6
Isa akataliwa Nasiri
(Mathayo 13:53-58; Luka 4:16-30)
1 Isa akaondoka huko na kwenda mji wa kwao, akiandamana na wanafunzi wake. 2 Ilipofika siku ya Sabato, akaanza kufundisha katika sinagogi, na wengi waliomsikia wakashangaa.
Nao wakauliza, “Mtu huyu ameyapata wapi mambo haya yote? Tazama ni hekima ya namna gani hii aliyopewa? Tazama matendo ya miujiza ayafanyayo kwa mikono yake! 3 Huyu si yule seremala, mwana wa Mariamu? Na ndugu zake si Yakobo, Yose*yaani Yusufu, Yuda na Simoni? Dada zake wote si tuko nao hapa kwetu?” Nao wakachukizwa sana kwa ajili yake, wakakataa kumwamini.
4 Isa akawaambia, “Nabii hakosi heshima isipokuwa katika mji wake mwenyewe, na miongoni mwa jamaa na ndugu zake, na nyumbani mwake.” 5 Hakufanya miujiza yoyote huko isipokuwa kuweka mikono yake juu ya wagonjwa wachache na kuwaponya. 6 Naye akashangazwa sana kwa kutoamini kwao.
Isa awatuma wale kumi na wawili
(Mathayo 10:5-15; Luka 9:1-6)
Kisha Isa akawa anaenda kutoka kijiji kimoja hadi kingine akifundisha. 7 Akawaita wale kumi na wawili, akawatuma wawili wawili, na kuwapa mamlaka kutoa pepo wachafu.
8 Akawaagiza akisema, “Msichukue chochote kwa ajili ya safari isipokuwa fimbo tu. Msichukue mkate, wala mkoba, wala fedha kwenye mikanda yenu. 9 Vaeni viatu, lakini msivae nguo ya ziada. 10 Mkiingia kwenye nyumba yoyote, kaeni humo hadi mtakapoondoka katika mji huo. 11 Kama mahali popote hawatawakaribisha wala kuwasikiliza, mtakapoondoka huko, kung’uteni mavumbi kutoka miguu yenu ili kuwe ushuhuda dhidi yao.”
12 Kwa hiyo wakaenenda na kuhubiri kwamba inawapasa watu kutubu na kuacha dhambi. 13 Wakatoa pepo wachafu wengi, wakawapaka wagonjwa wengi mafuta na kuwaponya.
Yahya akatwa kichwa
(Mathayo 14:1-12; Luka 9:7-9)
14 Mfalme Herode akasikia habari hizi, kwa maana jina la Isa lilikuwa limejulikana sana. Watu wengine walikuwa wakisema, “Yahya amefufuliwa kutoka kwa wafu, ndiyo sababu nguvu za kutenda miujiza zinafanya kazi ndani yake.”
15 Wengine wakasema, “Yeye ni Ilya.”
Nao wengine wakasema, “Yeye ni nabii, kama mmoja wa manabii wa zamani.”
16 Lakini Herode aliposikia habari hizi, akasema, “Huyo ni Yahya, niliyemkata kichwa, amefufuliwa kutoka kwa wafu!”
17 Herode mwenyewe alikuwa ameagiza kwamba Yahya akamatwe, afungwe na kutiwa gerezani. Alifanya hivi kwa sababu ya Herodia, mke wa Filipo, ndugu yake, ambaye Herode alikuwa amemwoa. 18 Yahya alikuwa amemwambia Herode, “Si halali kwako kuwa na mke wa ndugu yako.” 19 Kwa hiyo Herodia alikuwa amemwekea Yahya kinyongo, akataka kumuua. Lakini hakuweza, 20 kwa sababu Herode alimwogopa Yahya akijua kwamba ni mtu mwenye haki na mtakatifu, hivyo akamlinda. Herode alifadhaika sana alipomsikia Yohana, lakini bado alipenda kumsikiliza.
21 Hatimaye Herodia alipata wakati mwafaka aliokuwa akiutafuta. Mfalme Herode alifanya karamu kubwa wakati wa sikukuu ya kuzaliwa kwake. Akawaalika maafisa wake wakuu, majemadari wa jeshi na watu mashuhuri wa Galilaya. 22 Binti Herodia alipoingia na kucheza, akamfurahisha Herode pamoja na wageni wake walioalikwa chakulani.
Mfalme Herode akamwambia yule binti, “Niombe kitu chochote utakacho, nami nitakupa.” 23 Tena akamwahidi kwa kiapo, akamwambia, “Chochote utakachoomba nitakupa, hata kama ni nusu ya ufalme wangu.”
24 Yule binti akatoka nje, akaenda kumuuliza mama yake, “Niombe nini?”
Mama yake akamjibu, “Omba kichwa cha Yahya.”
