8
Isa alisha wanaume 4,000
(Mathayo 15:32-39)
Katika siku hizo, umati mkubwa wa watu walikusanyika tena. Kwa kuwa walikuwa hawana chakula, Isa akawaita wanafunzi wake akawaambia, “Ninahurumia umati huu wa watu, kwa sababu sasa wamekuwa nami kwa muda wa siku tatu na hawana chakula. Nikiwaaga waende nyumbani bila kula, watazimia njiani kwa sababu baadhi yao wametoka mbali.”
Wanafunzi wake wakamjibu, “Lakini hapa nyikani tutapata wapi mikate ya kutosha kuwalisha?”
Isa akawauliza, “Mna mikate mingapi?”
Wakajibu, “Tuna mikate saba.”
Akawaambia watu waketi chini. Akaichukua ile mikate saba na kushukuru, baadaye akaimega na kuwapa wanafunzi wake ili wawagawie watu. Wanafunzi wake wakafanya hivyo. Walikuwa pia na visamaki vichache, Isa akavibariki, akawaamuru wanafunzi wake wawagawie watu. Wale watu walikula na kutosheka. Baadaye wanafunzi wakakusanya vipande vilivyosalia, wakajaza vikapu saba. Watu waliokula walikuwa wapata elfu nne. Baada ya kuwaaga, 10 aliingia kwenye mashua pamoja na wanafunzi wake, akaenda sehemu za Dalmanutha.
Mafarisayo waomba ishara
(Mathayo 12:38-42)
11 Mafarisayo*Kundi la kidini la Wayahudi; walifuata Torati kwa dhati, hasa maagizo kuhusu utakaso. Pia waliamini katika malaika, ufufuo wa wafu, na kuja kwa Masihi ambaye atarejesha ufalme wa Daudi na ukuu wa taifa la Israeli. wakaja, wakaanza kumhoji Isa. Ili kumtega, wakamwomba awaoneshe ishara kutoka mbinguni. 12 Akahuzunika moyoni, akawaambia, “Kwa nini kizazi hiki kinataka ishara? Amin nawaambieni, hakitapewa ishara yoyote.” 13 Kisha akawaacha, akarudi kwenye mashua, akavuka hadi ng’ambo.
Chachu ya Mafarisayo na ya Herode
(Mathayo 16:5-12)
14 Wanafunzi walikuwa wamesahau kuchukua mikate ya kutosha. Walikuwa na mkate mmoja tu kwenye mashua. 15 Isa akawaonya: “Jihadharini na chachu ya Mafarisayo na ya Herode.”
16 Wakajadiliana wao kwa wao, na kusema, “Anasema hivi kwa sababu hatukuleta mikate.”
17 Isa, akifahamu majadiliano yao, akawauliza: “Mbona mnajadiliana kuhusu kutokuwa na mikate? Je, bado hamtambui wala hamwelewi? Je, mbona mioyo yenu ni migumu kiasi hicho? 18 Je, mna macho lakini mnashindwa kuona, na mna masikio lakini mnashindwa kusikia? Je, hamkumbuki? 19 Nilipoimega ile mikate mitano kwa watu elfu tano, mlikusanya vikapu vingapi vilivyojaa mabaki?”
Wakamjibu, “Kumi na viwili.”
20 “Je, nilipoimega ile mikate saba kwa watu elfu nne, mlikusanya vikapu vingapi vilivyojaa mabaki?”
Wakamjibu, “Saba.”
21 Ndipo akawauliza, “Je, bado hamwelewi?”
Isa amponya Kipofu huko Bethsaida
22 Wakafika Bethsaida na baadhi ya watu wakamleta mtu mmoja kipofu wakamsihi Isa amguse. 23 Isa akamshika mkono huyo kipofu akampeleka nje ya kijiji. Baada ya kuyatemea mate macho ya yule kipofu na kumwekea mikono, Isa akamuuliza, “Unaona chochote?”
24 Yule kipofu akaangalia, akasema, “Ninaona watu, wanaonekana kama miti inayotembea.”
25 Isa akamwekea tena mikono machoni. Kisha macho yake yakafunguka, kuona kwake kukarejea naye akaona kila kitu dhahiri. 26 Isa akamtuma nyumbani mwake, akamwambia, “Hata kijijini usiingie.”
Petro amkiri Isa kuwa Al-Masihi
(Mathayo 16:13-20; Luka 9:18-21)
27 Isa na wanafunzi wake wakaelekea vijiji vya Kaisaria-Filipi. Walipokuwa njiani, Isa akawauliza, “Watu husema mimi ni nani?”
28 Wakamjibu, “Baadhi husema wewe ni Yahya, wengine husema ni Ilya, na bado wengine husema wewe ni mmoja wa manabii.”
29 Akawauliza, “Je, ninyi mnasema mimi ni nani?”
Petro akajibu, “Wewe ndiwe Al-MasihiAl-Masihi maana yake Aliyetiwa mafuta..”
30 Isa akawaonya wasimwambie mtu yeyote habari zake.
Isa atabiri kifo chake
(Mathayo 16:21-28; Luka 9:22-27)
31 Ndipo akaanza kuwafundisha wanafunzi wake kuwa Mwana wa Adamu lazima atapata mateso mengi na kukataliwa na wazee, viongozi wa makuhani, na walimu wa Torati, na kwamba itampasa auawe lakini baada ya siku tatu afufuliwe. 32 Aliyasema haya waziwazi. Ndipo Petro akamchukua kando na akaanza kumkemea.
33 Lakini Isa akageuka na kuwaangalia wanafunzi wake, na akamkemea Petro. Akasema, “Rudi nyuma yangu, Shetani! Moyo wako hauwazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.”
34 Ndipo akawaita umati ule wa watu pamoja na wanafunzi wake, akasema, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, ni lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake, anifuate. 35 Kwa maana yeyote anayetaka kuyaokoa maisha yake atayapoteza, lakini yeyote atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili atayaokoa. 36 Je, itamfaidi nini mtu kuupata ulimwengu wote, lakini akayapoteza maisha yake? 37 Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake? 38 Mtu yeyote akinionea aibu mimi na maneno yangu katika kizazi hiki cha uzinzi na dhambi, Mwana wa AdamuMwana wa Adamu ni jina la Isa Al-Masihi kujishirikisha na udhaifu wa mwanadamu. naye atamwonea aibu wakati atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu.”

*8:11 Kundi la kidini la Wayahudi; walifuata Torati kwa dhati, hasa maagizo kuhusu utakaso. Pia waliamini katika malaika, ufufuo wa wafu, na kuja kwa Masihi ambaye atarejesha ufalme wa Daudi na ukuu wa taifa la Israeli.

8:29 Al-Masihi maana yake Aliyetiwa mafuta.

8:38 Mwana wa Adamu ni jina la Isa Al-Masihi kujishirikisha na udhaifu wa mwanadamu.