2
Isa amponya mtu aliyepooza
(Mathayo 9:1-8; Luka 5:17-26)
1 Baada ya siku kadhaa Isa alirudi Kapernaumu, watu wakasikia kwamba yupo nyumbani. 2 Watu wengi wakakusanyika, kiasi kwamba hapakubaki nafasi yoyote hata mlangoni! Naye akawahubiria Neno. 3 Ndipo baadhi ya watu wakaja wakamletea Isa mtu aliyepooza, akiwa amebebwa na watu wanne. 4 Kwa kuwa hawakuweza kumfikisha kwa Isa kwa sababu ya umati wa watu, walitoboa tundu kwenye paa juu ya mahali Isa alikuwa, wakamshusha mtu aliyepooza akiwa amelalia mkeka wake. 5 Isa alipoiona imani yao, alimwambia yule mtu aliyepooza, “Mwanangu, dhambi zako zimesamehewa.”
6 Basi baadhi ya walimu wa Torati waliokuwa wameketi pale wakawaza mioyoni mwao, 7 “Kwa nini mtu huyu anasema hivi? Huyu anakufuru! Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake?”
8 Mara moja Isa akatambua rohoni mwake kile walichokuwa wanawaza mioyoni mwao, naye akawaambia, “Kwa nini mnawaza hivyo mioyoni mwenu? 9 Je, ni lipi lililo rahisi zaidi: kumwambia huyu aliyepooza, ‘Umesamehewa dhambi zako,’ au kusema, ‘Inuka, uchukue mkeka wako, uende’? 10 Lakini ili mpate kujua kwamba Mwana wa Adamu anayo mamlaka duniani ya kusamehe dhambi”: Isa akamwambia yule aliyepooza, 11 “Nakuambia, inuka, chukua mkeka wako, uende nyumbani kwako.” 12 Yule mtu aliyekuwa amepooza akasimama, akachukua mkeka wake, akatembea machoni pao wote! Jambo hili likawashangaza wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, “Hatujapata kuona jambo kama hili kamwe!”
Isa amwita Lawi
(Mathayo 9:9-13; Luka 5:27-32)
13 Isa akaenda tena kandokando ya Bahari ya Galilaya. Umati mkubwa wa watu wakamfuata, naye akaanza kuwafundisha. 14 Alipokuwa akitembea, akamwona Lawi mwana wa Alfayo ameketi forodhani mahali pa kutoza ushuru. Isa akamwambia, “Nifuate.” Naye Lawi akaondoka, akamfuata Isa.
15 Isa alipokuwa ameketi akila chakula nyumbani mwa Lawi, watoza ushuru wengi na wenye dhambi walikuwa wakila pamoja naye na wanafunzi wake, kwa maana ni watu wengi waliokuwa wakimfuata. 16 Walimu wa Torati waliokuwa Mafarisayo*Kundi la kidini la Wayahudi; walifuata Torati kwa dhati, hasa maagizo kuhusu utakaso. Pia waliamini katika malaika, ufufuo wa wafu, na kuja kwa Masihi ambaye atarejesha ufalme wa Daudi na ukuu wa taifa la Israeli. walipomwona akila pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi, wakawauliza wanafunzi wake: “Mbona Isa anakula na watoza ushuru na wenye dhambi?”
17 Isa aliposikia haya akawaambia, “Watu wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio wagonjwa. Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.”
Isa aulizwa kuhusu kufunga
(Mathayo 9:14-17; Luka 5:33-39)
18 Basi wanafunzi wa Yahya pamoja na Mafarisayo walikuwa wakifunga. Watu wakamjia Isa na kumuuliza, “Mbona wanafunzi wa Yahya na wa Mafarisayo hufunga, lakini wanafunzi wako hawafungi?”
19 Isa akawajibu, “Wageni wa bwana arusi wawezaje kufunga wakati angali pamoja nao? Wakati bwana arusi bado yuko pamoja nao, hawawezi kufunga. 20 Lakini wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kwao. Siku hiyo ndipo watakapofunga.
21 “Hakuna mtu ashoneaye kiraka cha nguo mpya kwenye nguo iliyochakaa. Akifanya hivyo, kile kiraka kipya kitachanika kutoka ile nguo iliyochakaa, nayo itachanika zaidi. 22 Wala hakuna mtu awekaye divai mpya kwenye viriba vikuukuu. Akifanya hivyo, ile divai mpya itavipasua hivyo viriba, nayo hiyo divai itamwagika na viriba vitaharibika. Lakini divai mpya huwekwa kwenye viriba vipya.”
Isa ni Bwana wa Sabato
(Mathayo 12:1-8; Luka 6:1-5)
23 Siku moja ya Sabato, Isa pamoja na wanafunzi wake walikuwa wakipita katikati ya mashamba ya nafaka. Walipokuwa wakitembea, wanafunzi wake wakaanza kuvunja masuke. 24 Mafarisayo wakamwambia, “Tazama, mbona wanafanya jambo lisilo halali kufanywa siku ya Sabato?”
25 Isa akawajibu, “Je, hamjasoma alivyofanya Daudi yeye na wenzake walipokuwa na njaa, wakahitaji chakula? 26 Daudi aliingia katika nyumba ya Mungu, Abiathari alipokuwa kuhani mkuu, akaila ile mikate iliyowekwa wakfu, ambayo ni halali kuliwa na makuhani tu. Naye pia akawapa wenzake.”
27 Kisha Isa akawaambia, “Sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu, lakini si mwanadamu kwa ajili ya Sabato. 28 Hivyo, Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.”
*2:16 Kundi la kidini la Wayahudi; walifuata Torati kwa dhati, hasa maagizo kuhusu utakaso. Pia waliamini katika malaika, ufufuo wa wafu, na kuja kwa Masihi ambaye atarejesha ufalme wa Daudi na ukuu wa taifa la Israeli.