23
Msemo 7 
  1 Uketipo kula chakula na mtawala,  
angalia vyema kile kilicho mbele yako,   
 2 na utie kisu kooni mwako  
kama ukiwa mlafi.   
 3 Usitamani vyakula vyake vitamu  
kwa kuwa chakula hicho ni cha hila.   
Msemo 8 
  4 Usijitaabishe ili kuupata utajiri,  
uwe na hekima kuonesha kujizuia.   
 5 Kufumba na kufumbua utajiri hutoweka,  
huwa kama umepata mabawa ghafula,  
ukaruka na kutoweka angani kama tai.   
Msemo 9 
  6 Usile chakula cha mtu mchoyo,  
usitamani vyakula vyake vitamu,   
 7 kwa maana yeye ni aina ya mtu  
ambaye kila mara anafikiri kuhusu gharama.  
Anakuambia, “Kula na kunywa,”  
lakini moyo wake hauko pamoja nawe.   
 8 Utatapika kile kidogo ulichokula,  
nawe utakuwa umepoteza bure  
maneno yako ya kumsifu.   
Msemo 10 
  9 Usizungumze na mpumbavu,  
kwa maana atadhihaki hekima ya maneno yako.   
Msemo 11 
  10 Usisogeze jiwe la mpaka wa zamani  
wala kunyemelea kwenye mashamba ya yatima,   
 11 kwa kuwa Mtetezi wao ni mwenye nguvu,  
atawatetea dhidi yako.   
Msemo 12 
  12 Elekeza moyo wako kwenye mafundisho  
na masikio yako kwenye maneno ya maarifa.   
Msemo 13 
  13 Usimnyime mtoto adhabu,  
ukimwadhibu kwa fimbo, hatakufa.   
 14 Mwadhibu kwa fimbo  
na kuiokoa nafsi yake kutoka mautini*mautini maana yake ni Kuzimu.   
Msemo 14 
  15 Mwanangu, kama moyo wako una hekima,  
basi moyo wangu utafurahi,   
 16 utu wangu wa ndani utafurahi,  
wakati midomo yako  
itakapozungumza lililo sawa.   
Msemo 15 
  17 Usiuruhusu moyo wako kuwaonea wivu wenye dhambi,  
bali kila mara uwe na bidii katika kumcha Mwenyezi Mungu.   
 18 Hakika kuna tumaini la baadaye kwa ajili yako,  
nalo tarajio lako halitakatiliwa mbali.   
Msemo 16 
  19 Sikiliza, mwanangu na uwe na hekima,  
weka moyo wako kwenye njia iliyo sawa.   
 20 Usiwe miongoni mwa wanywao mvinyo,  
au wale walao nyama kwa pupa,   
 21 kwa maana walevi na walafi huwa maskini,  
nako kusinzia huwavika matambara.   
Msemo 17 
  22 Msikilize baba yako, aliyekuzaa,  
wala usimdharau mama yako atakapokuwa mzee.   
 23 Nunua kweli wala usiiuze,  
pata hekima, adabu na ufahamu.   
 24 Baba wa mwenye haki ana furaha kubwa,  
naye aliye na mwana mwenye hekima humfurahia.   
 25 Baba yako na mama yako na wafurahi,  
mama aliyekuzaa na ashangilie!   
Msemo 18 
  26 Mwanangu, nipe moyo wako,  
macho yako na yafuate njia zangu,   
 27 kwa maana kahaba ni shimo refu  
na mwanamke mpotovu ni kisima chembamba.   
 28 Kama mnyang’anyi, hungojea akivizia,  
naye huzidisha wasio waaminifu miongoni mwa wanaume.   
Msemo 19 
  29 Ni nani mwenye ole?  
Ni nani mwenye huzuni?  
Ni nani mwenye ugomvi?  
Ni nani mwenye malalamiko?  
Ni nani aliye na majeraha yasiyo na sababu?  
Ni nani mwenye macho mekundu?   
 30 Ni hao wanaokaa sana kwenye mvinyo,  
hao wanaoenda kuonja mabakuli ya mvinyo uliochanganywa.   
 31 Usiukodolee macho mvinyo ukiwa mwekundu,  
unapometameta kwenye bilauri,  
unaposhuka taratibu!   
 32 Mwishowe huuma kama nyoka  
na kutia sumu yake kama nyoka mwenye sumu.   
 33 Macho yako yataona mambo mageni,  
na moyo wako kuwazia mambo yaliyopotoka.   
 34 Utakuwa kama alalaye baharini,  
alalaye juu ya kamba ya merikebu.   
 35 Utasema, “Wamenipiga lakini sikuumia!  
Wamenichapa, lakini sisikii!  
Nitaamka lini  
ili nikanywe tena?”