4
Mlima wa Mwenyezi Mungu 
 (Isaya 2:2-4)  
 1 Katika siku za mwisho  
mlima wa Hekalu la Mwenyezi Mungu utaimarishwa  
kama mlima mkuu miongoni mwa milima yote;  
utainuliwa juu ya vilima,  
na watu wa mataifa watamiminika humo.   
 2 Mataifa mengi yatakuja na kusema,  
“Njooni, twendeni kwenye mlima wa Mwenyezi Mungu,  
kwenye nyumba ya Mungu wa Yakobo.  
Atatufundisha njia zake,  
ili tuweze kuenenda katika mapito yake.”  
Torati itatoka Sayuni,  
neno la Mwenyezi Mungu litatoka Yerusalemu.   
 3 Atahukumu kati ya mataifa mengi,  
na ataamua migogoro ya mataifa  
yenye nguvu na yaliyo mbali.  
Watafua panga zao ziwe majembe,  
na mikuki yao kuwa miundu ya kukata matawi.  
Taifa halitainua upanga dhidi ya taifa jingine,  
wala hawatajifunza vita tena.   
 4 Kila mtu ataketi chini ya mzabibu wake  
na chini ya mtini wake,  
wala hakuna mtu atakayewaogopesha,  
kwa kuwa Mwenyezi Mungu,  
Mungu wa majeshi ya mbinguni amesema.   
 5 Mataifa yote yanaweza kutembea  
katika jina la miungu yao;  
sisi tutatembea katika jina la Mwenyezi Mungu,  
Mungu wetu milele na milele.   
Mpango wa Mwenyezi Mungu 
  6 “Katika siku hiyo,” asema Mwenyezi Mungu,  
“nitawakusanya walemavu;  
nitawakusanya walio uhamishoni  
na wale niliowahuzunisha.   
 7 Nitawafanya walemavu kuwa mabaki,  
wale waliofukuzwa kuwa taifa lenye nguvu.  
Mwenyezi Mungu atawatawala katika Mlima Sayuni  
kuanzia siku hiyo na hata milele.   
 8 Lakini kwako wewe, ee mnara wa ulinzi wa kundi,  
ee ngome ya Binti Sayuni,  
milki ya awali itarudishwa kwako,  
ufalme utakuja kwa Binti Yerusalemu.”   
 9 Kwa nini sasa unalia kwa nguvu:  
kwani huna mfalme?  
Je, mshauri wako amekufa, hata maumivu yakukamate  
kama ya mwanamke  
aliye na uchungu wa kuzaa?   
 10 Gaagaa kwa uchungu, ee Binti Sayuni,  
kama mwanamke mwenye uchungu wa kuzaa,  
kwa kuwa sasa ni lazima uuache mji  
ukapige kambi uwanjani.  
Utaenda Babeli;  
huko utaokolewa.  
Huko Mwenyezi Mungu atakukomboa  
kutoka mikononi mwa adui zako.   
 11 Lakini sasa mataifa mengi  
yamekusanyika dhidi yako.  
Wanasema, “Mwache anajisiwe,  
macho yetu na yatazame Sayuni kwa furaha!”   
 12 Lakini hawayajui  
mawazo ya Mwenyezi Mungu;  
hawauelewi mpango wake,  
yeye awakusanyaye kama miganda  
kwenye sakafu ya kupuria.   
 13 “Inuka upure, ee Binti Sayuni,  
kwa kuwa nitakupa pembe za chuma;  
nitakupa kwato za shaba  
na utavunja vipande vipande mataifa mengi.”  
Utatoa mapato yao waliopata kwa udanganyifu kwa Mwenyezi Mungu,  
utajiri wao kwa Bwana wa dunia yote.