29
Anayekaza shingo baada ya maonyo mengi,
ataangamia ghafula, na kamwe hatapona.
 
Wenye haki wanapostawi, watu hufurahi;
waovu watawalapo, watu hulia kwa huzuni.
 
Mtu apendaye hekima huleta furaha kwa baba yake,
bali aambatanaye na makahaba hutapanya mali yake.
 
Kwa haki mfalme huipa nchi uthabiti,
bali mfalme aliye na tamaa ya rushwa huiangamiza.
 
Yeyote amsifuye jirani yake isivyostahili,
anautandaza wavu kuitega miguu yake.
 
Mwovu hutegwa na dhambi yake mwenyewe,
bali mwenye haki hushangilia na kufurahi.
 
Mwenye haki hujali haki kwa ajili ya maskini,
bali mwovu hajishughulishi na hilo.
 
Wanaodhihaki huuchochea mji,
bali wenye hekima huzuia hasira.
 
Mwenye hekima akienda mahakamani na mpumbavu,
mpumbavu hukasirika na kudhihaki, wala hakuna amani.
 
10 Watu wanaomwaga damu humchukia mtu mwadilifu,
na hutafuta kumuua mtu mnyofu.
 
11 Mpumbavu huonesha hasira yake yote,
bali mwenye hekima hujizuia.
 
12 Mtawala akisikiliza uongo,
maafisa wake wote huwa waovu.
 
13 Mtu maskini na mtu mdhalimu wanafanana kwa jambo hili:
Mwenyezi Mungu hutia nuru macho yao wote wawili.
 
14 Kama mfalme akiwaamua maskini kwa haki,
kiti chake kitakuwa thabiti daima.
 
15 Fimbo ya maonyo hutia hekima,
bali mtoto asiyeonywa humwaibisha mama yake.
 
16 Waovu wanapostawi,
dhambi huongezeka pia;
lakini wenye haki wataliona anguko lao.
 
17 Mkanye mwanao, naye atakupa amani;
atakuletea furaha unayotamani.
 
18 Mahali pasipo na ufunuo, watu huacha kujizuia,
bali ana heri mtu yule anayeitii sheria.
 
19 Mtumishi hawezi kuonywa kwa maneno matupu,
hata akielewa, hataitikia.
 
20 Je, unamwona mtu azungumzaye kwa haraka?
Kuna matumaini zaidi kwa mpumbavu kuliko yeye.
 
21 Kama mtu akimdekeza mtumishi wake tangu ujanani,
atamletea sikitiko mwishoni.
 
22 Mtu mwenye hasira huchochea ugomvi,
naye mtu mwenye hasira ya haraka
hutenda dhambi nyingi.
 
23 Kiburi cha mtu humshusha,
bali mtu mwenye roho ya unyenyekevu
hupata heshima.
 
24 Anayekubaliana na mwizi ni adui wa nafsi yake mwenyewe;
huapishwa lakini hathubutu kushuhudia.
 
25 Kuwaogopa watu huwa ni mtego,
bali yeyote amtumainiaye Mwenyezi Mungu atakuwa salama.
 
26 Wengi hutafuta kusikilizwa na mtawala,
bali mtu hupata haki kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
 
27 Mwenye haki huwachukia sana wasio waaminifu;
waovu huwachukia sana wenye haki.