24
Mafuta na mikate mbele za Mwenyezi Mungu
1 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, 2 “Waagize Waisraeli wakuletee mafuta safi ya zeituni yaliyokamuliwa kwa ajili ya mwanga ili taa ziwe zinawaka daima. 3 Nje ya pazia la Sanduku la Ushuhuda ndani ya Hema la Kukutania, Haruni ataziwasha taa mbele za Mwenyezi Mungu kuanzia jioni hadi asubuhi daima. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo. 4 Taa zilizo juu ya kinara cha dhahabu safi mbele za Mwenyezi Mungu lazima zihudumiwe daima.
5 “Chukua unga laini, uoke mikate kumi na miwili, ukitumia sehemu mbili za kumi ya efa*Sehemu mbili za kumi ya efa ni sawa na kilo mbili. ya unga kwa kila mkate. 6 Iweke katika mistari miwili, kila mstari mikate sita, uiweke mbele za Mwenyezi Mungu juu ya meza iliyotengenezwa kwa dhahabu safi. 7 Kando ya kila mstari, weka uvumba safi kama sehemu ya kumbukumbu ili kuwakilisha mikate kuwa sadaka iliyotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa kuteketezwa kwa moto. 8 Mikate hii itawekwa mbele za Mwenyezi Mungu kila wakati, Sabato baada ya Sabato, kwa niaba ya Waisraeli, kuwa agano la kudumu. 9 Hii ni mali ya Haruni na wanawe, watakaoila katika mahali patakatifu, kwa sababu ni sehemu takatifu sana ya fungu lao milele la sadaka iliyotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa kuteketezwa kwa moto.”
Mwenye kukufuru apigwa mawe
10 Basi mwana wa mama Mwisraeli na baba Mmisri alienda miongoni mwa Waisraeli, nayo mapigano yakatokea ndani ya kambi kati yake na Mwisraeli. 11 Huyu mwana wa mwanamke Mwisraeli akalikufuru Jina la Mwenyezi Mungu kwa kulaani; kwa hiyo wakamleta kwa Musa. (Mama yake aliitwa Shelomithi binti Dibri, wa kabila la Dani.) 12 Nao wakamweka mahabusu hadi mapenzi ya Mwenyezi Mungu yawe wazi kwao.
13 Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Musa: 14 “Mchukue huyo aliyekufuru nje ya kambi. Wale wote waliomsikia akikufuru wataweka mikono juu ya kichwa chake, kisha kusanyiko lote watampiga mawe. 15 Waambie Waisraeli: ‘Ikiwa mtu yeyote atamlaani Mungu wake, atakuwa na hatia kwa uovu wake. 16 Yeyote atakayekufuru Jina la Mwenyezi Mungu ni lazima auawe. Kusanyiko lote watampiga kwa mawe. Iwe ni mgeni au mzawa, atakapolikufuru Jina la Mwenyezi Mungu, ni lazima auawe.
17 “ ‘Kama mtu yeyote atamuua mtu mwingine, ni lazima auawe. 18 Mtu yeyote auaye mnyama wa mtu mwingine lazima afidie, uhai kwa uhai. 19 Ikiwa mtu yeyote atamjeruhi jirani yake, chochote alichomtenda naye atatendewa: 20 iwapo amemvunja mfupa atavunjwa mfupa, jicho kwa jicho, jino kwa jino. Kama alivyomjeruhi mwenzake, vivyo hivyo ndivyo atakavyojeruhiwa. 21 Yeyote auaye mnyama wa mtu lazima alipe fidia, lakini yeyote auaye mtu, lazima auawe. 22 Mtakuwa na sheria hiyo hiyo kwa mgeni na kwa mzawa. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.’ ”
23 Kisha Musa akasema na Waisraeli, nao wakamchukua yule aliyekufuru nje ya kambi na kumpiga mawe. Waisraeli wakafanya kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa.