8
Kuwekwa kwa taa
Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Sema na Haruni umwambie, ‘Utakapoziweka zile taa saba, zinatakiwa kuangaza eneo lililo mbele ya kinara cha taa.’ ”
Haruni akafanya hivyo; akaziweka zile taa ili zielekee mbele kwenye kinara cha taa, kama vile Mwenyezi Mungu alivyomwamuru Musa. Hivi ndivyo kinara cha taa kilivyotengenezwa: Kilitengenezwa kwa dhahabu iliyofuliwa, kuanzia kwenye kitako chake hadi kwenye maua yake. Kinara cha taa kilitengenezwa sawasawa kabisa na kielelezo ambacho Mwenyezi Mungu alikuwa amemwonesha Musa.
Kutengwa kwa Walawi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu
Mwenyezi Mungu akamwambia Musa: “Watwae Walawi kutoka miongoni mwa Waisraeli wengine na uwatakase. Ili kuwatakasa, fanya hivi: Nyunyizia maji ya utakaso juu yao; kisha uwaambie wanyoe nywele kwenye mwili mzima, wafue nguo zao na hivyo wajitakase wenyewe. Waambie wamchukue fahali mchanga pamoja na sadaka yake ya nafaka ya unga laini uliochanganywa na mafuta; kisha utamchukua fahali mchanga wa pili kwa ajili ya sadaka ya dhambi. Walete Walawi mbele ya Hema la Kukutania na ukusanye jumuiya yote ya Waisraeli. 10 Utawaleta Walawi mbele za Mwenyezi Mungu, na Waisraeli wataweka mikono yao juu ya Walawi. 11 Haruni atawaweka Walawi mbele za Mwenyezi Mungu wawe sadaka ya kuinuliwa kutoka kwa Waisraeli, ili wawe tayari kuifanya kazi ya Mwenyezi Mungu.
12 “Baada ya Walawi kuweka mikono yao juu ya vichwa vya hao mafahali wawili, tumia mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi kwa Mwenyezi Mungu, na mwingine kuwa sadaka ya kuteketezwa, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya Walawi. 13 Waambie hao Walawi wasimame mbele ya Haruni na wanawe, kisha wawatoe wawe sadaka ya kuinuliwa kwa Mwenyezi Mungu. 14 Kwa njia hii utakuwa umewatenga Walawi kutoka kwa Waisraeli wengine, nao Walawi watakuwa wangu.
15 “Utakapokuwa umekwisha kuwatakasa Walawi na kuwatoa wawe sadaka ya kuinuliwa, watakuja kufanya kazi yao katika Hema la Kukutania. 16 Wao ndio Waisraeli ambao watatolewa kabisa kwangu. Nimewatwaa kama mali yangu mwenyewe badala ya mzaliwa wa kwanza, mzaliwa wa kwanza wa kiume kutoka kwa kila mwanamke Mwisraeli. 17 Kila mzaliwa wa kwanza wa kiume katika Israeli, awe wa mwanadamu au mnyama, ni wangu. Nilipowaua wazaliwa wote wa kwanza huko Misri, niliwatenga kwa ajili yangu mwenyewe. 18 Nami nimewatwaa Walawi badala ya wazaliwa wote wa kwanza wa kiume katika Israeli. 19 Kati ya Waisraeli wote, nimempa Haruni na wanawe Walawi kama zawadi ili wafanye kazi katika Hema la Kukutania kwa niaba ya Waisraeli, na kufanya upatanisho kwa ajili yao ili pasiwepo na pigo lolote litakalowapata Waisraeli wakati watakapokaribia mahali patakatifu.”
20 Musa, Haruni na jumuiya yote ya Waisraeli wakawafanyia Walawi kama Mwenyezi Mungu alivyomwamuru Musa. 21 Walawi wakajitakasa wenyewe na wakafua nguo zao. Kisha Haruni akawasogeza mbele za Mwenyezi Mungu kuwa sadaka ya kuinuliwa, na kufanya upatanisho kwa ajili yao ili kuwatakasa. 22 Baada ya hayo, Walawi walikuja kufanya kazi yao katika Hema la Kukutania chini ya usimamizi wa Haruni na wanawe. Waliwafanyia Walawi kama vile Mwenyezi Mungu alivyomwamuru Musa.
23 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, 24 “Hili linawahusu Walawi: Wanaume wenye umri wa miaka ishirini na tano au zaidi watakuja kushiriki katika kazi kwenye Hema la Kukutania, 25 lakini watakapofika umri wa miaka hamsini, ni lazima waache kazi zao za kawaida wala wasiendelee. 26 Wanaweza kuwasaidia ndugu zao kufanya wajibu wao katika Hema la Kukutania, lakini wao wenyewe kamwe hawatafanya hiyo kazi. Basi, hivi ndivyo utakavyogawa wajibu kwa Walawi.”