6
Isa ni Bwana wa Sabato
(Mathayo 12:1-8; Marko 2:23-28)
Ikawa siku moja ya Sabato Isa alikuwa akipita katika mashamba ya nafaka, nao wanafunzi wake wakaanza kuvunja masuke ya nafaka, wakayafikicha kwa mikono yao na kula punje zake. Baadhi ya Mafarisayo wakawauliza, “Mbona mnafanya mambo yasiyo halali kufanywa siku ya Sabato?”
Isa akawajibu, “Je, ninyi hamjasoma alivyofanya Daudi wakati yeye na wenzake walikuwa na njaa? Aliingia ndani ya nyumba ya Mungu, akaichukua na kuila ile mikate iliyowekwa wakfu, ambayo ni halali kuliwa na makuhani tu. Naye pia akawapa wenzake.” Kisha Isa akawaambia, “Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.”
Isa amponya mtu aliyepooza mkono
(Mathayo 12:9-14; Marko 3:1-6)
Ikawa siku nyingine ya Sabato, Isa aliingia ndani ya sinagogi*Nyumba ya ibada na mafunzo. na akawa anafundisha. Huko palikuwa na mtu ambaye mkono wake wa kuume ulikuwa umepooza. Mafarisayo na walimu wa Torati walikuwa wakitafuta sababu ya kumshtaki Isa. Kwa hivyo wakawa wanamwangalia sana ili waone kama ataponya katika siku ya Sabato. Lakini Isa alijua mawazo yao, hivyo akamwambia yule mtu mwenye mkono uliopooza, “Inuka usimame mbele ya watu wote.” Hivyo yule mtu akainuka, akasimama mbele yao wote.
Ndipo Isa akawaambia wale walimu wa Torati na Mafarisayo, “Nawauliza ninyi, ni lipi lililo halali siku ya Sabato? Ni kutenda mema au kutenda mabaya? Ni kuokoa maisha au kuyaangamiza?”
10 Akawatazama watu wote waliokuwepo, kisha akamwambia yule mtu, “Nyoosha mkono wako!” Akaunyoosha, na mkono wake ukawa umeponywa kabisa. 11 Wale wakuu wakakasirika sana, wakashauriana wao kwa wao ni nini watakachomtendea Isa.
Isa achagua mitume kumi na wawili
(Mathayo 10:1-4; Marko 3:13-19)
12 Ikawa katika siku hizo Isa alienda mlimani kuomba, akakesha usiku kucha akimwomba Mungu. 13 Kulipopambazuka, akawaita wanafunzi wake, naye akachagua kumi na wawili, ambao pia aliwaita mitume:
 
