9
Isa akaendelea kuwaambia, “Amin, nawaambia, kuna watu waliosimama hapa ambao hawataonja mauti kabla ya kuuona ufalme wa Mungu ukija kwa nguvu.”
Isa abadilika sura
(Mathayo 17:1-13; Luka 9:28-36)
Baada ya siku sita, Isa akawachukua Petro, Yakobo na Yohana, akawapeleka juu ya mlima mrefu, mahali walipokuwa faraghani. Huko, Isa akageuka sura mbele yao. Mavazi yake yakawa na weupe wa kuzima macho, meupe kuliko vile mtu yeyote duniani angeweza kuyang’arisha. Musa na Ilya wakawatokea, wakawa wanazungumza na Isa.
Petro akamwambia Isa, “Mwalimu, ni vyema sisi tukae hapa. Turuhusu tujenge vibanda vitatu: kimoja chako, kingine cha Musa na kingine cha Ilya.” Petro hakujua aseme nini kwa maana yeye na wenzake walikuwa wameogopa sana.
Ndipo pakatokea wingu, likawafunika, nayo sauti kutoka lile wingu ikasema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa. Msikieni yeye.”
Mara walipotazama huku na huku, hawakuona tena mtu mwingine yeyote pamoja nao isipokuwa Isa.
Walipokuwa wakishuka kutoka mlimani, Isa akawakataza wasimwambie mtu yeyote mambo waliyoyaona, hadi Mwana wa Adamu atakapokuwa amefufuka kutoka kwa wafu. 10 Wakalihifadhi jambo hilo wao wenyewe, lakini wakawa wanajiuliza, “Huku kufufuka kwa wafu maana yake nini?”
11 Wakamuuliza, “Kwa nini walimu wa Torati husema kwamba ni lazima Ilya aje kwanza?”
12 Isa akawajibu, “Ni kweli, Ilya yuaja kwanza ili kutengeneza mambo yote. Mbona basi imeandikwa kwamba Mwana wa Adamu ni lazima ateseke sana na kudharauliwa? 13 Lakini nawaambia, Ilya amekwisha kuja, nao wakamtendea walivyopenda, kama ilivyoandikwa kumhusu.”
Isa amponya kijana mwenye pepo mchafu
(Mathayo 17:14-21; Luka 9:37-45)
14 Walipowafikia wale wanafunzi wengine, wakawakuta wamezungukwa na umati mkubwa wa watu na baadhi ya walimu wa Torati wakibishana nao. 15 Mara wale watu walipomwona Isa, wakastaajabu sana, wakamkimbilia ili kumsalimu.
16 Akawauliza wanafunzi wake, “Mnabishana nao kuhusu nini?”
17 Mtu mmoja miongoni mwa umati ule wa watu akajibu, “Mwalimu, nilimleta kwako mwanangu ambaye ana pepo mchafu anayemfanya asiweze kuongea. 18 Kila mara huyo pepo mchafu ampagaapo mwanangu, humwangusha chini na kumfanya atokwe povu mdomoni na kusaga meno, kisha mwili wake hukauka. Niliwaomba wanafunzi wako wamtoe huyo pepo mchafu, lakini hawakuweza.”
19 Isa akawaambia, “Enyi kizazi kisichoamini! Nitakuwa pamoja nanyi hadi lini? Nitawavumilia hadi lini? Mleteni mvulana kwangu.”
20 Nao wakamleta yule mvulana. Yule pepo mchafu alipomwona Isa, mara akamtia yule mvulana kifafa, akaanguka, akagaagaa chini huku akitokwa na povu kinywani.
21 Isa akamuuliza baba yake, “Mwanao amekuwa katika hali hii tangu lini?”
Akamjibu, “Tangu utoto wake. 22 Mara kwa mara huyo pepo mchafu amekuwa akimwangusha kwenye moto au kwenye maji ili kumwangamiza. Lakini kama unaweza kufanya jambo lolote, tafadhali tuhurumie utusaidie.”
23 Isa akamwambia, “Ati, ‘Kama unaweza kufanya jambo lolote’? Yote yawezekana kwake yeye aaminiye.”
24 Mara baba yake yule mvulana akapaza sauti akisema, “Ninaamini. Nisaidie kutokuamini kwangu!”
25 Isa alipoona kwamba umati wa watu wanakusanyika pamoja mbio, akamkemea yule pepo mchafu, akimwambia, “Wewe pepo bubu na kiziwi, nakuamuru umtoke, wala usimwingie tena!”
26 Baada ya yule pepo mchafu kupiga kelele, akamtia kifafa kwa nguvu, akamtoka. Yule mvulana alikuwa kama maiti, hivyo watu wengi wakasema, “Amekufa.” 27 Lakini Isa akamshika mkono, akamwinua, naye akasimama.
