5
Mtawala aliyeahidiwa kutoka Bethlehemu
1 Panga majeshi yako, ee mji wa majeshi,
kwa kuwa kuzingirwa kumepangwa dhidi yetu.
Watampiga mtawala wa Israeli
shavuni kwa fimbo.
2 “Lakini wewe, Bethlehemu Efrata,
ingawa u mdogo miongoni mwa koo za Yuda,
kutoka kwako atatokea kwa ajili yangu
yeye atakayekuwa mtawala katika Israeli,
ambaye asili yake ni kutoka zamani,
kutoka milele.”
3 Kwa hiyo Israeli utaachwa
hadi mwanamke aliye na uchungu atakapozaa mwana,
na ndugu zake wengine warudi
kujiunga na Waisraeli.
4 Atasimama na kulichunga kundi lake
katika nguvu ya Mwenyezi Mungu,
katika utukufu wa jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wake.
Nao wataishi kwa usalama, kwa kuwa wakati huo
ukuu wake utaenea hadi miisho ya dunia.
5 Naye atakuwa amani yao.
Ukombozi na uharibifu
Mwashuru atakapovamia nchi yetu
na kupita katika ngome zetu,
tutawainua wachungaji saba dhidi yake,
hata viongozi wanane wa watu.
6 Wataitawala nchi ya Ashuru kwa upanga,
nchi ya Nimrodi kwa upanga.
Atatuokoa kutoka kwa Mwashuru
atakapoivamia nchi yetu
na kuingia katika mipaka yetu.
7 Mabaki ya Yakobo yatakuwa
katikati ya mataifa mengi
kama umande kutoka kwa Mwenyezi Mungu,
kama manyunyu juu ya majani,
ambayo hayamngoji mtu
wala kukawia kwa mwanadamu.
8 Mabaki ya Yakobo yatakuwa miongoni mwa mataifa,
katikati ya mataifa mengi,
kama simba miongoni mwa wanyama wa msituni,
kama mwana simba miongoni
mwa makundi ya kondoo,
ambaye anaumiza vibaya na kuwararua
kila anapopita katikati yao,
wala hakuna awezaye kuokoa.
9 Mkono wako utainuliwa juu kwa ushindi juu ya watesi wako,
nao adui zako wote wataangamizwa.
10 “Katika siku ile,” asema Mwenyezi Mungu,
“nitaangamiza farasi wenu kati yenu,
na kubomoa magari yenu ya vita.
11 Nitaiangamiza miji ya nchi yenu,
na kuziangusha chini ngome zenu zote.
12 Nitaangamiza uchawi wenu,
na hamtapiga tena ramli.
13 Nitaangamiza sanamu zenu,
na mawe yenu ya ibada yatoke kati yenu;
hamtasujudia tena
kazi ya mikono yenu.
14 Nitang’oa nguzo za Ashera kati yenu,
na kubomoa miji yenu.
15 Nitalipiza kisasi kwa hasira na ghadhabu,
kwa mataifa ambayo hayajanitii.”