15
Mapokeo ya wazee
(Marko 7:1-13)
1 Ndipo baadhi ya Mafarisayo*Kundi la kidini la Wayahudi; walifuata Torati kwa dhati, hasa maagizo kuhusu utakaso. Pia waliamini katika malaika, ufufuo wa wafu, na kuja kwa Masihi ambaye atarejesha ufalme wa Daudi na ukuu wa taifa la Israeli. na walimu wa Torati wakamjia Isa kutoka Yerusalemu na kumuuliza, 2 “Mbona wanafunzi wako wanakiuka mapokeo ya wazee? Kwa maana wao hawanawi mikono yao kabla ya kula!”
3 Isa akawajibu, “Mbona ninyi mnavunja amri ya Mungu kwa ajili ya mapokeo yenu? 4 Kwa maana Mungu alisema, ‘Waheshimu baba yako na mama yako,’ na, ‘Yeyote amtukanaye baba yake au mama yake, na auawe.’ 5 Lakini ninyi mwafundisha kwamba mtu akimwambia baba yake au mama yake, ‘Kile ambacho ningeweza kukusaidia kimewekwa wakfu kwa Mungu,’ 6 basi hana tena sababu ya kumheshimu baba yake nacho. Basi kwa ajili ya mafundisho yenu mnavunja amri ya Mungu. 7 Ninyi wanafiki! Isaya alikuwa sawa alipotabiri juu yenu kwamba:
8 “ ‘Watu hawa huniheshimu kwa midomo yao,
lakini mioyo yao iko mbali nami.
9 Huniabudu bure;
nayo mafundisho yao
ni maagizo ya wanadamu tu.’ ”
Vitu vinavyomnajisi mtu
(Marko 7:14-23)
10 Isa akaita umati wa watu waliokuwa hapo, akawaambia, “Sikilizeni na mwelewe: 11 kinachomfanya mtu kuwa najisi mbele za Mungu si kile kiingiacho kinywani mwake, bali ni kile kitokacho kinywani mwake.”
12 Kisha wanafunzi wake wakamjia na kumuuliza, “Je, unajua kwamba Mafarisayo walichukizwa sana waliposikia yale uliyosema?”
13 Akawajibu, “Kila mmea ambao Baba†Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. yangu wa mbinguni hakuupanda utang’olewa. 14 Waacheni; wao ni viongozi vipofu, wanaoongoza vipofu. Kama kipofu akimwongoza kipofu mwenzake, wote wawili watatumbukia shimoni.”
15 Petro akasema, “Tueleze maana ya huu mfano.”
16 Isa akawauliza, “Je, bado ninyi hamfahamu? 17 Je, hamwelewi kwamba chochote kiingiacho kinywani huenda tumboni, na hatimaye hutolewa nje kikiwa uchafu? 18 Lakini kitokacho kinywani hutoka moyoni, na hiki ndicho kimtiacho mtu unajisi. 19 Kwa maana ndani ya moyo hutoka mawazo mabaya, uuaji, uzinzi, uasherati, wizi, ushahidi wa uongo na masingizio. 20 Haya ndio yamtiayo mtu unajisi; lakini kula bila kunawa mikono hakumtii mtu unajisi.”
Imani ya mwanamke Mkanaani
(Marko 7:24-30)
21 Isa aliondoka mahali pale, akaenda sehemu za Tiro na Sidoni. 22 Mwanamke mmoja Mkanaani aliyeishi sehemu jirani na hizo akaja kwake akilia, akasema, “Nihurumie, Ee Bwana, Mwana wa Daudi‡Ina maana kwamba Isa ni mrithi wa kiti cha enzi cha Mwenyezi Mungu (Zaburi 89:3-4).! Binti yangu amepagawa na pepo mchafu, na anateseka sana.”
23 Lakini Isa hakumjibu neno. Hivyo wanafunzi wake wakamwendea na kumsihi sana, wakisema, “Mwambie aende zake, kwa maana anaendelea kutupigia kelele.”
24 Isa akajibu, “Nimetumwa tu kwa ajili ya kondoo wa Israeli waliopotea.”
25 Lakini yule mwanamke akaja, akapiga magoti mbele ya Isa, akasema, “Bwana, nisaidie!”
26 Isa akajibu, “Si haki kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.”
27 Yule mwanamke akajibu, “Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yanayoanguka kutoka kwa meza za bwana zao.”
28 Ndipo Isa akamwambia, “Mwanamke, imani yako ni kubwa! Iwe kwako kama unavyotaka.” Naye binti yake akapona tangu saa ile.
Isa aponya watu wengi
29 Isa akaondoka na kwenda kando ya Bahari ya Galilaya. Kisha akapanda mlimani, akaketi huko. 30 Umati mkubwa wa watu wakamjia, wakiwaleta vilema, vipofu, viwete, bubu na wengine wengi, wakawaweka miguuni pake; naye akawaponya. 31 Hao watu wakashangaa walipoona bubu wakisema, vilema wakipona, viwete wakitembea na vipofu wakiona, wakamtukuza Mungu wa Israeli.
Isa alisha wanaume 4,000
(Marko 8:1-10)
32 Kisha Isa akawaita wanafunzi wake, akawaambia, “Ninahurumia umati huu wa watu, kwa sababu sasa wamekuwa pamoja nami kwa muda wa siku tatu, na hawana chakula chochote. Nami sipendi kuwaaga watu wakiwa na njaa, wasije wakazimia njiani.”
33 Wanafunzi wake wakasema, “Tutapata wapi mikate ya kutosha kulisha umati mkubwa namna hii, nasi tuko nyikani?”
34 Isa akawauliza, “Mnayo mikate mingapi?”
Wakamjibu, “Tunayo mikate saba na visamaki vichache.”
35 Isa akaagiza watu wote waketi chini. 36 Kisha akachukua ile mikate saba na wale samaki, naye akamshukuru Mungu, akavimega na kuwapa wanafunzi wake, nao wakawapa watu. 37 Wote wakala na kushiba. Baadaye wanafunzi wakakusanya vipande vilivyosalia, wakajaza vikapu saba. 38 Idadi ya watu walikuwa wanaume elfu nne, bila kuhesabu wanawake na watoto.
39 Baada ya kuaga umati wa watu, Isa aliingia katika mashua, akaenda sehemu za Magadani§yaani Magdala katika Galilaya.
*15:1 Kundi la kidini la Wayahudi; walifuata Torati kwa dhati, hasa maagizo kuhusu utakaso. Pia waliamini katika malaika, ufufuo wa wafu, na kuja kwa Masihi ambaye atarejesha ufalme wa Daudi na ukuu wa taifa la Israeli.
†15:13 Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu.
‡15:22 Ina maana kwamba Isa ni mrithi wa kiti cha enzi cha Mwenyezi Mungu (Zaburi 89:3-4).
§15:39 yaani Magdala katika Galilaya