotiwa chachu. Katika siku ya kwanza, mtakuwa na kusanyiko takatifu, na msifanye kazi zenu za kawaida. Kwa siku saba mtamletea Mwenyezi Mungu sadaka ya kuteketezwa kwa moto. Kwenye siku hiyo ya saba mtafanya kusanyiko takatifu, na msifanye kazi zenu za kawaida.’ ”
Malimbuko
Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, 10 “Sema na Waisraeli na uwaambie: ‘Mtakapoingia katika nchi nitakayowapa na kuvuna mazao ya nchi hiyo, leteni kwa kuhani mganda wa nafaka ya kwanza mtakayovuna. 11 Naye atauinua huo mganda mbele za Mwenyezi Mungu ili ukubaliwe kwa niaba yenu; kuhani ataupunga siku inayofuata Sabato. 12 Siku hiyo mtakapoinua huo mganda, lazima mtoe kwa Mwenyezi Mungu dhabihu ya kuteketezwa kwa moto ya mwana-kondoo wa mwaka mmoja asiye na dosari, 13 pamoja na sadaka yake ya nafaka ya sehemu mbili za kumi ya efa*Sehemu mbili za kumi ya efa ni sawa na kilo mbili. ya unga laini uliochanganywa na mafuta, sadaka iliyotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa kuteketezwa kwa moto; hii itakuwa sadaka iliyo harufu nzuri ya kupendeza, na sadaka yake ya kinywaji ya robo ya hiniRobo ya hini ni sawa na lita moja. ya divai. 14 Kamwe msile mkate wowote, au nafaka iliyokaangwa au nafaka mpya, hadi siku ile mtakayomletea Mungu wenu sadaka hii. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo, popote mnapoishi.
Sikukuu ya Majuma
(Hesabu 28:26-31)
15 “ ‘Tangu siku ile iliyofuata Sabato, siku mliyotoa sadaka ya mganda wa kuinuliwa, hesabuni majuma saba kamili. 16 Mtahesabu siku hamsini hadi siku inayofuata Sabato ya saba, ndipo mtatoa sadaka ya nafaka mpya kwa Mwenyezi Mungu. 17 Kutoka popote mnapoishi, mtaleta mikate miwili iliyotengenezwa kwa sehemu mbili za kumi ya efa moja ya unga laini, uliookwa kwa chachu, kuwa sadaka ya kuinuliwa ya malimbuko kwa Mwenyezi Mungu. 18 Toeni pamoja na hiyo mikate wana-kondoo saba, kila mmoja wa mwaka mmoja asiye na dosari, na fahali mchanga, na kondoo dume wawili. Watakuwa sadaka ya kuteketezwa kwa moto iliyotolewa kwa Mwenyezi Mungu, pamoja na sadaka za nafaka na sadaka za vinywaji, sadaka iliyotolewa kwa moto yenye harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi Mungu. 19 Kisha toeni dhabihu ya beberu mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi, na wana-kondoo wawili, kila mmoja wa mwaka mmoja, kwa ajili ya sadaka ya amani. 20 Kuhani atawainua hao wana-kondoo wawili mbele za Mwenyezi Mungu kuwa sadaka ya kuinuliwa, pamoja na mkate wa malimbuko. Ni sadaka takatifu kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kuhani. 21 Siku hiyo hiyo mtatangaza kusanyiko takatifu, na msifanye kazi zenu za kawaida. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo, popote mtakapoishi.
