2
Faida za hekima
1 Mwanangu, kama utayakubali maneno yangu
na kuyaweka akiba maagizo yangu ndani mwako,
2 kutega sikio lako kwenye hekima
na kuweka moyo wako katika ufahamu,
3 na kama utaiita busara,
na kuita kwa sauti upate ufahamu,
4 na ukiitafuta kama fedha
na kuitafuta sana kama hazina iliyofichwa,
5 ndipo utakapoelewa kumcha Mwenyezi Mungu
na kupata maarifa ya Mungu.
6 Kwa maana Mwenyezi Mungu hutoa hekima,
na kinywani mwake hutoka maarifa na ufahamu.
7 Anahifadhi ushindi kwa ajili ya mwadilifu,
yeye ni ngao kwa wale wasio na lawama,
8 kwa kuwa hulinda mwenendo wa mwenye haki
na kuhifadhi njia ya waaminifu wake.
9 Ndipo utafahamu lipi lililo kweli na haki,
na sawa: yaani kila njia nzuri.
10 Kwa maana hekima itaingia moyoni mwako,
nayo maarifa yataifurahisha nafsi yako.
11 Busara itakuhifadhi
na ufahamu utakulinda.
12 Hekima itakuokoa kutoka njia za waovu,
kutoka kwa watu ambao maneno yao yamepotoka,
13 wale wanaoacha mapito ya unyoofu,
wakatembea katika njia za giza,
14 wale wanaopenda kutenda mabaya,
na kufurahia upotovu wa ubaya,
15 ambao mapito yao yamepotoka,
na ambao ni wapotovu katika njia zao.
16 Itakuokoa pia kutokana na mwanamke kahaba,
kutokana na mke aliyepotoka mwenye maneno
ya kushawishi kutenda ubaya,
17 aliyemwacha mwenzi wa ujana wake
na kupuuza agano alilofanya mbele ya Mungu.
18 Kwa maana nyumba yake huelekea kwenye kifo
na mapito yake kwenye roho za waliokufa.
19 Hakuna yeyote aendaye kwake akarudi,
au kufikia mapito ya uzima.
20 Hivyo utatembea katika njia za watu wema
na kushikamana na mapito ya wenye haki.
21 Kwa maana wanyofu wataishi katika nchi,
nao wasio na lawama watabakia ndani yake.
22 Bali waovu watakatiliwa mbali kutoka nchi,
nao wasio waaminifu watang’olewa kutoka humo.