5
Isa amponya mtu mwenye pepo mchafu
(Mathayo 8:28-34; Luka 8:26-39)
Isa na wanafunzi wake wakafika upande wa pili wa ziwa, wakaingia katika nchi ya Wagerasi. Isa alipotoka kwenye mashua, mara mtu mmoja mwenye pepo mchafu akatoka makaburini, akakutana naye. Mtu huyu aliishi makaburini, wala hakuna aliyeweza kumzuia hata kwa kumfunga minyororo. Kwa kuwa mara kwa mara alikuwa amefungwa minyororo mikononi na miguuni, lakini akaikata hiyo minyororo na kuzivunja zile pingu miguuni mwake. Hapakuwa na mtu yeyote aliyekuwa na nguvu za kumzuia. Usiku na mchana alikuwa makaburini na milimani, akipiga kelele na kujikatakata kwa mawe.
Alipomwona Isa kwa mbali, alimkimbilia, akapiga magoti mbele yake. Akapaza sauti kwa nguvu akisema, “Una nini nami, Isa, Mwana wa Mungu*Yaani Mwana wa asili moja na Mwenyezi Mungu (Yohana 1:1-2), wa kiroho, bali si wa kimwili. Aliye Juu Sana? Ninakusihi kwa jina la Mungu, usinitese!” Kwa kuwa Isa alikuwa amemwambia, “Mtoke mtu huyu, wewe pepo mchafu!”
Isa akamuuliza, “Jina lako ni nani?”
Akamjibu, “Jina langu ni Legionimaana yake Jeshi, kwa kuwa tuko wengi.” 10 Akamsihi Isa sana asiwapeleke nje ya nchi ile.
11 Palikuwa na kundi kubwa la nguruwe lililokuwa likilisha karibu kando ya kilima. 12 Wale pepo wachafu wakamsihi Isa wakisema, “Tuamuru twende kwenye wale nguruwe. Turuhusu tuwaingie.” 13 Basi Isa akawaruhusu, nao wale pepo wachafu wakatoka, wakawaingia hao nguruwe. Lile kundi lilikuwa na nguruwe wapatao elfu mbili, nao wote wakateremkia gengeni kwa kasi, nao wakatumbukia ziwani na kuzama.
14 Wale watu waliokuwa wakichunga hao nguruwe wakakimbilia mjini na vijijini kueleza yaliyotukia. Watu wakaenda kuona hayo yaliyokuwa yametukia. 15 Walipofika kwa Isa, wakamwona yule mtu aliyekuwa amepagawa na legioni ya pepo wachafu akiwa ameketi hapo, amevaa nguo na mwenye akili timamu. Wakaogopa. 16 Wale walioyaona mambo hayo wakawaeleza watu wengine yaliyomtokea yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo wachafu, na habari za lile kundi la nguruwe pia. 17 Basi watu wakaanza kumwomba Isa aondoke katika nchi yao.
18 Isa alipokuwa anaingia kwenye mashua, yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo wachafu akamsihi Isa waende pamoja. 19 Isa hakumruhusu, bali alimwambia, “Nenda nyumbani kwa jamaa yako ukawaeleze mambo makuu aliyokutendea Mwenyezi Mungu, na jinsi alivyokuhurumia.” 20 Yule mtu akaenda zake, akaanza kutangaza katika Dekapoli mambo makuu Isa aliyomtendea. Nao watu wote wakastaajabu.
Isa amponya mwanamke na kumfufua msichana
(Mathayo 9:18-26; Luka 8:40-56)
21 Isa alipokwisha kuvuka tena na kufika ng’ambo, umati mkubwa wa watu wakamzunguka hapo kando ya bahari. 22 Kisha mmoja wa viongozi wa sinagogiNyumba ya ibada na mafunzo. aliyeitwa Yairo akafika pale. Naye alipomwona Isa, akapiga magoti miguuni pake, 23 akamsihi akisema, “Binti yangu mdogo ni mgonjwa mahututi. Tafadhali nakusihi, njoo uweke mikono yako juu yake ili apate kupona, naye ataishi.” 24 Hivyo Isa akaenda pamoja naye.
Umati mkubwa wa watu wakamfuata, nao watu wakawa wanamsonga. 25 Hapo palikuwa na mwanamke aliyekuwa amesumbuliwa na tatizo la kutokwa damu kwa miaka kumi na mbili. 26 Mwanamke huyu alikuwa ameteseka sana kwa mikono ya matabibu wengi, na kutumia kila kitu alichokuwa nacho. Lakini badala ya kupona, hali yake ilizidi kuwa mbaya. 27 Alikuwa amesikia habari za Isa, naye akaja kwa nyuma yake kwenye umati wa watu, akaligusa vazi lake, 28 kwa maana alisema moyoni mwake, “Nikiligusa vazi lake tu, nitaponywa.” 29 Mara kutoka damu kwake kukakoma, naye akajisikia mwilini mwake amepona kabisa.
30 Ghafula Isa akatambua kuwa nguvu zimemtoka. Akageukia umati wa watu na kuuliza, “Ni nani aliyegusa mavazi yangu?”
31 Wanafunzi wake wakamjibu, “Unaona jinsi watu wanavyokusonga. Wawezaje kuuliza, ‘Ni nani aliyenigusa?’ ”
32 Lakini Isa akaangalia pande zote ili aone ni nani aliyemgusa. 33 Yule mwanamke, akijua kilichomtokea, akaja, akaanguka miguuni pake akitetemeka kwa hofu, akamweleza ukweli wote. 34 Isa akamwambia, “Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani, upone kabisa ugonjwa wako.”
35 Alipokuwa bado anaongea, watu wakafika kutoka nyumbani mwa Yairo. Wakamwambia, “Binti yako amekufa. Kwa nini kuendelea kumsumbua Mwalimu?”
36 Aliposikia hayo waliyosema, Isa akamwambia huyo kiongozi wa sinagogi, “Usiogope. Amini tu.”
37 Hakumruhusu mtu yeyote amfuate isipokuwa Petro, Yakobo na Yohana, nduguye Yakobo. 38 Walipofika nyumbani mwa yule kiongozi wa sinagogi, Isa akaona ghasia, watu wakilia na kuomboleza kwa sauti kubwa. 39 Alipokwisha kuingia ndani, akawaambia, “Kwa nini mnafanya ghasia na kulia? Mtoto hajafa, bali amelala tu.” 40 Wale watu wakamcheka.
Baada ya kuwafukuza wote nje, Isa akaenda na baba na mama wa yule mtoto, pamoja na wale wanafunzi aliokuwa nao, wakaingia ndani hadi pale alipokuwa mtoto yule. 41 Akamshika mtoto mkono, akamwambia, “Talitha koum!” (maana yake, “Msichana, nakuambia: amka!”) 42 Mara yule msichana akasimama, akaanza kutembea (alikuwa na umri wa miaka kumi na mbili). Walipoona haya, wakastaajabu sana. 43 Isa akawaagiza kwa ukali wasimweleze mtu yeyote jambo hilo, naye akawaambia wampe yule msichana chakula.

*5:7 Yaani Mwana wa asili moja na Mwenyezi Mungu (Yohana 1:1-2), wa kiroho, bali si wa kimwili.

5:9 maana yake Jeshi

5:22 Nyumba ya ibada na mafunzo.