14 Simoni (aliyemwita Petro) na Andrea nduguye,
Yakobo,
Yohana,
Filipo,
Bartholomayo,
15 Mathayo,
Tomaso,
Yakobo mwana wa Alfayo,
Simoni aliyeitwa ZeloteWazelote walikuwa kikundi cha Kiyahudi wenye imani kali waliompinga Kaisari na utawala wa Rumi.,
16 Yuda mwana wa Yakobo,
na Yuda Iskariote, aliyekuwa msaliti.
Isa afundisha na kuponya wagonjwa
(Mathayo 4:23-25)
17 Akashuka pamoja nao, akasimama mahali penye uwanja tambarare. Hapo palikuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wake na umati mkubwa wa watu kutoka sehemu zote za Yudea, kutoka Yerusalemu, na kutoka pwani ya Tiro na Sidoni. 18 Walikuwa wamekuja kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao. Wale waliokuwa wakiteswa na pepo wachafu akawaponya. 19 Watu wote walikuwa wanajitahidi kumgusa kwa sababu nguvu zilikuwa zikimtoka na kuwaponya wote.
Baraka na laana
(Mathayo 5:1-12)
20 Akawatazama wanafunzi wake, akasema:
“Mmebarikiwa ninyi mlio maskini,
kwa sababu ufalme wa Mungu ni wenu.
21 Mmebarikiwa ninyi mlio na njaa sasa,
kwa sababu mtashibishwa.
Mmebarikiwa ninyi mnaolia sasa,
kwa sababu mtacheka.
22 Mmebarikiwa ninyi, watu watakapowachukia,
watakapowatenga na kuwatukana
na kulikataa jina lenu kama neno ovu,
kwa ajili ya Mwana wa Adamu.
23 “Furahini na kurukaruka kwa shangwe, kwa sababu thawabu yenu ni kubwa mbinguni, kwa kuwa hivyo ndivyo baba zao walivyowatenda manabii.
24 “Lakini ole wenu ninyi mlio matajiri,
kwa sababu mmekwisha kupokea faraja yenu.
25 Ole wenu ninyi mlioshiba sasa,
maana mtaona njaa.
Ole wenu ninyi mnaocheka sasa,
maana mtaomboleza na kulia.
26 Ole wenu watu watakapowasifu,
kwani ndivyo baba zao walivyowasifu
manabii wa uongo.
Wapendeni adui zenu
(Mathayo 5:38-48)
27 “Lakini nawaambia ninyi mnaonisikia: Wapendeni adui zenu. Watendeeni mema wanaowachukia. 28 Wabarikini wale wanaowalaani, waombeeni wale wanaowatendea mabaya. 29 Kama mtu akikupiga shavu moja, mgeuzie na la pili pia. Mtu akikunyang’anya koti lako, usimzuie kuchukua joho pia. 30 Mpe kila akuombaye, na kama mtu akichukua mali yako usitake akurudishie. 31 Watendeeni wengine kama ambavyo mngetaka wawatendee ninyi.
32 “Mkiwapenda tu wale wanaowapenda, mwapata sifa gani? Hata wenye dhambi huwapenda wale wanaowapenda. 33 Tena mkiwatendea mema wale tu wanaowatendea ninyi mema, mwapata sifa gani? Hata wenye dhambi hufanya vivyo hivyo. 34 Tena mnapowakopesha wale tu mnaotegemea wawalipe, mwapata sifa gani? Hata wenye dhambi huwakopesha wenye dhambi wenzao wakitarajia kulipwa mali yao yote. 35 Lakini wapendeni adui zenu, watendeeni mema, wakopesheni bila kutegemea kurudishiwa mlichokopesha. Ndipo thawabu yenu itakapokuwa kubwa, nanyi mtakuwa wana wa Aliye Juu Sana, kwa sababu yeye ni mwema kwa watu wasio na shukrani na kwa wale waovu. 36 Kuweni na huruma, kama BabaJina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi. yenu alivyo na huruma.
Kuwahukumu wengine
(Mathayo 7:1-5)
37 “Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa. Msilaumu, nanyi hamtalaumiwa. Sameheni, nanyi mtasamehewa. 38 Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa. Kipimo cha kujaa na kushindiliwa na kusukwasukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile mpimacho, ndicho mtakachopimiwa.”
39 Pia akawapa mfano akasema, “Je, kipofu aweza kumwongoza kipofu? Je, wote wawili hawatatumbukia shimoni? 40 Mwanafunzi hawezi kumzidi mwalimu wake, ila yule aliyehitimu aweza kuwa kama mwalimu wake.
41 “Mbona unatazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, wala huoni boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe? 42 Utawezaje kumwambia ndugu yako, ‘Ndugu yangu, acha nitoe kibanzi kilicho ndani ya jicho lako,’ wakati wewe mwenyewe huoni boriti iliyo ndani ya jicho lako? Ewe mnafiki, ondoa boriti ndani ya jicho lako kwanza, ndipo utaweza kuona dhahiri jinsi ya kuondoa kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako.
Mti na matunda yake
(Mathayo 12:33-35)
43 “Hakuna mti mzuri uzaao matunda mabaya, wala hakuna mti mbaya uzaao matunda mazuri. 44 Kila mti hujulikana kwa matunda yake. Kwa maana watu hawachumi tini kwenye miiba, wala zabibu kwenye michongoma. 45 Vivyo hivyo mtu mwema hutoa mambo mema kutoka hazina ya moyo wake, naye mtu mwovu hutoa mambo maovu kutoka hazina ya moyo wake. Kwa kuwa mtu hunena kwa kinywa chake yale yaliyoujaza moyo wake.
Mjenzi mwenye busara na mjenzi mpumbavu
(Mathayo 7:24-27)
46 “Kwa nini mnaniita, ‘Bwana, Bwana,’ nanyi hamfanyi ninayowaambia? 47 Nitawaonesha jinsi alivyo mtu yule anayekuja kwangu na kusikia maneno yangu na kuyatenda. 48 Yeye ni kama mtu aliyejenga nyumba, akachimba chini sana, na kuweka msingi kwenye mwamba. Mafuriko yalipokuja, mkondo wa maji ukaipiga ile nyumba, lakini haikutikisika, kwa sababu ilikuwa imejengwa vizuri. 49 Lakini yeye anayesikia maneno yangu wala asiyatende, ni kama mtu aliyejenga nyumba juu ya ardhi bila kuweka msingi. Mafuriko yalipoikumba nyumba ile, ikaanguka mara na kubomoka kabisa.”

*6:6 Nyumba ya ibada na mafunzo.

6:15 Wazelote walikuwa kikundi cha Kiyahudi wenye imani kali waliompinga Kaisari na utawala wa Rumi.

6:36 Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi.