3
Isa amponya mtu aliyepooza mkono
(Mathayo 12:9-14; Luka 6:6-11)
1 Isa akaingia tena ndani ya sinagogi*Nyumba ya ibada na mafunzo., na kulikuwa na mtu aliyepooza mkono. 2 Wakawa wanamwangalia waone kama atamponya huyo mtu siku ya Sabato, ili wapate sababu ya kumshtaki. 3 Isa akamwambia yule mtu mwenye mkono uliopooza, “Njoo hapa mbele ya watu wote.”
4 Kisha Isa akawauliza, “Je, ni lipi lililo halali siku ya Sabato: Ni kutenda mema au kutenda mabaya? Ni kuokoa maisha au kuua?” Lakini wao wakanyamaza.
5 Isa akawatazama kwa hasira watu waliomzunguka pande zote, akahuzunika sana kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao. Akamwambia yule mtu mwenye mkono uliopooza, “Nyoosha mkono wako.” Akaunyoosha, nao ukawa umeponywa kabisa! 6 Kisha Mafarisayo wakatoka nje, nao wakaanza kufanya njama ya kumuua Isa wakishirikiana na Maherode†Wafuasi wa Mfalme Herode waliokubaliana na utawala wa Rumi..
Makundi ya watu wamfuata Isa
7 Isa na wanafunzi wake wakaondoka huko, wakaenda baharini, nao umati mkubwa wa watu kutoka Galilaya wakamfuata. 8 Waliposikia mambo yote aliyokuwa akiyafanya, makundi ya watu wakamjia kutoka Yudea, Yerusalemu, Idumaya, na ng’ambo ya Yordani, pamoja na wale wa maeneo ya Tiro na Sidoni. 9 Kwa sababu ya umati mkubwa wa watu, aliwaambia wanafunzi wake watayarishe mashua ndogo kwa ajili yake, ili kuwazuia watu kumsonga. 10 Kwa kuwa alikuwa amewaponya wagonjwa wengi, wale wenye magonjwa walikuwa wanasukumana ili wapate kumgusa. 11 Kila mara pepo wachafu walipomwona, walianguka chini mbele yake na kupiga kelele wakisema, “Wewe ndiwe Mwana wa Mungu‡Yaani Mwana wa asili moja na Mwenyezi Mungu (Yohana 1:1-2), wa kiroho, bali si wa kimwili..” 12 Lakini aliwaonya wasiwaambie wengine kumhusu.
Isa achagua mitume kumi na wawili
(Mathayo 10:1-4; Luka 6:12-16)
13 Isa akapanda mlimani na kuwaita wale aliowataka, nao wakamjia. 14 Akawachagua watu kumi na wawili ambao aliwaita mitume, ili wapate kuwa naye, na awatume kwenda kuhubiri 15 na kuwa na mamlaka ya kutoa pepo wachafu.
16 Hawa ndio wale kumi na wawili aliowachagua:
Simoni (ambaye alimwita Petro);
17 Yakobo mwana wa Zebedayo, na Yohana nduguye (ambao aliwaita Boanerge, maana yake Wana wa Ngurumo);
18 Andrea,
Filipo,
Bartholomayo,
Mathayo,
Tomaso,
Yakobo mwana wa Alfayo,
Thadayo,
Simoni Mkananayo§yaani Mzelote; Wazelote walikuwa kikundi cha Kiyahudi wenye imani kali waliompinga Kaisari na utawala wa Rumi.,
19 na Yuda Iskariote aliyemsaliti Isa.
Isa na Beelzebuli
(Mathayo 12:22-32; Luka 11:14-23)
20 Kisha Isa alipoingia ndani ya nyumba, umati wa watu wakakusanyika tena, kiasi kwamba yeye na wanafunzi wake hawakuweza kula chakula. 21 Ndugu zake walipopata habari wakaja ili kumchukua kwa maana watu walikuwa wakisema, “Amerukwa na akili.”
22 Walimu wa Torati walioteremka kutoka Yerusalemu walisema, “Amepagawa na Beelzebuli*kwa Kiyunani ni Beelzebubu, yaani mkuu wa pepo wachafu! Anatoa pepo wachafu kwa nguvu ya mkuu wa pepo wachafu!”
23 Basi Isa akawaita na kuzungumza nao kwa mifano akasema: “Shetani awezaje kumtoa Shetani? 24 Kama ufalme ukigawanyika dhidi yake wenyewe, ufalme huo hauwezi kusimama. 25 Nayo nyumba ikigawanyika dhidi yake yenyewe, nyumba hiyo haiwezi kusimama. 26 Na kama Shetani akijipinga mwenyewe na awe amegawanyika, hawezi kusimama, bali mwisho wake umetimia. 27 Hakuna mtu yeyote awezaye kuingia kwenye nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuteka nyara mali yake asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu. Ndipo ataweza kuteka nyara mali yake. 28 Amin, nawaambia, watu wataweza kusamehewa dhambi na kufuru zao zote; 29 lakini yeyote anayemkufuru Roho Mtakatifu wa Mungu hatasamehewa kamwe, atakuwa na hatia ya dhambi ya milele.”
30 Isa alisema hivi kwa sababu walikuwa wanasema, “Ana pepo mchafu.”
Mama yake na ndugu zake Isa
(Mathayo 12:46-50; Luka 8:19-21)
31 Kisha wakaja ndugu zake Isa pamoja na mama yake. Wakiwa wamesimama nje, wakamtuma mtu kumwita. 32 Umati wa watu walikuwa wameketi kumzunguka, nao wakamwambia, “Mama yako na ndugu zako wako nje, wanakutafuta.”
33 Akawauliza, “Mama yangu na ndugu zangu ni nani?”
34 Kisha akawatazama wale watu waliokuwa wameketi kumzunguka pande zote, akasema, “Hawa ndio mama yangu na ndugu zangu. 35 Mtu yeyote anayetenda mapenzi ya Mungu, huyo ndiye kaka yangu, na dada yangu, na mama yangu.”
*3:1 Nyumba ya ibada na mafunzo.
†3:6 Wafuasi wa Mfalme Herode waliokubaliana na utawala wa Rumi.
‡3:11 Yaani Mwana wa asili moja na Mwenyezi Mungu (Yohana 1:1-2), wa kiroho, bali si wa kimwili.
§3:18 yaani Mzelote; Wazelote walikuwa kikundi cha Kiyahudi wenye imani kali waliompinga Kaisari na utawala wa Rumi.
*3:22 kwa Kiyunani ni Beelzebubu, yaani mkuu wa pepo wachafu