27
 1 Usijisifu kwa ajili ya kesho,  
kwa kuwa hujui ni nini kitakachozaliwa kwa siku moja.   
 2 Mwache mwingine akusifu,  
wala si kinywa chako mwenyewe;  
mtu mwingine afanye hivyo  
na si midomo yako mwenyewe.   
 3 Jiwe ni zito na mchanga ni mzigo,  
lakini kukasirishwa na mpumbavu ni kuzito kuliko vyote viwili.   
 4 Hasira ni ukatili na ghadhabu kali ni gharika,  
lakini ni nani awezaye kusimama mbele ya wivu?   
 5 Afadhali karipio la wazi  
kuliko upendo uliofichika.   
 6 Majeraha kutoka kwa rafiki yaonesha uaminifu,  
lakini adui huzidisha busu.   
 7 Yeye aliyeshiba huchukia kabisa asali,  
bali kwa mwenye njaa  
hata kile kilicho kichungu  
kwake ni kitamu.   
 8 Kama ndege atangatangavyo mbali na kiota chake,  
ndivyo alivyo mtu atangatangaye  
mbali na nyumbani mwake.   
 9 Manukato na uvumba huleta furaha moyoni,  
nao uzuri wa rafiki huchipuka  
katika ushauri wake wa uaminifu.   
 10 Usimwache rafiki yako wala rafiki wa baba yako,  
tena usiende nyumbani mwa ndugu yako  
wakati umepatwa na maafa.  
Bora jirani wa karibu  
kuliko ndugu aliye mbali.   
 11 Mwanangu, uwe na hekima,  
nawe ulete furaha moyoni mwangu,  
ndipo nitakapoweza kumjibu yeyote  
anitendaye kwa dharau.   
 12 Mtu mwenye busara huona hatari na kujificha,  
bali mjinga huendelea mbele, naye hupata madhara.   
 13 Chukua vazi la yule awekaye dhamana  
kwa ajili ya mgeni;  
lishikilie liwe dhamana  
kwa ajili ya mgeni.   
 14 Mtu akimbariki jirani yake kwa sauti kuu  
asubuhi na mapema,  
itahesabiwa kuwa ni laana.   
 15 Mke mgomvi ni kama  
matone yasiyokoma siku ya mvua.   
 16 Kumzuia ni kama kuuzuia upepo,  
au kukamata mafuta kwa kiganja cha mkono.   
 17 Kama vile chuma kinoavyo chuma,  
ndivyo mtu amnoavyo mwenzake.   
 18 Yeye autunzaye mtini atakula tunda lake,  
naye amtunzaye bwana wake ataheshimiwa.   
 19 Kama uso uonekanavyo kwenye maji,  
ndivyo hivyo moyo wa mtu humwonesha alivyo.   
 20 Kuzimu*Kuzimu kwa Kiebrania ni Sheol, yaani Shimo lisilo na mwisho. na Uharibifu†kwa Kiebrania ni Abadon havishibi,  
wala macho ya mwanadamu hayashibi.   
 21 Kalibu husafisha fedha na tanuru husafisha dhahabu,  
bali mtu hupimwa kwa sifa anazopewa na watu.   
 22 Hata ukimtwanga mpumbavu kwenye kinu,  
ukimtwanga kama nafaka kwa mchi,  
hutauondoa upumbavu wake.   
 23 Hakikisha kuwa unajua hali ya makundi yako ya kondoo na mbuzi;  
angalia ng’ombe wako kwa makini.   
 24 Kwa kuwa utajiri haudumu milele,  
nalo taji halidumu vizazi vyote.   
 25 Wakati majani makavu yameondolewa  
na mapya yamechipua,  
nayo majani toka milimani yamekusanywa,   
 26 wana-kondoo watakupatia mavazi  
na mbuzi thamani ya shamba.   
 27 Utakuwa na maziwa mengi ya mbuzi  
kukulisha wewe na jamaa yako,  
na kuwalisha wajakazi wako.