25 Yule binti akarudi haraka kwa mfalme, akamwambia, “Nataka unipe sasa hivi kichwa cha Yahya kwenye sinia.”
26 Mfalme akasikitika sana, lakini kwa sababu alikuwa ameapa viapo mbele ya wageni wake, hakutaka kumkatalia. 27 Mara mfalme akatuma askari mmoja wa walinzi wake kukileta kichwa cha Yahya. Akaenda na kumkata Yahya kichwa humo gerezani, 28 akakileta kichwa chake kwenye sinia na kumpa yule msichana, naye yule msichana akampa mama yake. 29 Wanafunzi wa Yahya walipopata habari hizi, wakaja na kuuchukua mwili wake, wakauzika kaburini.
Isa alisha wanaume 5,000
(Mathayo 14:13-21; Luka 9:10-17; Yohana 6:1-14)
30 Wale mitume wakakusanyika kwa Isa na kumpa taarifa ya mambo yote waliyokuwa wamefanya na kufundisha. 31 Basi kwa kuwa watu wengi mno walikuwa wakija na kutoka, hata wakawa hawana nafasi ya kula, Isa akawaambia wanafunzi wake, “Twendeni peke yetu mahali pa faragha, mpate kupumzika.”
32 Hivyo wakaondoka kwa mashua peke yao, wakaenda mahali pasipo na watu. 33 Lakini watu wengi waliowaona wakiondoka, wakawatambua, nao wakaenda haraka kwa miguu kutoka miji yote, nao wakatangulia kufika. 34 Isa alipofika kando ya bahari, aliona kundi kubwa la watu, akawahurumia kwa maana walikuwa kama kondoo wasiokuwa na mchungaji. Kwa hiyo akaanza kuwafundisha mambo mengi.
35 Mchana ulipokuwa umeendelea sana, wanafunzi wake walienda kwake, wakamwambia, “Mahali hapa ni nyikani, nazo saa zimeenda sana. 36 Waage watu ili waende mashambani na vijijini jirani, wakajinunulie chakula.”
37 Lakini Isa akawajibu, “Ninyi wapeni chakula.”
Wakamwambia, “Je, twende tukanunue mikate ya dinari mia mbili†Dinari moja ilikuwa kama mshahara wa kibarua wa siku moja. ili tuwape watu hawa wale?”
38 Akawauliza, “Kuna mikate mingapi? Nendeni mkaangalie.”
Walipokwisha kujua, wakarudi, wakamwambia, “Kuna mikate mitano na samaki wawili.”
39 Kisha Isa akawaamuru wawaketishe watu makundi makundi kwenye majani, 40 nao wakaketi kwenye vikundi vya watu mia mia, na wengine hamsini hamsini. 41 Isa akaichukua ile mikate mitano na wale samaki wawili, akainua macho yake akatazama mbinguni, akavibariki na kuimega ile mikate. Kisha akawapa wanafunzi wake ili wawagawie wale watu wote. Pia akawagawia wote wale samaki wawili. 42 Watu wote wakala, wakashiba. 43 Nao wanafunzi wake wakakusanya vipande vilivyosalia vya mikate na samaki, wakajaza vikapu kumi na viwili. 44 Idadi ya wanaume waliokula walikuwa elfu tano.
Isa atembea juu ya maji
(Mathayo 14:22-33; Yohana 6:16-21)
45 Mara Isa akawaambia wanafunzi wake waingie kwenye mashua wamtangulie kwenda Bethsaida, wakati yeye alikuwa akiwaaga wale watu. 46 Baada ya kuwaaga, akaenda mlimani kuomba.
47 Ilipofika jioni, ile mashua ilikuwa imefika katikati ya bahari, na Isa alikuwa peke yake katika nchi kavu. 48 Akawaona wanafunzi wake wanahangaika na kupiga makasia kwa nguvu, kwa sababu upepo ulikuwa wa mbisho. Wakati wa zamu ya nne ya usiku, Isa akawaendea wanafunzi wake, akiwa anatembea juu ya maji. Alikuwa karibu kuwapita, 49 lakini walipomwona akitembea juu ya maji, wakadhani ni mzimu. Wakapiga yowe, 50 kwa sababu wote walipomwona waliogopa.
Mara Isa akasema nao, akawaambia, “Jipeni moyo! Ni mimi. Msiogope!” 51 Akapanda ndani ya mashua nao, na ule upepo ukakoma! Wakashangaa kabisa, 52 kwa kuwa walikuwa hawajaelewa kuhusu ile mikate. Mioyo yao ilikuwa migumu.
Isa awaponya wagonjwa Genesareti
(Mathayo 14:34-36)
53 Walipokwisha kuvuka, wakafika nchi ya Genesareti, wakatia nanga. 54 Mara waliposhuka kutoka mashua yao, watu wakamtambua Isa. 55 Wakaenda katika vijiji vyote upesi, wakawabeba wagonjwa kwenye mikeka ili kuwapeleka mahali popote waliposikia kuwa Isa yupo. 56 Kila mahali Isa alipoenda, iwe vijijini, mijini au mashambani, watu waliwaweka wagonjwa wao masokoni. Wakamwomba awaruhusu hao wagonjwa waguse japo upindo wa vazi lake. Nao wote waliomgusa waliponywa.