Misemo ya Aguri
30
Misemo ya Aguri mwana wa Yake; usia:
Huyu mtu alimwambia Ithieli,
naam, kwa Ithieli na Ukali:
 
“Mimi ni mjinga kuliko wanadamu wote;
sina ufahamu wa kibinadamu.
Sijajifunza hekima,
wala sina maarifa ya kumjua yeye Aliye Mtakatifu.
Ni nani ameshapanda mbinguni na kushuka?
Ni nani ameshakusanya upepo
kwenye vitanga vya mikono yake?
Ni nani ameshafungia maji kwenye nguo yake?
Ni nani ameimarisha miisho yote ya dunia?
Jina lake ni nani, na mwanawe anaitwa nani?
Niambie kama unajua!
 
“Kila neno la Mungu ni kamilifu;
yeye ni ngao kwa wale wanaomkimbilia.
Usiongeze kwenye maneno yake,
ama atakukemea na kukuthibitisha kuwa mwongo.
 
“Ninakuomba vitu viwili, Ee Mwenyezi Mungu;
usininyime kabla sijafa:
Uutenge mbali nami udanganyifu na uongo;
usinipe umaskini wala utajiri,
bali unipe chakula cha kunitosha kila siku.
Nisije nikawa na vingi vya kuzidi nikakukana
na kusema, ‘Mwenyezi Mungu ni nani?’
Au nisije nikawa maskini nikaiba,
nami nikaliaibisha jina la Mungu wangu.
 
10 “Usimchongee mtumishi kwa bwana wake,
asije akakulaani, ukapatilizwa kwalo.
 
11 “Kuna wanaowalaani baba zao,
wala hawawabariki mama zao;
12 ambao ni safi machoni pao wenyewe
lakini hawakuoshwa uchafu wao;
13 ambao daima macho yao ni ya kiburi,
na kutazama kwao ni kwa dharau;
14 ambao meno yao ni panga
na mataya yao yamewekwa visu
ili kuwaangamiza maskini katika nchi,
na wahitaji kutoka miongoni mwa wanadamu.
 
15 “Mruba anao binti wawili.
Wao hulia daima: ‘Nipe! Nipe!’
 
“Kuna vitu vitatu visivyotosheka kamwe,
naam, viko vinne visivyosema, ‘Yatosha!’:
16 Ni kaburi, tumbo lisilozaa,
nchi isiyoshiba maji kamwe,
na moto, usiosema kamwe, ‘Yatosha!’
 
17 “Jicho lile limdhihakilo baba,
lile linalodharau kumtii mama,
litang’olewa na kunguru wa bondeni,
litaliwa na tai.
 
18 “Kuna vitu vitatu vinavyonishangaza sana,
naam, vinne nisivyovielewa:
19 Ni mwendo wa tai katika anga,
mwendo wa nyoka juu ya mwamba,
mwendo wa meli katika maji makuu ya bahari,
nao mwendo wa mtu pamoja na msichana.
 
20 “Huu ndio mwendo wa mwanamke mzinzi,
hula akapangusa kinywa chake na kusema,
‘Sikufanya chochote kibaya.’
 
21 “Kwa mambo matatu nchi hutetemeka,
naam, kwa mambo manne haiwezi kuvumilia:
22 mtumwa anapokuwa mfalme,
mpumbavu anaposhiba chakula,
23 mwanamke asiyependwa anapoolewa,
na mjakazi anapochukua nafasi ya bibi yake.
 
24 “Vitu vinne duniani vilivyo vidogo,
lakini vina akili nyingi sana:
25 Mchwa ni viumbe wenye nguvu ndogo,
hata hivyo hujiwekea akiba ya chakula chao wakati wa kiangazi.
26 Pelele ni viumbe vyenye uwezo mdogo,
hata hivyo hujitengenezea nyumba zao kwenye miamba.
27 Nzige hawana mfalme,
hata hivyo huenda pamoja vikosi vikosi.
28 Mjusi anaweza kushikwa kwa mkono,
hata hivyo huonekana katika majumba ya wafalme.
 
29 “Viko vitu vitatu ambavyo vinapendeza katika mwendo wao,
naam, vinne ambavyo hutembea kwa mwendo wa madaha:
30 simba, mwenye nguvu miongoni mwa wanyama,
wala haogopi chochote;
31 jogoo atembeaye kwa maringo,
pia beberu,
na mfalme jeshi lake linapomzunguka.
 
32 “Ikiwa umefanya upumbavu na ukajitukuza mwenyewe,
au kama umepanga mabaya,
basi funika mdomo wako kwa mkono wako.
33 Kwa maana kama vile kusukasuka maziwa hutoa siagi,
na pia kule kufinya pua hutoa damu,
kadhalika kuchochea hasira huleta ugomvi.”