Zaburi 148
Mwito kwa ulimwengu kumsifu Mwenyezi Mungu
Msifuni Mwenyezi Mungu.*kwa Kiebrania ni Hallelu Yah; pia 148:7, 14.
 
Msifuni Mwenyezi Mungu kutoka mbinguni,
msifuni juu vileleni.
Msifuni, enyi malaika wake wote,
msifuni yeye, enyi jeshi lake lote la mbinguni.
Msifuni yeye, enyi jua na mwezi,
msifuni yeye, enyi nyota zote zinazong’aa.
Msifuni yeye, enyi mbingu zilizo juu sana,
na ninyi maji juu ya anga.
Vilisifu jina la Mwenyezi Mungu
kwa maana aliamuru navyo vikaumbwa.
Aliviweka mahali pake milele na milele,
alitoa amri ambayo haibadiliki milele.
 
Msifuni Mwenyezi Mungu kutoka duniani,
ninyi wanyama wakubwa wa baharini,
na vilindi vyote vya bahari,
miali ya radi na mvua ya mawe, theluji na mawingu,
pepo za dhoruba zinazotimiza amri zake,
ninyi milima na vilima vyote,
miti ya matunda na mierezi yote,
10 wanyama pori na mifugo yote,
viumbe vidogo na ndege warukao,
11 wafalme wa dunia na mataifa yote,
ninyi wakuu na watawala wote wa dunia,
12 vijana wa kiume na wanawali,
wazee na watoto.
 
13 Wote na walisifu jina la Mwenyezi Mungu,
kwa maana jina lake pekee limetukuka,
utukufu wake uko juu ya nchi na mbingu.
14 Amewainulia watu wake pembepembe inawakilisha mwenye nguvu, yaani mfalme,
sifa ya watakatifu wake wote,
ya Israeli, watu walio karibu na moyo wake.
 
Msifuni Mwenyezi Mungu.

*Zaburi 148:1 kwa Kiebrania ni Hallelu Yah; pia 148:7, 14.

Zaburi 148:14 pembe inawakilisha mwenye nguvu, yaani mfalme