3
Walawi
1 Hivi ndivyo vizazi vya Haruni na Musa kwa wakati ambao Mwenyezi Mungu alizungumza na Musa katika Mlima Sinai.
2 Majina ya wana wa Haruni yalikuwa: Nadabu mzaliwa wa kwanza na Abihu, Eleazari na Ithamari. 3 Hayo yalikuwa majina ya wana wa Haruni, makuhani wapakwa mafuta, waliokuwa wamesimikwa kuhudumu kama makuhani. 4 Hata hivyo Nadabu na Abihu walikufa mbele za Mwenyezi Mungu walipotoa sadaka kwa moto usioruhusiwa mbele zake katika Jangwa la Sinai. Hawakuwa na wana; kwa hiyo Eleazari na Ithamari walihudumu peke yao kama makuhani wakati wote wa maisha ya Haruni baba yao.
5 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, 6 “Walete kabila la Lawi mbele ya Haruni kuhani ili wamsaidie. 7 Watafanya huduma kwa ajili yake na kwa jumuiya yote katika Hema la Kukutania kwa kufanya kazi za Maskani. 8 Watatunza samani zote za Hema la Kukutania, wakitimiza wajibu wa kuhudumia Waisraeli kwa kufanya kazi ya Maskani. 9 Wakabidhi Walawi kwa Haruni na wanawe; hao ndio Waisraeli ambao wanakabidhiwa kwake kabisa. 10 Waweke Haruni na wanawe kuhudumu kama makuhani; mtu mwingine yeyote atakayesogea mahali patakatifu atauawa.”
11 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, 12 “Nimewatwaa Walawi kutoka miongoni mwa Waisraeli badala ya mzaliwa wa kwanza wa kiume wa kila mwanamke wa Mwisraeli. Walawi ni wangu, 13 kwa kuwa wazaliwa wote wa kwanza ni wangu. Nilipowaua wazaliwa wa kwanza huko Misri, nilimtenga kila mzaliwa wa kwanza katika Israeli awe wangu, akiwa mwanadamu au mnyama. Watakuwa wangu. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.”
14 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa katika Jangwa la Sinai, 15 “Wahesabu Walawi kwa jamaa zao na koo zao. Mhesabu kila mwanaume mwenye umri wa mwezi mmoja au zaidi.” 16 Kwa hiyo Musa akawahesabu, kama alivyoamriwa na neno la Mwenyezi Mungu.
17 Haya yalikuwa majina ya wana wa Lawi:
Gershoni, Kohathi na Merari.
18 Haya ndio yaliyokuwa majina ya koo za Wagershoni:
Libni na Shimei.
19 Koo za Wakohathi zilikuwa ni:
Amramu, Ishari, Hebroni na Uzieli.
20 Koo za Wamerari zilikuwa ni:
Mahli na Mushi.
Hizo zilikuwa koo za Walawi, kufuatana na jamaa zao.
21 Kulikuwa na koo za Walibni na Washimei kwa Gershoni; hizo zilikuwa koo za Wagershoni.
22 Idadi ya wanaume wote wa umri wa mwezi mmoja au zaidi waliohesabiwa walikuwa elfu saba na mia tano.
23 Ukoo wa Wagershoni walitakiwa kuweka kambi zao upande wa magharibi, nyuma ya Maskani.
24 Kiongozi wa jamaa za Wagershoni alikuwa Eliasafu mwana wa Laeli.
25 Katika Hema la Kukutania, Wagershoni walikuwa na wajibu wa kutunza Maskani na hema, vifuniko vyake, pazia katika mlango wa kuingilia ndani ya Hema la Kukutania, 26 mapazia ya ua, pazia katika ingilio la ua unaozunguka Maskani na madhabahu, pamoja na kamba, na kila kinachohusika kwa matumizi yake.
27 Kwa Kohathi kulikuwa koo za Waamrami, Waishari, Wahebroni na Wauzieli; hizo zilikuwa koo za Wakohathi.
28 Hesabu ya wanaume wote wenye umri wa mwezi mmoja au zaidi, walikuwa elfu nane na mia sita.
Wakohathi waliwajibika kutunza mahali patakatifu.
