14
Yahya akatwa kichwa
(Marko 6:14-29; Luka 9:7-9)
Wakati huo, Mfalme Herode, mtawala wa Galilaya, alisikia habari za Isa, akawaambia watumishi wake, “Huyu ni Yahya; amefufuka kutoka kwa wafu! Hii ndiyo sababu nguvu za kutenda miujiza zinafanya kazi ndani yake.”
Herode alikuwa amemkamata Yahya, akamfunga na kumweka gerezani kwa sababu ya Herodia, mke wa Filipo, ndugu yake, kwa kuwa Yahya alikuwa amemwambia Herode: “Si halali kwako kuwa na huyo mwanamke.” Herode alitaka sana kumuua Yahya, lakini akaogopa watu, kwa maana walimtambua kuwa ni nabii.
Katika siku ya kuadhimisha sikukuu ya kuzaliwa kwa Herode, binti Herodia alicheza mbele ya watu waliohudhuria. Alimfurahisha Herode sana, kiasi kwamba aliahidi kwa kiapo kumpa huyo binti chochote angeomba. Huyo binti, akiwa amechochewa na mama yake, akasema, “Nipe kichwa cha Yahya kwenye sinia.” Mfalme alisikitika, lakini kwa sababu ya viapo alivyoapa mbele ya wageni, akaamuru kwamba apatiwe ombi lake. 10 Hivyo akaagiza Yahya akatwe kichwa mle gerezani. 11 Kichwa chake kikaletwa kwenye sinia, akapewa yule binti, naye akampelekea mama yake. 12 Wanafunzi wa Yahya wakaja na kuuchukua mwili wake, wakamzika. Kisha wakaenda wakamwambia Isa.
Isa alisha wanaume 5,000
(Marko 6:30-44; Luka 9:10-17; Yohana 6:1-14)
13 Isa aliposikia yaliyokuwa yametukia, aliondoka kwa chombo akaenda mahali pasipo na watu ili awe peke yake. Lakini watu walipopata habari, wakamfuata kwa miguu kupitia nchi kavu kutoka miji. 14 Isa alipofika kando ya bahari, aliona makundi makubwa ya watu, akawahurumia na akawaponya wagonjwa wao.
15 Ilipofika jioni, wanafunzi wake walienda kwake, wakamwambia, “Mahali hapa ni nyikani, na muda sasa umekwisha. Waage makundi ya watu ili waende zao vijijini wakajinunulie chakula.”
16 Isa akawaambia, “Hakuna sababu ya wao kuondoka. Ninyi wapeni chakula.”
17 Wakamjibu, “Tuna mikate mitano na samaki wawili tu.”
18 Akawaambia, “Nileteeni hivyo vitu hapa.” 19 Isa akaagiza umati wa watu wakae chini kwenye nyasi. Akaichukua ile mikate mitano na wale samaki wawili, akainua macho yake akatazama mbinguni, akavibariki na kuimega ile mikate. Kisha akawapa wanafunzi, nao wanafunzi wakawagawia ule umati. 20 Wote wakala, wakashiba. Nao wanafunzi wakakusanya vipande vilivyosalia, wakajaza vikapu kumi na viwili. 21 Idadi ya watu waliokula walikuwa wanaume wapatao elfu tano, bila kuhesabu wanawake na watoto.
Isa atembea juu ya maji
(Marko 6:45-52; Yohana 6:16-21)
22 Mara Isa akawaambia wanafunzi wake waingie katika mashua wamtangulie kwenda ng’ambo ya bahari, wakati yeye alikuwa akiaga ule umati. 23 Baada ya kuwaaga, akaenda zake mlimani peke yake kuomba. Jioni ilipofika, Isa alikuwa huko peke yake. 24 Wakati huo ile mashua ilikuwa mbali kutoka nchi kavu ikisukwasukwa na mawimbi, kwa sababu upepo ulikuwa wa mbisho.
25 Wakati wa zamu ya nne ya usiku*yaani kati ya saa tisa na saa kumi na mbili asubuhi, Isa akawaendea wanafunzi wake akiwa anatembea juu ya maji. 26 Wanafunzi wake walipomwona akitembea juu ya maji, waliingiwa na hofu kuu, wakasema, “Ni mzimu.” Wakapiga yowe kwa kuogopa.
27 Lakini mara Isa akasema nao, akawaambia, “Jipeni moyo! Ni mimi. Msiogope.”
28 Petro akamjibu, “Bwana Isa, ikiwa ni wewe, niambie nije kwako nikitembea juu ya maji.”
29 Isa akamwambia, “Njoo.”
Basi Petro akatoka kwenye chombo, akatembea juu ya maji kumwelekea Isa. 30 Lakini alipoona upepo mkali aliingiwa na hofu, naye akaanza kuzama, akapaza sauti na kusema, “Bwana, niokoe!”
31 Mara Isa akaunyoosha mkono wake na kumshika, akamwambia, “Wewe mwenye imani haba, kwa nini uliona shaka?”
32 Nao walipoingia ndani ya mashua, upepo ukakoma. 33 Ndipo wote waliokuwa ndani ya ile mashua wakamwabudu Isa, wakisema, “Hakika, wewe ndiwe Mwana wa MunguYaani Mwana wa asili moja na Mwenyezi Mungu (Yohana 1:1-2), wa kiroho, bali si wa kimwili..”
Isa awaponya wagonjwa Genesareti
(Marko 6:53-56)
34 Walipokwisha kuvuka, wakafika nchi ya Genesareti. 35 Watu wa eneo lile walipomtambua Isa, walipeleka habari sehemu zote za jirani. Watu wakamletea wagonjwa wao wote, 36 wakamsihi awaruhusu wagonjwa waguse tu pindo la vazi lake, nao wote waliomgusa, wakaponywa.

*14:25 yaani kati ya saa tisa na saa kumi na mbili asubuhi

14:33 Yaani Mwana wa asili moja na Mwenyezi Mungu (Yohana 1:1-2), wa kiroho, bali si wa kimwili.