20
Maji kutoka mwamba
(Kutoka 17:1-7)
1 Katika mwezi wa kwanza, jumuiya yote ya Waisraeli walifika kwenye Jangwa la Sini, nao wakakaa Kadeshi. Miriamu akafa huko na kuzikwa.
2 Mahali hapo hapakuwa na maji kwa ajili ya jumuiya hiyo, nao wakakusanyika ili kumpinga Musa na Haruni. 3 Watu wakagombana na Musa, na kusema, “Laiti tungekufa ndugu zetu walipokufa mbele za Mwenyezi Mungu! 4 Kwa nini mmewaleta jumuiya ya Mwenyezi Mungu kwenye jangwa hili, ili tufe humu, sisi na mifugo yetu? 5 Kwa nini mmetupandisha kutoka Misri hadi mahali hapa pa kutisha? Hapa hakuna nafaka wala tini, zabibu au makomamanga. Wala hapa hakuna maji ya kunywa!”
6 Musa na Haruni wakaondoka pale kwenye kusanyiko hadi kwenye mlango wa Hema la Kukutania na kuanguka kifudifudi, nao utukufu wa Mwenyezi Mungu ukawatokea. 7 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, 8 “Chukua ile fimbo, na wewe na ndugu yako Haruni mkawakusanye watu wote. Nena na ule mwamba mbele ya macho yao, nao utatoa maji yake. Utatoa maji kutoka huo mwamba kwa ajili ya jumuiya ili wao na mifugo yao waweze kunywa.”
9 Kwa hiyo Musa akaichukua hiyo fimbo kutoka pale ilipokuwa mbele za Mwenyezi Mungu kama alivyomwagiza. 10 Musa na Haruni wakakusanya kusanyiko pamoja mbele ya huo mwamba, naye Musa akawaambia, “Sikilizeni, enyi waasi. Je, ni lazima tuwatoleeni maji kutoka mwamba huu?” 11 Ndipo Musa akainua mkono wake na kuupiga mwamba mara mbili kwa fimbo yake. Maji yakabubujika, nayo jumuiya na mifugo yao wakanywa.
12 Lakini Mwenyezi Mungu akamwambia Musa na Haruni, “Kwa sababu hamkuniamini mimi kiasi cha kuniheshimu kama mtakatifu machoni pa Waisraeli, hamtaiingiza jumuiya hii katika nchi ninayowapa.”
13 Haya yalikuwa maji ya Meriba*maana yake Kugombana, ambapo Waisraeli waligombana na Mwenyezi Mungu, naye akajionesha kuwa mtakatifu kati yao.
Edomu wakatalia Israeli kupita
14 Musa akawatuma wajumbe kutoka Kadeshi kwenda kwa mfalme wa Edomu, akisema:
“Hili ndilo ndugu yako Israeli asemalo: Wewe unafahamu juu ya taabu zote ambazo zimetupata. 15 Baba zetu walishuka Misri, nasi tumeishi huko miaka mingi. Wamisri walitutesa sisi na baba zetu, 16 lakini tulipomlilia Mwenyezi Mungu, alisikia kilio chetu na akamtuma malaika akatutoa Misri.
“Sasa tupo hapa Kadeshi, mji ulio mpakani mwa nchi yako. 17 Tafadhali turuhusu tupite katika nchi yako. Hatutapita katika shamba lolote, wala shamba la mizabibu, au kunywa maji kwenye kisima chochote. Tutasafiri kufuata njia kuu ya mfalme, na hatutageuka kulia wala kushoto hadi tuwe tumeshapita nchi yako.”
18 Lakini mfalme wa Edomu akajibu:
“Hamtapita hapa. Mkijaribu kupita, tutatoka na kuwashambulia kwa upanga.”
19 Waisraeli wakajibu:
“Sisi tutafuata njia kuu; tena ikiwa sisi au mifugo yetu tutakunywa tone la maji yenu, tutalilipia. Sisi tunataka tu kupita kwa miguu, wala si kitu kingine chochote.”
20 Watu wa Edomu wakajibu tena:
“Hamwezi kupita hapa.”
Ndipo watu wa Edomu wakatoka dhidi ya Waisraeli, jeshi kubwa lenye nguvu. 21 Kwa kuwa Waedomu waliwakatalia Waisraeli kupita katika nchi yao, Israeli wakageuka, wakawaacha.
Kifo cha Haruni
22 Jumuiya yote ya Waisraeli wakaondoka Kadeshi, wakafika kwenye Mlima Hori. 23 Kwenye Mlima Hori, karibu na mpaka wa Edomu, Mwenyezi Mungu akamwambia Musa na Haruni, 24 “Haruni atakusanywa pamoja na watu wake. Hataingia katika nchi ninayowapa Waisraeli, kwa sababu ninyi wawili mliasi dhidi ya agizo langu kwenye maji ya Meriba. 25 Watwae Haruni na Eleazari mwanawe, na uwapandishe juu katika Mlima Hori. 26 Mvue Haruni mavazi yake, na umvike Eleazari mwanawe, kwa maana Haruni atakusanywa pamoja na watu wake; atakufa huko.”
27 Musa akafanya kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza: Wakapanda Mlima Hori mbele ya macho ya jumuiya yote ya Waisraeli. 28 Musa akamvua Haruni mavazi yake na kumvika mwanawe Eleazari mavazi hayo. Naye Haruni akafia pale juu ya mlima. Kisha Musa na Eleazari wakateremka kutoka mlimani. 29 Jumuiya yote walipofahamu kwamba Haruni amekufa, Waisraeli wote wakamwomboleza kwa siku thelathini.