Zaburi 149
Wimbo wa kumsifu Mwenyezi Mungu kwa wema wake
1 Msifuni Mwenyezi Mungu.*kwa Kiebrania ni Hallelu Yah; pia 149:9.
Mwimbieni Mwenyezi Mungu wimbo mpya,
sifa zake katika kusanyiko la watakatifu.
2 Israeli na washangilie katika Muumba wao,
watu wa Sayuni na wafurahi katika Mfalme wao.
3 Na walisifu jina lake kwa kucheza
na wampigie muziki kwa matari na kinubi.
4 Kwa maana Mwenyezi Mungu anapendezwa na watu wake,
anawavika wanyenyekevu taji la wokovu.
5 Watakatifu washangilie katika heshima hii,
na waimbe kwa shangwe vitandani mwao.
6 Sifa za Mungu na ziwe vinywani mwao
na upanga ukatao kuwili mikononi mwao,
7 ili walipize mataifa kisasi
na adhabu juu ya mataifa,
8 wawafunge wafalme wao kwa minyororo,
wakuu wao kwa pingu za chuma,
9 ili kuwafanyia hukumu iliyoandikwa dhidi yao.
Huu ndio utukufu wa watakatifu wake wote.
Msifuni Mwenyezi Mungu.