*Zaburi hii ikiunganishwa na ya 10 zimetungwa kila beti likianzia na herufi ya alfabeti ya Kiebrania zikifuatana tangu Aleph (A) hadi Taw (T); zote ni 22.
Zaburi 9
Shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya haki yake
Kwa mwimbishaji. Mtindo wa muth-labeni.Muth-labeni ni mtajo mmojawapo katika lugha za muziki. Zaburi ya Daudi.
Ee Mwenyezi Mungu, nitakutukuza kwa moyo wangu wote,
nitayasimulia matendo yako yote ya ajabu.
Nitafurahi na kushangilia ndani yako.
Nitaliimbia sifa jina lako, Ewe Uliye Juu Sana.
 
Adui zangu wamerudi nyuma,
wamejikwaa na kuangamia mbele zako.
Kwa maana umetetea haki yangu na msimamo wangu;
umeketi kwenye kiti chako cha enzi,
ukihukumu kwa haki.
Umekemea mataifa na kuwaangamiza waovu;
umeyafuta majina yao milele na milele.
Uharibifu usiokoma umempata adui,
umeing’oa miji yao;
hata kumbukumbu lao limetoweka.
 
Mwenyezi Mungu anatawala milele,
ameweka kiti chake cha enzi apate kuhukumu.
Mungu atahukumu ulimwengu kwa haki,
atatawala mataifa kwa haki.
Mwenyezi Mungu ni kimbilio la wanaodhulumiwa,
ni ngome imara wakati wa shida.
10 Wote wanaolijua jina lako watakutumaini wewe,
kwa maana wewe Mwenyezi Mungu,
hujawaacha kamwe wanaokutafuta.
 
11 Mwimbieni Mwenyezi Mungu sifa, amefanywa mtawala Sayuni,
tangazeni miongoni mwa mataifa, yale aliyoyatenda.
12 Kwa maana yeye anayelipiza kisasi cha damu hukumbuka,
hapuuzi kilio cha wanaoonewa.
 
13 Ee Mwenyezi Mungu, tazama jinsi walivyo wengi
adui zangu wanaonitesa!
Nihurumie, uniinue kutoka malango ya mauti,
14 ili niweze kutangaza sifa zako
katika malango ya Binti Sayuni,
na huko niushangilie wokovu wako.
15 Mataifa wameanguka kwenye shimo walilolichimba,
miguu yao imenaswa kwenye wavu waliouficha.
16 Mwenyezi Mungu anajulikana kwa haki yake,
waovu wamenaswa katika kazi za mikono yao.
 
17 Waovu wataishia KuzimuKuzimu kwa Kiebrania ni Sheol, yaani Shimo lisilo na mwisho.,
naam, mataifa yote wanaomsahau Mungu.
18 Lakini mhitaji hatasahaulika siku zote,
wala matumaini ya walioonewa hayatapotea.
 
19 Ee Mwenyezi Mungu, inuka, usimwache binadamu ashinde.
Mataifa na yahukumiwe mbele zako.
20 Ee Mwenyezi Mungu, wapige kwa hofu,
mataifa na yajue kuwa wao ni watu tu.

*^ Zaburi hii ikiunganishwa na ya 10 zimetungwa kila beti likianzia na herufi ya alfabeti ya Kiebrania zikifuatana tangu Aleph (A) hadi Taw (T); zote ni 22.

^ Muth-labeni ni mtajo mmojawapo katika lugha za muziki.

Zaburi 9:17 Kuzimu kwa Kiebrania ni Sheol, yaani Shimo lisilo na mwisho.