6
Maonyo dhidi ya upumbavu
Mwanangu, kama umekuwa mdhamini wa jirani yako,
ikiwa umeshikana mikono kwa kuweka ahadi
kwa ajili ya mwingine,
kama umetegwa na ulichosema,
umenaswa kwa maneno ya kinywa chako,
basi fanya hivi mwanangu, ili ujiweke huru,
kwa kuwa umeanguka mikononi mwa jirani yako:
Nenda ukajinyenyekeshe kwake;
msihi jirani yako!
Usiruhusu usingizi machoni pako,
usiruhusu kope zako zisinzie.
Jiweke huru, kama paa kutoka mkononi mwa mwindaji,
kama ndege kutoka mtego wa mwindaji.
 
Ewe mvivu, mwendee mchwa;
zitafakari njia zake ukapate hekima!
Kwa maana yeye hana msimamizi,
wala mwangalizi, au mtawala,
lakini hujiwekea akiba wakati wa kiangazi
na hukusanya chakula chake wakati wa mavuno.
 
Ewe mvivu, utalala hata lini?
Utaamka lini kutoka usingizi wako?
10 Kulala kidogo, kusinzia kidogo,
kukunja mikono kidogo upate kupumzika:
11 umaskini utakuja juu yako kama mnyang’anyi,
na kupungukiwa kutakujia kama mtu mwenye silaha.
 
12 Mtu mbaya sana na mlaghai,
ambaye huzungukazunguka
na maneno ya upotovu,
13 ambaye anakonyeza kwa jicho lake,
anayetoa ishara kwa miguu yake
na kuashiria kwa vidole vyake,
14 ambaye hupanga ubaya
kwa udanganyifu moyoni mwake:
daima huchochea fitina.
15 Kwa hiyo maafa yatamkumba ghafula;
ataangamizwa mara moja, pasipo msaada.
 
16 Kuna vitu sita anavyovichukia Mwenyezi Mungu,
naam, viko saba vilivyo chukizo kwake:
17 macho ya kiburi,
ulimi udanganyao,
mikono imwagayo damu isiyo na hatia,
18 moyo uwazao mipango miovu,
miguu iliyo myepesi kukimbilia uovu,
19 shahidi wa uongo ambaye humwaga uongo,
na mtu ambaye huchochea fitina kati ya ndugu.
Onyo dhidi ya uasherati
20 Mwanangu, zishike amri za baba yako,
wala usiyaache mafundisho ya mama yako.
21 Yafunge katika moyo wako daima,
yakaze kuizunguka shingo yako.
22 Unapotembea, yatakuongoza;
unapolala, yatakulinda;
unapoamka, yatazungumza nawe.
23 Kwa maana amri hii ni taa,
mafundisho haya ni mwanga,
na maonyo ya nidhamu
ni njia ya uzima,
24 yakikulinda na mwanamke aliyepotoka,
kutokana na maneno laini ya mwanamke aliyepotoka.
25 Moyo wako usitamani uzuri wake,
wala macho yake yasikuteke,
26 kwa maana kahaba atakufanya uwe maskini,
hata ukose kipande cha mkate,
naye mwanamke mzinzi huwinda maisha yako hasa.
27 Je, mtu aweza kuchotea moto kwenye paja lake
bila nguo zake kuungua?
28 Je, mtu aweza kutembea juu ya makaa ya moto
bila miguu yake kuungua?
29 Ndivyo alivyo mtu alalaye na mke wa mwanaume mwingine;
hakuna yeyote amgusaye huyo mwanamke ambaye hataadhibiwa.
 
30 Watu hawamdharau mwizi akiiba
ili kukidhi njaa yake akiwa na njaa.
31 Lakini akikamatwa, lazima alipe mara saba,
ingawa inamgharimu utajiri wote wa nyumba yake.
32 Lakini mwanaume aziniye na mwanamke hana akili kabisa;
yeyote afanyaye hivyo hujiangamiza mwenyewe.
33 Mapigo na aibu ni fungu lake
na aibu yake haitafutika kamwe;
34 kwa maana wivu huamsha ghadhabu ya mume,
naye hataonesha huruma alipizapo kisasi.
35 Hatakubali fidia yoyote;
atakataa malipo, hata yakiwa makubwa kiasi gani.