3
Viongozi na manabii wakemewa 
  1 Kisha nikasema,  
“Sikilizeni enyi viongozi wa Yakobo,  
enyi watawala wa nyumba ya Israeli.  
Je, hampaswi kujua hukumu,   
 2 ninyi mnaochukia mema  
na kupenda maovu;  
ninyi mnaowachuna watu wangu ngozi  
na kuondoa nyama kwenye mifupa yao;   
 3 ninyi mnaokula nyama ya watu wangu,  
mnaowachuna ngozi  
na kuvunja mifupa yao vipande vipande;  
mnaowakatakata kama nyama  
ya kuwekwa kwenye sufuria  
na kama nyama  
ya kuwekwa kwenye chungu?”   
 4 Kisha watamlilia Mwenyezi Mungu,  
lakini hatawajibu.  
Wakati huo atawaficha uso wake  
kwa sababu ya uovu waliotenda.   
 5 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu:  
“Kuhusu manabii wanaowapotosha watu wangu,  
mtu akiwalisha,  
wanatangaza ‘amani’;  
kama hakufanya hivyo,  
wanaandaa kupigana vita dhidi yake.   
 6 Kwa hiyo usiku utawajieni, msiweze kuwa na maono,  
na giza, msiweze kubashiri.  
Jua litawachwea manabii hao,  
nao mchana utakuwa giza kwao.   
 7 Waonaji wataaibika  
na waaguzi watafedheheka.  
Wote watafunika nyuso zao  
kwa sababu hakuna jibu litokalo kwa Mungu.”   
 8 Lakini mimi nimejazwa nguvu,  
nimejazwa Roho wa Mwenyezi Mungu,  
haki na uweza,  
kumtangazia Yakobo kosa lake,  
na Israeli dhambi yake.   
 9 Sikieni hili, enyi viongozi wa nyumba ya Yakobo,  
enyi watawala wa nyumba ya Israeli,  
mnaodharau haki  
na kupotosha kila lililo sawa;   
 10 mnaojenga Sayuni kwa kumwaga damu  
na Yerusalemu kwa uovu.   
 11 Viongozi wake wanahukumu kwa rushwa,  
na makuhani wake wanafundisha kwa malipo,  
nao manabii wake wanatabiri kwa fedha.  
Hata hivyo wanamwegemea Mwenyezi Mungu na kusema,  
“Je, Mwenyezi Mungu si yumo miongoni mwetu?  
Hakuna maafa yatakayotupata.”   
 12 Kwa ajili yenu,  
Sayuni italimwa kama shamba,  
Yerusalemu itakuwa lundo la kokoto,  
na kilima cha Hekalu  
kitakuwa kichuguu  
kilichofunikwa na vichaka.