Misemo ya Mfalme Lemueli
31
1 Misemo ya Mfalme Lemueli, usia wa mama yake aliyomfundisha:
2 “Sikiliza, ee mwanangu! Sikiliza, ee mwana wa tumbo langu!
Sikiliza, ee mwana wa nadhiri zangu!*au Ewe uliye jibu la maombi yangu.
3 Usitumie nguvu zako kwa wanawake,
uhodari wako kwa wale wanaowaharibu wafalme.
4 “Ee Lemueli, haifai wafalme,
haifai wafalme kunywa mvinyo,
haifai watawala kutamani sana kileo,
5 wasije wakanywa na kusahau vile sheria inavyoamuru
na kuwanyima haki zao wote waliodhulumiwa.
6 Wape kileo wale wanaoangamia,
mvinyo wale walio na uchungu,
7 Wanywe na kusahau umaskini wao
na wasikumbuke taabu yao tena.
8 “Sema kwa ajili ya wale wasioweza kujisemea,
kwa ajili ya haki za wote walioachwa ukiwa.
9 Sema na uamue kwa haki,
tetea haki za maskini na wahitaji.”
Maneno ya mwisho: Mke mwenye sifa nzuri
10 †Mithali 31:10-31 imetungwa kila mstari ukianzia na herufi ya alfabeti ya Kiebrania zikifuatana tangu Aleph (A) hadi Taw (T); zote ni 22. Mke mwenye sifa nzuri, ni nani awezaye kumpata?
Yeye ni wa thamani sana kuliko marijani.
11 Mume wake anamwamini kikamilifu,
wala hakosi kitu chochote cha thamani.
12 Humtendea mumewe mema, wala si mabaya,
siku zote za maisha yake.
13 Huchagua sufu na kitani,
naye hufanya kazi kwa mikono yenye bidii.
14 Yeye ni kama meli za biashara,
akileta chakula chake kutoka mbali.
15 Yeye huamka kukiwa bado giza,
naye huwapa jamaa yake chakula
na wajakazi wake mafungu yao.
16 Huangalia shamba na kulinunua;
kutokana na mapato yake hupanda shamba la mizabibu.
17 Hufanya kazi zake kwa nguvu,
mikono yake ina nguvu kwa ajili ya kazi zake.
18 Huona kwamba biashara yake ina faida,
wala taa yake haizimiki usiku.
19 Huweka mikono yake kwenye pia,
navyo vidole vyake hushikilia kijiti chenye uzi.
20 Huwanyooshea maskini mikono yake
na kuwakunjulia wahitaji vitanga vyake.
21 Theluji inaposhuka, hana hofu
kwa ajili ya watu wa nyumbani mwake,
kwa maana wote wamevikwa
nguo za kutia joto.
22 Yeye hutengeneza mazulia ya urembo
ya kufunika kitanda chake,
huvaa kitani safi na urujuani.
23 Mume wake anaheshimiwa kwenye lango la mji,
aketipo miongoni mwa wazee wa nchi.
24 Hutengeneza mavazi ya kitani na kuyauza,
naye huwauzia wafanyabiashara mishipi.
25 Amevikwa nguvu na heshima,
anaweza kucheka bila kuwa na hofu kwa siku zijazo.
26 Huzungumza kwa hekima,
na mafundisho ya kuaminika yapo ulimini mwake.
27 Huangalia mambo ya nyumbani mwake
wala hali chakula cha uvivu.
28 Watoto wake huamka na kumwita aliyebarikiwa,
mumewe pia humsifu, akisema:
29 “Wanawake wengi hufanya vitu vyenye sifa nzuri,
lakini wewe umewapita wote.”
30 Kujipamba ili kuvutia ni udanganyifu,
na uzuri unapita upesi;
bali mwanamke anayemcha Mwenyezi Mungu atasifiwa.
31 Mpe thawabu anayostahili,
nazo kazi zake na zimletee sifa kwenye lango la mji.