Zaburi 150
Msifuni Mwenyezi Mungu kwa ukuu wake
1 Msifuni Mwenyezi Mungu.*kwa Kiebrania ni Hallelu Yah; pia 150:6.
Msifuni Mungu katika patakatifu pake,
msifuni katika mbingu zake kuu.
2 Msifuni kwa matendo yake makuu,
msifuni kwa kadiri ya wingi wa ukuu wake.
3 Msifuni kwa mvumo wa tarumbeta,
msifuni kwa kinubi na zeze,
4 msifuni kwa matari na kucheza,
msifuni kwa kinanda cha nyuzi na filimbi,
5 msifuni kwa matoazi yaliayo,
msifuni kwa matoazi yavumayo sana.
6 Kila chenye pumzi na kimsifu Mwenyezi Mungu.
Msifuni Mwenyezi Mungu!