22 “ ‘Mnapovuna mavuno ya ardhi yenu, msivune hadi mpakani mwa shamba lenu, au kukusanya masazo ya mavuno yenu. Hayo utayaacha kwa ajili ya maskini na mgeni. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.’ ”
Sikukuu ya Tarumbeta
(Hesabu 29:1-6)
23 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, 24 “Waambie Waisraeli: ‘Katika siku ya kwanza ya mwezi wa saba mtakuwa na Sabato ya mapumziko, kusanyiko takatifu la ukumbusho litakaloadhimishwa kwa kupiga tarumbeta. 25 Msifanye kazi zenu zozote za kawaida, lakini toeni sadaka kwa Mwenyezi Mungu iliyoteketezwa kwa moto.’ ”
Siku ya Upatanisho
(Hesabu 29:7-11)
26 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, 27 “Siku ya kumi ya mwezi huu wa saba ni Siku ya Upatanisho. Mtafanya kusanyiko takatifu, mfunge, na kutoa sadaka ya kuteketezwa kwa moto kwa Mwenyezi Mungu. 28 Msifanye kazi siku hiyo, kwa sababu ni Siku ya Upatanisho, ambapo upatanisho unafanyika kwa ajili yenu mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wenu. 29 Mtu ambaye hatafunga siku hiyo ni lazima akatiliwe mbali na watu wake. 30 Mtu atakayefanya kazi siku hiyo nitamwangamiza kutoka miongoni mwa watu wake. 31 Hamtafanya kazi kamwe. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo popote mnapoishi. 32 Ni Sabato ya mapumziko kwenu, na lazima mfunge. Tangu jioni ya siku ya tisa ya mwezi hadi jioni inayofuata, mtaishika Sabato yenu.”
Sikukuu ya Vibanda
(Hesabu 29:12-40)
33 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, 34 “Waambie Waisraeli: ‘Katika siku ya kumi na tano ya mwezi wa saba, Sikukuu ya vibanda itaanza, nayo itaadhimishwa kwa siku saba kwa Mwenyezi Mungu. 35 Siku ya kwanza ni kusanyiko takatifu, msifanye kazi zenu za kawaida. 36 Kwa siku saba toeni sadaka kwa Mwenyezi Mungu za kuteketezwa kwa moto. Kwenye siku ya nane fanyeni kusanyiko takatifu, na kutoa sadaka ya kuteketezwa kwa moto kwa Mwenyezi Mungu. Ni kusanyiko la mwisho, msifanye kazi zenu za kawaida.
37 (“ ‘Hizi ni sikukuu za Mwenyezi Mungu zilizoamriwa, ambazo mtazitangaza kuwa makusanyiko matakatifu kwa kuleta sadaka kwa Mwenyezi Mungu za kuteketeza kwa moto: sadaka za kuteketezwa na sadaka za nafaka, dhabihu na sadaka za vinywaji zitahitajika kila siku. 38 Sadaka hizi ni nyongeza ya zile mnazozitoa katika Sabato za Mwenyezi Mungu, na pia ni nyongeza ya matoleo yenu ya chochote mlichoweka nadhiri, na sadaka zenu zote za hiari mnazozitoa kwa Mwenyezi Mungu.)
39 “ ‘Basi kuanzia siku ya kumi na tano ya mwezi wa saba, baada ya kuvuna mazao yote ya nchi, mtaadhimisha sikukuu kwa Mwenyezi Mungu kwa siku saba; siku ya kwanza ni Sabato ya mapumziko, na pia siku ya nane ni Sabato ya mapumziko. 40 Siku ya kwanza mtachukua matunda mazuri ya miti, matawi ya mitende, matawi yenye majani mengi, na matawi ya mirebi, nanyi mtashangilia mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kwa siku saba. 41 Mtaadhimisha siku hii kuwa sikukuu kwa Mwenyezi Mungu kwa siku saba kila mwaka. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo; iadhimisheni mwezi wa saba. 42 Mtaishi katika vibanda kwa siku saba: Wazawa wote wa Waisraeli wataishi katika vibanda, 43 ili wazao wenu wajue kuwa niliwafanya Waisraeli waishi kwenye vibanda nilipowatoa Misri. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.’ ”
44 Kwa hiyo Musa akawatangazia Waisraeli sikukuu zilizoamriwa na Mwenyezi Mungu.

*23:13 Sehemu mbili za kumi ya efa ni sawa na kilo mbili.

23:13 Robo ya hini ni sawa na lita moja.