22
1 Heri kuchagua jina jema kuliko utajiri mwingi;
kuheshimiwa ni bora kuliko fedha au dhahabu.
2 Tajiri na maskini wanafanana kwa hili:
Mwenyezi Mungu ni Muumba wao wote.
3 Mtu mwenye busara huona hatari na kujificha,
bali mjinga huendelea mbele, naye hupata madhara.
4 Unyenyekevu na kumcha Mwenyezi Mungu
huleta utajiri, heshima na uzima.
5 Katika mapito ya waovu kuna miiba na mitego,
bali yeye ailindaye nafsi yake hukaa mbali nayo.
6 Mfundishe mtoto njia impasayo kuiendea,
naye hataiacha hata akiwa mzee.
7 Matajiri huwatawala maskini
naye akopaye ni mtumwa wa akopeshaye.
8 Yeye aupandaye uovu huvuna taabu,
nayo fimbo ya ghadhabu yake itaangamizwa.
9 Mtu mkarimu yeye mwenyewe atabarikiwa
kwa kuwa hushiriki chakula chake na maskini.
10 Mfukuze mwenye dhihaka,
na mvutano utatoweka;
ugomvi na matukano vitakoma.
11 Yeye apendaye moyo safi na yeye ambaye maneno yake ni ya neema,
mfalme atakuwa rafiki yake.
12 Macho ya Mwenyezi Mungu hulinda maarifa,
bali huyapinga maneno ya asiye mwaminifu.
13 Mvivu husema, “Yuko simba nje!”
au, “Nitauawa katika mitaa!”
14 Kinywa cha mwanamke kahaba ni shimo refu;
yeye aliye chini ya ghadhabu ya Mwenyezi Mungu
atatumbukia ndani yake.
15 Upumbavu umefungwa ndani ya moyo wa mtoto,
bali fimbo ya adhabu itaufukuzia mbali naye.
16 Yeye anayemdhulumu maskini ili kujiongezea mali,
naye anayempa tajiri zawadi, wote huwa maskini.
Misemo thelathini ya wenye hekima
Msemo 1
17 Tega sikio na usikie misemo ya wenye hekima,
elekeza moyo wako kwenye yale nifundishayo,
18 kwa maana inapendeza unapoyahifadhi moyoni mwako
na kuwa nayo yote tayari mdomoni mwako.
19 Ili tumaini lako liwe katika Mwenyezi Mungu,
hata wewe, ninakufundisha leo.
20 Je, sijakuandikia misemo thelathini,
misemo ya mashauri na maarifa,
21 kukufundisha maneno ya kweli na ya kuaminika,
ili uweze kutoa majibu sahihi
kwake yeye aliyekutuma?
Msemo 2
22 Usiwadhulumu maskini kwa sababu ni maskini,
wala kumdhulumu mhitaji mahakamani,
23 kwa sababu Mwenyezi Mungu atawatetea
naye atawateka hao waliowateka.
Msemo 3
24 Usifanye urafiki na mtu mwenye hasira ya haraka,
usishirikiane na yule aliye mwepesi kukasirika,
25 la sivyo utajifunza njia zake
na kujiingiza mwenyewe kwenye mtego.
Msemo 4
26 Usiwe mwenye kupeana mikono katika rehani,
au kuweka dhamana kwa ajili ya madeni;
27 ukikosa njia ya kulipa,
kitanda chako kitachukuliwa
ukiwa umekilalia.
Msemo 5
28 Usisogeze jiwe la mpaka wa zamani
lililowekwa na baba zako.
Msemo 6
29 Je, unamwona mtu stadi katika kazi yake?
Atahudumu mbele ya wafalme;
hatahudumu mbele ya watu duni.