Zaburi 8
Utukufu wa Mwenyezi Mungu na heshima ya mwanadamu 
 Kwa mwimbishaji. Mtindo wa gitithi. Zaburi ya Daudi. 
  1 Ee Mwenyezi Mungu, Bwana wetu,  
tazama jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani kote!  
Umeuweka utukufu wako  
juu ya mbingu.   
 2 Midomoni mwa watoto wachanga na wanaonyonya  
umeamuru sifa,  
kwa sababu ya watesi wako,  
kumnyamazisha adui na mlipiza kisasi.   
 3 Nikiziangalia mbingu zako,  
kazi ya vidole vyako,  
mwezi na nyota,  
ulizoziratibisha,   
 4 mwanadamu ni kitu gani hata unamfikiria,  
binadamu ni nani hata unamjali?   
 5 Umemfanya chini kidogo kuliko viumbe wa mbinguni,  
ukamvika taji la utukufu na heshima.   
 6 Umemfanya mtawala juu ya kazi za mikono yako;  
umeweka vitu vyote chini ya miguu yake.   
 7 Mifugo na makundi yote pia,  
naam, na wanyama wa kondeni,   
 8 ndege wa angani na samaki wa baharini,  
naam, kila kinachoogelea katika njia za bahari.   
 9 Ee Mwenyezi Mungu, Bwana wetu,  
tazama jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani kote!