21
Nchi ya Aradi yaangamizwa
Mfalme wa Aradi, aliyekuwa Mkanaani aliyeishi huko Negebu, aliposikia kwamba Waisraeli walikuwa wanakuja kwa njia ya Atharimu, aliwashambulia Waisraeli na kuwateka baadhi yao. Ndipo Israeli akaweka nadhiri hii kwa Mwenyezi Mungu: “Ikiwa utawatia watu hawa mikononi mwetu, tutaiangamiza kabisa miji yao.” Mwenyezi Mungu akasikiliza ombi la Waisraeli, naye akawapa ushindi juu ya Wakanaani. Wakawaangamiza kabisa na miji yao; hivyo mahali pale pakaitwa Horma*maana yake Maangamizi.
Nyoka wa shaba
Waisraeli wakasafiri kutoka Mlima Hori kupitia njia inayoelekea Bahari ya Shamuyaani Bahari Nyekundu au Bahari ya Mafunjo, kuizunguka Edomu. Lakini watu wakakosa uvumilivu njiani, wakamnung’unikia Mungu na Musa, wakisema, “Kwa nini umetupandisha kutoka Misri ili tufe jangwani? Hakuna mkate! Hakuna maji! Nasi tunachukia sana chakula hiki duni!”
Ndipo Mwenyezi Mungu akapeleka nyoka wenye sumu kati yao; wakawauma watu, nao Waisraeli wengi wakafa. Watu wakamjia Musa na kusema, “Tumetenda dhambi wakati tuliponena dhidi ya Mwenyezi Mungu na dhidi yako. Mwombe Mwenyezi Mungu ili atuondolee hawa nyoka.” Hivyo Musa akawaombea hao watu.
Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Tengeneza nyoka wa shaba na umweke juu ya mti; yeyote aliyeumwa na nyoka anaweza kumtazama na akaishi tena.” Kwa hiyo Musa akatengeneza nyoka wa shaba na kumweka juu ya mti. Kisha wakati mtu yeyote aliumwa na nyoka, naye akamtazama yule nyoka wa shaba, aliishi.
Safari kwenda Moabu
10 Waisraeli waliendelea na safari yao na wakapiga kambi huko Obothi. 11 Kisha wakaondoka Obothi na kupiga kambi huko Iye-Abarimu, katika jangwa linalotazamana na Moabu kuelekea mawio ya jua. 12 Kutoka hapo waliendelea mbele wakapiga kambi kwenye Bonde la Zeredi. 13 Wakasafiri kutoka hapo na kupiga kambi kando ya Mto Arnoni, ambao uko katika jangwa lililoenea hadi nchi ya Waamori. Mto Arnoni ni mpaka wa Moabu, kati ya Moabu na Waamori. 14 Ndiyo sababu Kitabu cha Vita vya Mwenyezi Mungu kinasema:
“Wahebu nchini Sufa, na mabonde,
Mto Arnoni, 15 na miteremko ya mabonde
inayofika hadi makazi ya Ari,
na kuegemea mpakani mwa Moabu.”
16 Kutoka hapo waliendelea mbele hadi kisima cha Beeri; kwenye kisima ambacho Mwenyezi Mungu alimwambia Musa, “Wakusanye watu pamoja, nami nitawapa maji.”
17 Kisha Israeli akaimba wimbo huu:
“Bubujika, ee kisima!
Imba kuhusu maji,
18 kuhusu kisima ambacho kilichimbwa na wakuu,
ambacho watu mashuhuri walikifukua,
watu mashuhuri wakiwa na fimbo za utawala na bakora.”
Kisha wakatoka jangwani kwenda Matana, 19 kutoka Matana wakafika Nahalieli, kutoka Nahalieli wakafika Bamothi, 20 na kutoka Bamothi wakafika kwenye bonde lililoko Moabu, mahali kilele cha Pisga kinatazamana na nyika.
Kushindwa kwa Sihoni na Ogu
(Kumbukumbu 2:26–3:11)
21 Israeli akawatuma wajumbe kumwambia Sihoni mfalme wa Waamori:
22 “Uturuhusu tupite katika nchi yako. Hatutageuka kando kwenda katika mashamba au mashamba ya mizabibu, ama kunywa maji kutoka kisima chochote. Tutasafiri kwenye njia kuu ya mfalme hata tutakapokuwa tumekwisha kupita katika nchi yako.”
23 Lakini Sihoni hakumruhusu Israeli apite katika nchi yake. Alilikutanisha jeshi lake lote, wakaondoka kwenda jangwani ili kupigana na Israeli. Alipofika huko Yahazi, akapigana na Israeli. 24 Hata hivyo, Israeli walimshinda kwa upanga na kuimiliki nchi yake kutoka Mto Arnoni hadi Mto Yaboki, lakini ni kufikia nchi ya Waamoni tu, kwa sababu mipaka yake ilikuwa imezungushwa ukuta. 25 Israeli wakaiteka miji yote ya Waamori na kuimiliki, pamoja na Heshboni na makazi yote yanayoizunguka. 26 Heshboni ulikuwa mji wa Sihoni mfalme wa Waamori, aliyekuwa amepigana dhidi ya mfalme wa Moabu aliyetangulia, na akawa amechukua ardhi yake yote hadi Mto Arnoni.
27 Ndiyo sababu watunga mashairi husema:
“Njoo Heshboni na ujengwe tena;
mji wa Sihoni na ufanywe upya.
 
28 “Moto uliwaka kutoka Heshboni,
mwali wa moto kutoka mji wa Sihoni.
Uliteketeza Ari ya Moabu,
raia wa mahali pa Arnoni palipoinuka.
29 Ole wako, ee Moabu!
Umeharibiwa, enyi watu wa Kemoshi!
Amewatoa wanawe kuwa wakimbizi,
na binti zake kama mateka
kwa Mfalme Sihoni wa Waamori.
 
30 “Lakini tumewashinda;
Heshboni umeharibiwa hadi Diboni.
Tumebomoa hadi kufikia Nofa,
ulioenea hadi Medeba.”
31 Kwa hiyo Israeli akaishi katika nchi ya Waamori.
32 Baada ya Musa kutuma wapelelezi kwenda mji wa Yazeri, Waisraeli waliteka makazi ya mji huo, na kuwafukuza Waamori walioishi huko. 33 Kisha wakageuka na kwenda katika njia inayoelekea Bashani, naye Ogu mfalme wa Bashani pamoja na jeshi lake lote wakatoka kupigana nao huko Edrei.
34 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Usimwogope Ogu, kwa sababu nimeshamkabidhi mikononi mwako, pamoja na jeshi lake lote na nchi yake. Mtendee kama ulivyomtendea Sihoni mfalme wa Waamori, ambaye alitawala huko Heshboni.”
35 Kwa hiyo wakamuua, pamoja na wanawe na jeshi lake lote, bila ya kumwacha hata mtu mmoja hai. Nao wakaimiliki nchi yake.

*21:3 maana yake Maangamizi

21:4 yaani Bahari Nyekundu au Bahari ya Mafunjo