3
Faida nyingine za hekima
Mwanangu, usisahau mafundisho yangu,
bali zitunze amri zangu moyoni mwako,
kwa kuwa zitakuongezea miaka mingi ya maisha yako
na kukuletea mafanikio.
 
Usiache kamwe upendo na uaminifu vitengane nawe;
vifunge shingoni mwako,
viandike katika ubao wa moyo wako.
Ndipo utapata kibali na jina zuri
mbele za Mungu na mwanadamu.
 
Mtumaini Mwenyezi Mungu kwa moyo wako wote
wala usizitegemee akili zako mwenyewe;
katika njia zako zote mkiri yeye,
naye atayanyoosha mapito yako.
 
Usiwe mwenye hekima machoni pako mwenyewe;
mche Mwenyezi Mungu ukajiepushe na uovu.
Hii itakuletea afya mwilini mwako,
na lishe kwenye mifupa yako.
 
Mheshimu Mwenyezi Mungu kwa mali yako
na kwa malimbuko ya mazao yako yote;
10 ndipo ghala zako zitakapojaa hadi kufurika,
viriba vyako vitafurika kwa mvinyo mpya.
 
11 Mwanangu, usidharau adhabu ya Mwenyezi Mungu
na usichukie maonyo yake,
12 kwa sababu Mwenyezi Mungu huwaadibisha wale anaowapenda,
kama vile baba afanyavyo
kwa mwana apendezwaye naye.
 
13 Heri mtu yule apataye hekima,
mtu yule apataye ufahamu,
14 kwa maana hekima ana faida kuliko fedha
na mapato yake ni bora kuliko ya dhahabu safi.
15 Hekima ana thamani kuliko marijani;
hakuna chochote unachokitamani
kinachoweza kulinganishwa naye.
16 Maisha marefu yako katika mkono wake wa kuume;
katika mkono wake wa kushoto
kuna utajiri na heshima.
17 Njia zake zinapendeza,
mapito yake yote ni amani.
18 Yeye ni mti wa uzima kwa wale wanaomkumbatia;
wale wamshikao watabarikiwa.
 
19 Kwa hekima Mwenyezi Mungu aliiweka misingi ya dunia,
kwa ufahamu aliziweka mbingu mahali pake;
20 kwa maarifa yake vilindi viligawanywa,
nayo mawingu yanadondosha umande.
 
21 Mwanangu, hifadhi maamuzi mema na busara,
usiache vitoke machoni pako;
22 ndipo vitakapokuwa uzima nafsini mwako
na pambo la neema shingoni mwako.
23 Kisha utaenda katika njia yako salama,
wala mguu wako hautajikwaa;
24 unapolala, hutaogopa;
unapolala, usingizi wako utakuwa mtamu.
 
25 Usiogope maafa ya ghafula
au maangamizi yanayowapata waovu,
26 kwa kuwa Mwenyezi Mungu atakuwa tumaini lako
na kuepusha mguu wako kunaswa katika mtego.
 
27 Usizuie wema kwa wale wanaostahili
ikiwa katika uwezo wako kutenda.
28 Usimwambie jirani yako,
“Njoo baadaye, nitakupa kesho”:
wakati wewe unacho kitu kile karibu nawe.
 
29 Usipange mabaya dhidi ya jirani yako,
anayeishi karibu nawe kwa uaminifu.
30 Usimshtaki mtu bila sababu,
wakati hajakudhuru kwa lolote.
 
31 Usimwonee wivu mtu mwenye jeuri
wala kuchagua njia yake yoyote,
32 kwa kuwa Mwenyezi Mungu humchukia mtu mpotovu,
lakini siri yake iko kwa mwenye haki.
 
33 Laana ya Mwenyezi Mungu i juu ya nyumba ya mwovu,
lakini yeye huibariki nyumba ya mwenye haki.
34 Huwadhihaki wale wanaodhihaki,
lakini huwapa neema wale wanyenyekevu na walioonewa.
35 Wenye hekima hurithi heshima,
bali huwaaibisha wapumbavu.