Zaburi 11
Kumtumaini Mwenyezi Mungu
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.
Kwa Mwenyezi Mungu ninakimbilia.
Unawezaje basi kuniambia:
“Ruka kama ndege utorokee kwenye mlima wako.
Hebu tazama, waovu wanapinda nyuta zao;
wanaweka mishale kwenye nyuzi zake
ili wakiwa gizani, wawapige
walio wanyofu wa moyo.
Wakati misingi imeharibiwa,
mwenye haki anaweza kufanya nini?”
 
Mwenyezi Mungu yuko ndani ya Hekalu lake takatifu;
Mwenyezi Mungu yuko kwenye kiti chake cha enzi mbinguni.
Huwaangalia wana wa watu,
macho yake yanawachunguza.
Mwenyezi Mungu huwachunguza wenye haki,
lakini nafsi yake inachukia waovu
na wale wanaopenda mapigano.
Atawanyeshea waovu makaa ya moto mkali
na kiberiti kinachowaka;
upepo wenye joto kali ndio fungu lao.
 
Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye haki,
yeye hupenda haki.
Wanyofu watauona uso wake.