5
Wanafunzi wa kwanza wa Isa
(Mathayo 4:18-22; Marko 1:16-20; Yohana 1:35-51)
Siku moja Isa alipokuwa amesimama karibu na Ziwa la Genesareti*yaani Bahari ya Galilaya, watu wengi walimsonga ili wapate kusikia neno la Mungu. Akaona mashua mbili ukingoni mwa ziwa, zikiwa zimeachwa hapo na wavuvi waliokuwa wanaosha nyavu zao. Akaingia katika mojawapo ya hizo mashua ambayo ilikuwa ya Simoni, akamwomba aisogeze ndani ya maji kidogo kutoka ufuoni. Kisha akaketi na kufundisha watu akiwa mle ndani ya mashua.
Alipomaliza kunena, akamwambia Simoni, “Sasa peleka mashua hadi kilindini kisha mshushe nyavu zenu mkavue samaki.”
Simoni akamjibu, “BwanaWale ambao hawakumfahamu Isa kuwa Masihi walimwita “Bwana” kwa heshima ya kawaida., tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha na hatukuvua chochote. Lakini, kwa neno lako nitazishusha nyavu.”
Nao walipozishusha nyavu zao, wakavua samaki wengi sana, nyavu zao zikajaa zikaanza kukatika. Wakawaashiria wavuvi wenzao kwenye ile mashua nyingine ili waje kuwasaidia. Wakaja, wakajaza mashua zote mbili samaki hata zikaanza kuzama.
Simoni Petro alipoona haya yaliyotukia, alianguka miguuni pa Isa na kumwambia, “Bwana, ondoka kwangu. Mimi ni mtu mwenye dhambi!” Kwa kuwa yeye na wavuvi wenzake walikuwa wameshangazwa sana na wingi wa samaki waliokuwa wamepata. 10 Vivyo hivyo wenzake Simoni, yaani Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, walishangazwa pia.
Ndipo Isa akamwambia Simoni, “Usiogope, tangu sasa utakuwa mvuvi wa watu.” 11 Hivyo wakasogeza mashua zao hadi ufuoni mwa bahari, wakaacha kila kitu na kumfuata.
Isa amtakasa mtu mwenye ukoma
(Mathayo 8:1-4; Marko 1:40-45)
12 Ikawa siku moja Isa alipokuwa katika mji fulani, mtu mmoja mwenye ukoma mwili mzima akamjia. Alipomwona Isa, alianguka chini hadi uso wake ukagusa ardhi, akamsihi akisema, “Bwana, ukitaka, unaweza kunitakasa.”
13 Isa akanyoosha mkono wake, akamgusa yule mtu, akamwambia, “Nataka. Takasika!” Na mara ukoma wake ukatakasika.
14 Isa akamwagiza akisema, “Usimwambie mtu yeyote, bali nenda ukajioneshe kwa kuhani na ukatoe sadaka alizoagiza Musa kwa utakaso wako, ili kuwa ushuhuda kwao.”
15 Lakini habari zake Isa zikazidi sana kuenea kotekote kuliko wakati mwingine wowote. Makundi makubwa ya watu walikuwa wakikusanyika ili kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao. 16 Lakini mara kwa mara Isa alijitenga nao ili kwenda mahali pa faragha kuomba.
Isa amponya mtu aliyepooza
(Mathayo 9:1-8; Marko 2:1-12)
17 Siku moja Isa alipokuwa akifundisha, MafarisayoKundi la kidini la Wayahudi; walifuata Torati kwa dhati, hasa maagizo kuhusu utakaso. Pia waliamini katika malaika, ufufuo wa wafu, na kuja kwa Masihi ambaye atarejesha ufalme wa Daudi na ukuu wa taifa la Israeli. na walimu wa Torati, waliokuwa wametoka kila kijiji cha Galilaya na kutoka Yudea na Yerusalemu, walikuwa wameketi huko. Nao uweza wa Mwenyezi Mungu ulikuwa juu yake kuponya wagonjwa. 18 Wakaja watu wamembeba mgonjwa aliyepooza kwenye mkeka. Wakajaribu kumwingiza ndani ili wamweke mbele ya Isa. 19 Walipokuwa hawawezi kufanya hivyo kwa sababu ya umati wa watu, wakapanda juu ya paa, wakaondoa baadhi ya matofali, wakamteremsha yule mgonjwa kwa mkeka wake hadi katikati ya umati ule pale mbele ya Isa.
