5
Onyo dhidi ya uzinzi
Mwanangu, sikiliza kwa makini hekima yangu,
sikiliza vizuri maneno yangu ya busara,
ili uweze kutunza busara
na midomo yako ihifadhi maarifa.
Kwa maana midomo ya mwanamke kahaba
hudondoza asali,
na maneno ya kinywa chake
ni laini kuliko mafuta;
lakini mwisho wake ni mchungu kama nyongo,
mkali kama upanga ukatao kuwili.
Miguu yake hushuka kuelekea kwenye kifo;
hatua zake huelekea moja kwa moja kaburini*Kaburini hapa maana yake ni Kuzimu; kwa Kiebrania ni Sheol..
Yeye hafikirii kuhusu njia ya uzima;
njia zake zimepotoka, lakini yeye hajui.
 
Sasa basi wanangu, nisikilizeni;
msiache ninalowaambia.
Njia zenu ziwe mbali naye,
msiende karibu na mlango wa nyumba yake,
usije ukapoteza heshima yako kwa wengine,
na miaka yako kwa aliye mkatili,
10 wageni wasije wakasherehekea utajiri wako,
na jitihada yako ikatajirisha
nyumba ya mwanaume mwingine.
11 Mwishoni mwa maisha yako utalia kwa uchungu,
wakati nyama na mwili wako vimechakaa.
12 Utasema, “Tazama jinsi gani nilivyochukia adhabu!
Tazama jinsi moyo wangu ulivyodharau maonyo!
13 Sikuwatii walimu wangu,
wala kuwasikiliza wakufunzi wangu.
14 Nimefika ukingoni mwa maangamizi
katika kusanyiko la watu wa Mungu.”
 
15 Kunywa maji kwenye kisima chako mwenyewe,
maji yanayotiririka kutoka kisima chako mwenyewe.
16 Je, chemchemi zako zifurike katika barabara za mji
na vijito vyako vya maji viwanjani?
17 Na viwe vyako mwenyewe,
kamwe visishirikishwe wageni.
18 Chemchemi yako na ibarikiwe
na umfurahie mke wa ujana wako.
19 Kulungu jike apendaye, kulungu mzuri:
matiti yake na yakutosheleze siku zote,
nawe utekwe daima na upendo wake.
20 Kwa nini mwanangu, utekwe na mwanamke kahaba?
Kwa nini ukumbatie kifua cha mke wa mwanaume mwingine?
 
21 Kwa maana njia za mtu ni wazi kabisa mbele za Mwenyezi Mungu,
naye huyapima mapito yake yote.
22 Matendo mabaya ya mtu mwovu humnasa yeye mwenyewe;
kamba za dhambi yake humkamata kwa nguvu.
23 Atakufa kwa kukosa nidhamu,
akipotoshwa kwa upumbavu wake mwenyewe.

*5:5 Kaburini hapa maana yake ni Kuzimu; kwa Kiebrania ni Sheol.