2
Mpangilio wa kambi za makabila
1 Mwenyezi Mungu aliwaambia Musa na Haruni: 2 “Waisraeli watapiga kambi zao kuzunguka Hema la Kukutania kwa umbali kiasi, kila mwanaume akiwa chini ya beramu yake, pamoja na bendera ya jamaa yake.”
3 Kwa upande wa mashariki kuelekea mawio ya jua,
kambi ya makundi ya Yuda watapiga kambi chini ya beramu yao. Kiongozi wa watu wa Yuda ni Nashoni mwana wa Aminadabu. 4 Kundi lake lina watu elfu sabini na nne na mia sita.
5 Kabila la Isakari watapiga kambi karibu na Yuda. Kiongozi wa watu wa Isakari ni Nethaneli mwana wa Suari. 6 Kundi lake lina watu elfu hamsini na nne na mia nne.
7 Kabila la Zabuloni litafuata. Kiongozi wa watu wa Zabuloni ni Eliabu mwana wa Heloni. 8 Kundi lake lina watu elfu hamsini na saba na mia nne.
9 Wanaume wote walio katika kambi ya Yuda, kufuatana na makundi yao, ni elfu mia moja themanini na sita na mia nne. Wao watatangulia kuondoka.
10 Kwa upande wa kusini kutakuwa na
kambi ya makundi ya Reubeni chini ya beramu yao. Kiongozi wa watu wa Reubeni ni Elisuri mwana wa Shedeuri. 11 Kundi lake lina watu elfu arobaini na sita na mia tano.
12 Kabila la Simeoni watapiga kambi karibu na Reubeni. Kiongozi wa watu wa Simeoni ni Shelumieli mwana wa Surishadai. 13 Kundi lake lina watu elfu hamsini na tisa na mia tatu.
14 Kabila la Gadi litafuata. Kiongozi wa watu wa Gadi ni Eliasafu mwana wa Deueli. 15 Kundi lake lina watu elfu arobaini na tano mia sita na hamsini.
16 Wanaume wote walio katika kambi ya Reubeni, kufuatana na makundi yao, ni elfu mia moja hamsini na moja na mia nne na hamsini (151,450). Nao watakuwa nafasi ya pili kuondoka.
17 Kisha Hema la Kukutania na kambi ya Walawi vitakuwa katikati ya kambi zote. Wao watasafiri kwa utaratibu ule ule kama walivyopiga kambi, kila mmoja mahali pake mwenyewe chini ya beramu yake.
18 Upande wa magharibi kutakuwa na
kambi ya makundi ya Efraimu chini ya beramu yao. Kiongozi wa watu wa Efraimu ni Elishama mwana wa Amihudi. 19 Kundi lake lina watu elfu arobaini na mia tano.
20 Kabila la Manase litafuata baada ya Efraimu. Kiongozi wa watu wa Manase ni Gamalieli mwana wa Pedasuri. 21 Kundi lake lina watu elfu thelathini na mbili na mia mbili.
22 Kabila la Benyamini litafuata baada ya Manase. Kiongozi wa watu wa Benyamini ni Abidani mwana wa Gideoni. 23 Kundi lake lina watu elfu thelathini na tano na mia nne.
24 Wanaume wote walio katika kambi ya Efraimu kufuatana na makundi yao ni elfu mia moja na nane na mia moja. Nao watakuwa nafasi ya tatu kuondoka.
25 Upande wa kaskazini kutakuwa na
makundi ya kambi ya Dani, chini ya beramu yao. Kiongozi wa watu wa Dani ni Ahiezeri mwana wa Amishadai. 26 Kundi lake lina watu elfu sitini na mbili na mia saba.
27 Kabila la Asheri watapiga kambi karibu na Dani. Kiongozi wa watu wa Asheri ni Pagieli mwana wa Okrani. 28 Kundi lake lina watu elfu arobaini na moja na mia tano.
29 Kabila la Naftali litafuata. Kiongozi wa watu wa Naftali ni Ahira mwana wa Enani. 30 Kundi lake lina watu elfu hamsini na tatu na mia nne.
31 Wanaume wote walio katika kambi ya Dani ni elfu mia moja hamsini na saba na mia sita. Wao watakuwa wa mwisho kuondoka chini ya beramu yao.
32 Hawa ndio Waisraeli, wakiwa wamehesabiwa kufuatana na jamaa zao. Wote walio kambini kwa makundi yao ni watu elfu mia sita na tatu mia tano na hamsini (603,550). 33 Hata hivyo, Walawi hawakuhesabiwa pamoja na Waisraeli wengine, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa.
34 Kwa hiyo Waisraeli wakafanya kila kitu Mwenyezi Mungu alichomwamuru Musa. Hivyo ndivyo walivyopiga kambi chini ya beramu zao. Pia hivyo ndivyo walivyoondoka, kila mmoja akiwa na ukoo wake na jamaa yake.