28 Baada ya Isa kuingia ndani ya nyumba, wanafunzi wake wakamuuliza wakiwa peke yao, “Mbona sisi hatukuweza kumtoa huyo pepo mchafu?”
29 Isa akawajibu, “Pepo aina hii haiwezi kutoka isipokuwa kwa kuomba [na kufunga]*Maandiko mengine ya kale hayana maneno haya..”
Isa atabiri tena kifo chake na ufufuo
(Mathayo 17:22-23; Luka 9:43-45)
30 Wakaondoka huko, wakapitia Galilaya. Isa hakutaka mtu yeyote afahamu mahali walipo, 31 kwa maana alikuwa anawafundisha wanafunzi wake. Akawaambia, “Mwana wa Adamu atasalitiwa na kutiwa mikononi mwa watu. Nao watamuua, lakini siku tatu baada ya kuuawa atafufuka.” 32 Lakini wao hawakuelewa kile alimaanisha, nao waliogopa kumuuliza maana yake.
Aliye mkuu katika Ufalme wa mbinguni
(Mathayo 18:1-5; Luka 9:46-48; 22:24-30)
33 Basi wakafika Kapernaumu na baada ya kuingia nyumbani akawauliza, “Mlikuwa mnabishana nini kule njiani?” 34 Lakini hawakumjibu, kwa sababu njiani walikuwa wakibishana kuhusu nani miongoni mwao alikuwa mkuu zaidi ya wote.
35 Akaketi chini, akawaita wote kumi na wawili, akawaambia: “Kama mtu yeyote akitaka kuwa wa kwanza, hana budi kuwa wa mwisho na mtumishi wa wote.”
36 Kisha akamchukua mtoto mdogo, akamsimamisha katikati yao. Akamkumbatia, akawaambia, 37 “Mtu yeyote amkaribishaye mmoja wa hawa watoto wadogo kwa Jina langu, anikaribisha mimi. Naye anikaribishaye mimi, amkaribisha BabaJina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. yangu aliyenituma.”
Yeyote asiye kinyume nasi yuko upande wetu
(Luka 9:49-50)
38 Yohana akamwambia, “Mwalimu, tumemwona mtu akitoa pepo wachafu kwa jina lako, nasi tukamkataza, kwa sababu yeye si mmoja wetu.”
39 Isa akasema, “Msimkataze, kwa kuwa hakuna yeyote atendaye miujiza kwa Jina langu ambaye baada ya kitambo kidogo aweza kunena lolote baya dhidi yangu. 40 Kwa maana yeyote asiye kinyume chetu, yuko upande wetu. 41 Amin, nawaambia, yeyote awapaye ninyi kikombe cha maji kwa Jina langu kwa sababu ninyi ni mali ya Al-Masihi, hakika hataikosa thawabu yake.
Kujaribiwa ili kutenda dhambi
(Mathayo 18:6-9; Luka 17:1-2)
42 “Mtu yeyote akimsababisha mmoja wa hawa wadogo wanaoniamini kutenda dhambi, ingekuwa bora kwake afungiwe jiwe kubwa la kusagia shingoni mwake, na kutoswa baharini. 43 Mkono wako ukikusababisha kutenda dhambi, ukate. Ni afadhali kwako kuingia katika uzima ukiwa na mkono mmoja, kuliko kuwa na mikono miwili lakini ukaingia Jehanamu, mahali ambako moto hauzimiki. [ 44 Ni mahali ambako funza wao hawafi wala moto wao hauzimiki.]Maandiko mengine ya kale hayana maneno haya. 45 Mguu wako ukikusababisha kutenda dhambi, ukate. Ni afadhali kwako kuingia katika uzima ukiwa kiwete, kuliko kuwa na miguu miwili lakini ukaingia Jehanamu. [ 46 Ni mahali ambako funza wao hawafi wala moto wao hauzimiki.]§Maandiko mengine ya kale hayana maneno haya. 47 Nalo jicho lako likikusababisha kutenda dhambi, ling’oe. Ni afadhali kwako kuingia katika ufalme wa Mungu ukiwa na jicho moja, kuliko kuwa na macho mawili lakini ukatupwa Jehanamu. 48 Ni mahali ambako funza wao hawafi, wala moto wao hauzimiki.
49 Kila mmoja atatiwa chumvi kwa moto.
50 “Chumvi ni nzuri, lakini ikipoteza ladha yake utaifanyaje ili iweze kukolea tena? Mwe na chumvi ndani yenu, mkaishi kwa amani, kila mmoja na mwenzake.”

*9:29 Maandiko mengine ya kale hayana maneno haya.

9:37 Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu.

9:44 Maandiko mengine ya kale hayana maneno haya.

§9:46 Maandiko mengine ya kale hayana maneno haya.