20 Isa alipoiona imani yao, akamwambia yule mgonjwa, “Rafiki, dhambi zako zimesamehewa.”
21 Mafarisayo na wale walimu wa Torati wakaanza kuuliza, “Ni nani mtu huyu anayesema maneno ya kukufuru? Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake?”
22 Isa akijua mawazo yao akawauliza, “Kwa nini mnawaza hivyo mioyoni mwenu? 23 Je, ni lipi lililo rahisi zaidi, kumwambia, ‘Umesamehewa dhambi zako,’ au kusema, ‘Inuka, uende’? 24 Lakini ili mpate kujua kwamba Mwana wa Adamu anayo mamlaka duniani kusamehe dhambi.” Akamwambia yule aliyepooza, “Nakuambia, inuka, chukua mkeka wako, uende nyumbani mwako.” 25 Mara yule mtu aliyekuwa amepooza akasimama mbele yao wote, akachukua mkeka wake, akaenda zake nyumbani, huku akimtukuza Mungu. 26 Kila mmoja akashangaa na kumtukuza Mungu. Wakajawa na hofu ya Mungu, wakasema, “Leo tumeona mambo ya ajabu.”
Isa amwita Lawi
(Mathayo 9:9-13; Marko 2:13-17)
27 Baada ya haya, Isa alitoka na kumwona mtoza ushuru mmoja jina lake Lawi akiwa amekaa forodhani, mahali pake pa kutoza ushuru. Akamwambia, “Nifuate.” 28 Naye Lawi akaacha kila kitu, akaondoka, akamfuata.
29 Kisha Lawi akamfanyia Isa karamu kubwa nyumbani mwake, nao umati mkubwa wa watoza ushuru na watu wengine walikuwa wakila pamoja nao. 30 Lakini Mafarisayo na walimu wa Torati waliokuwa wa dhehebu lao wakawalalamikia wanafunzi wa Isa, wakisema, “Mbona mnakula na kunywa pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi?”
31 Isa akawajibu, “Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio wagonjwa. 32 Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi wapate kutubu.”
Isa aulizwa kuhusu kufunga
(Mathayo 9:14-17; Marko 2:18-22)
33 Wakamwambia Isa, “Wanafunzi wa Yahya na wa Mafarisayo mara kwa mara hufunga na kuomba, lakini wanafunzi wako wanaendelea kula na kunywa.”
34 Isa akawajibu, “Je, mnaweza kuwafanya wageni wa bwana arusi kufunga wakati yuko pamoja nao? 35 Lakini wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kwao. Hapo ndipo watakapofunga.”
36 Isa akawapa mfano huu, akawaambia: “Hakuna mtu achanaye kiraka kwenye nguo mpya na kukishonea kwenye nguo iliyochakaa. Akifanya hivyo, atakuwa amechana nguo mpya, na kile kiraka hakitalingana na ile nguo iliyochakaa. 37 Hakuna mtu awekaye divai mpya kwenye viriba vikuukuu. Akifanya hivyo, hiyo divai mpya itavipasua hivyo viriba, nayo yote itamwagika. 38 Divai mpya lazima iwekwe kwenye viriba vipya. 39 Wala hakuna mtu anayependelea divai mpya baada ya kunywa divai ya zamani, bali husema, ‘Ile ya zamani ni nzuri zaidi.’ ”

*5:1 yaani Bahari ya Galilaya

5:5 Wale ambao hawakumfahamu Isa kuwa Masihi walimwita “Bwana” kwa heshima ya kawaida.

5:17 Kundi la kidini la Wayahudi; walifuata Torati kwa dhati, hasa maagizo kuhusu utakaso. Pia waliamini katika malaika, ufufuo wa wafu, na kuja kwa Masihi ambaye atarejesha ufalme wa Daudi na ukuu wa taifa la Israeli.