29 Koo za Wakohathi zilitakiwa kuweka kambi zao upande wa kusini wa Maskani.
30 Kiongozi wa jamaa za koo za Wakohathi alikuwa Elisafani mwana wa Uzieli.
31 Waliwajibika kutunza Sanduku la Agano, meza, kinara cha taa, madhabahu, na vile vyombo vya mahali patakatifu vinavyotumika kuhudumu, pazia, na kila kitu kinachohusika na matumizi yake.
32 Kiongozi mkuu wa Walawi alikuwa Eleazari mwana wa kuhani, Haruni. Aliwekwa juu ya wale waliowajibika kutunza mahali patakatifu.
33 Kwa Merari kulikuwa na koo za Wamahli na Wamushi; hizi zilikuwa koo za Merari.
34 Hesabu ya wanaume wote wenye umri wa mwaka mmoja au zaidi waliohesabiwa, walikuwa elfu sita na mia mbili.
35 Kiongozi wa jamaa za koo za Wamerari alikuwa Surieli mwana wa Abihaili.
Hawa walitakiwa kuweka kambi zao upande wa kaskazini mwa Maskani.
36 Wamerari waliwekwa kutunza miimo ya Maskani, mataruma yake, nguzo, vitako na vifaa vyake vyote na kila kitu kilichohusika na matumizi yake, 37 na pia nguzo za ua unaozunguka pamoja na vitako vyake, vigingi vya hema na kamba zake.
38 Musa, na Haruni na wanawe walitakiwa kuweka kambi zao mashariki mwa Maskani, kuelekea mawio ya jua, mbele ya Hema la Kukutania.
Wao walihusika na utunzaji wa mahali patakatifu kwa niaba ya Waisraeli.
Mtu mwingine yeyote aliyepasogelea mahali patakatifu angeuawa.
39 Jumla ya hesabu ya Walawi waliohesabiwa na Musa na Haruni kwa amri ya Mwenyezi Mungu, kufuatana na koo zao, pamoja na kila mwanaume mwenye umri wa mwezi mmoja au zaidi, walikuwa elfu ishirini na mbili.
40 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Wahesabu wazaliwa wa kwanza wa kiume wote wa Waisraeli wenye umri wa mwezi mmoja au zaidi na uorodheshe majina yao. 41 Nitwalie Walawi badala ya wazaliwa wa kwanza wa Waisraeli, nayo mifugo ya Walawi badala ya wazaliwa wa mifugo ya Waisraeli. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.”
42 Hivyo Musa akawahesabu wazaliwa wa kwanza wote wa Waisraeli, kama Mwenyezi Mungu alivyomwamuru. 43 Jumla ya hesabu ya wazaliwa wa kwanza wanaume wenye umri wa mwezi mmoja au zaidi, walioorodheshwa kwa majina, walikuwa elfu ishirini na mbili na mia mbili na sabini na watatu (22,273).
44 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, 45 “Watwae Walawi badala ya wazaliwa wa kwanza wote wa Israeli, nayo mifugo ya Walawi badala ya mifugo yao. Walawi watakuwa wangu. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu. 46 Ili kukomboa wazaliwa wa kwanza mia mbili na sabini na watatu (273) wa Waisraeli ambao wamezidi hesabu ya Walawi, 47 kusanya shekeli tano*Shekeli tano ni sawa na gramu 55. kwa kila mmoja, kufuatana na shekeli ya mahali patakatifu, ambayo ina uzito wa gera ishirini†Gera 20 ni sawa na gramu 11.. 48 Mpe Haruni na wanawe hizo fedha kwa ajili ya ukombozi wa idadi ya Waisraeli waliozidi.”
49 Kwa hiyo Musa akakusanya fedha za ukombozi kutoka kwa wale ambao hesabu yao ilizidi wale waliokombolewa na Walawi. 50 Kutokana na wazaliwa wa kwanza wa Waisraeli alikusanya fedha yenye uzito wa shekeli elfu moja na mia tatu sitini na tano (1,365)‡Shekeli 1,365 ni sawa na kilo 15.5. kufuatana na shekeli ya mahali patakatifu. 51 Musa akampa Haruni na wanawe ile fedha ya ukombozi, kama alivyoamriwa na neno la Mwenyezi Mungu.