Mithali
Utangulizi: Kusudi na kiini
1
Mithali za Sulemani mwana wa Daudi, mfalme wa Israeli:
Kwa kupata hekima na nidhamu;
kwa kufahamu maneno ya busara;
kwa kujipatia nidhamu na busara,
kufanya lililo sawa, haki na bila kupendelea;
huwapa busara wajinga*Neno la Kiebrania lililotafsiriwa mjinga (wingi wajinga) linamaanisha mtu anayeamini chochote, asiye na maadili, na mwenye roho ya kutenda uovu.,
maarifa na akili kwa vijana;
wenye hekima na wasikilize nao waongeze elimu yao,
wenye kupambanua na wapate mwongozo;
kwa kufahamu mithali na mifano,
misemo na vitendawili vya wenye hekima.
 
Kumcha Mwenyezi Mungu ni chanzo cha maarifa,
lakini wapumbavuNeno la Kiebrania lililotafsiriwa mpumbavu (wingi wapumbavu) linamaanisha mtu asiye na maadili. hudharau hekima na adabu.
Maelezo juu ya hekima na upumbavu
Onyo dhidi ya ushawishi wa rafiki waovu
Mwanangu, sikiliza mwongozo wa baba yako,
wala usiyaache mafundisho ya mama yako.
Hayo yatakuwa taji la maua la neema kichwani pako,
na mkufu wa kuipamba shingo yako.
 
10 Mwanangu, wenye dhambi wakikushawishi,
usikubaliane nao.
11 Wakisema, “Twende tufuatane;
tukamvizie mtu na kumwaga damu,
njoo tukavizie nafsi isiyo na hatia;
12 tuwameze wakiwa hai kama kaburiKaburi hapa maana yake ni Kuzimu; kwa Kiebrania ni Sheol.,
wakiwa wazima kama wale wanaotumbukia shimoni.
13 Tutapata aina zote za vitu vya thamani
na kujaza nyumba zetu kwa nyara.
14 Njoo ushirikiane nasi,
vitu vyote tutakavyopata tutagawana.”
15 Mwanangu, usiandamane nao.
Usiweke mguu wako katika njia zao,
16 kwa kuwa miguu yao hukimbilia kwenye dhambi,
ni wepesi kumwaga damu.
17 Tazama ni jinsi gani ilivyo kazi bure kutandaza wavu
wakati ndege wote wanakuona!
18 Watu hawa huvizia kumwaga damu yao wenyewe;
hujivizia tu wenyewe!
19 Huu ndio mwisho wa wote ambao wanajipatia mali kwa hila;
huuondoa uhai wa wale wenye mali.
Onyo dhidi ya kukataa hekima
20 Hekima huita kwa sauti kuu barabarani,
hupaza sauti yake kwenye viwanja vikubwa;
21 kwenye makutano ya barabara za mji
zenye makelele mengi hupaza sauti,
kwenye malango ya mji hutoa hotuba yake:
 
22 “Enyi wajinga, mtashikilia ujinga wenu hadi lini?
Hadi lini wenye mizaha watafurahia mizaha,
na wapumbavu kuchukia maarifa?
23 Kama mngekuwa mmeitikia karipio langu,
ningekuwa nimemimina roho yangu kwenu
na kuwafahamisha maneno yangu.
24 Lakini kwa kuwa mlinikataa nilipowaita
na hakuna yeyote aliyekubali
niliponyoosha mkono wangu,
25 kwa kuwa mliyapuuza mashauri yangu yote
na hamkukubali karipio langu,
26 mimi nami nitawacheka katika maafa yenu,
nitawadhihaki janga litakapowapata:
27 janga litakapowapata kama tufani,
maafa yatakapowazoa kama upepo wa kisulisuli,
dhiki na taabu zitakapowalemea.
 
28 “Ndipo watakaponiita lakini sitawajibu;
watanitafuta lakini hawatanipata.
29 Kwa kuwa walichukia maarifa,
wala hawakuchagua kumcha Mwenyezi Mungu,
30 kwa kuwa hawakukubali mashauri yangu,
na kukataa maonyo yangu,
31 watakula matunda ya njia zao,
na watashibishwa matunda ya hila zao.
32 Kwa kuwa ukaidi wa wajinga utawaua,
na kuridhika kwa wajinga kutawaangamiza.
33 Lakini yeyote anisikilizaye ataishi kwa usalama,
atatulia, bila kuwa na hofu ya madhara.”

*1:4 Neno la Kiebrania lililotafsiriwa mjinga (wingi wajinga) linamaanisha mtu anayeamini chochote, asiye na maadili, na mwenye roho ya kutenda uovu.

1:7 Neno la Kiebrania lililotafsiriwa mpumbavu (wingi wapumbavu) linamaanisha mtu asiye na maadili.

1:12 Kaburi hapa maana yake ni Kuzimu; kwa Kiebrania ni Sheol.